Utangulizi :
Jarida hili la Mheshimiwa Chacha Zakayo Wangwe lina sehemu
tatu. Sehemu ya kwanza litaweka bayana na kufafanua sababu
za mimi kuchafuliwa kisiasa na baadhai ya viongozi wa ngazi
za juu za Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, na
sehemu ya pili itaonyesha baadhi ya maswali ya msingi
niliyopata kuuliza Bungeni na majibu yake na sehemu ya tatu
itakuwa na michango mbalimbali niliyopata kuchangia kwa muda
wa miezi miaka miwili na nusu.
Lengo hasa la Jarida hili ni kumwelewesha Mtanzania na
hususan MWANADEMOKRASIA juu ya tuhuma zilizoelekezwa kwangu
kwa lengo la kunichafua kisiasa huku viongozi wa CHADEMA
wakidai kukisafisha chama jambo ambalo si kweli na ni
kampeni chafu zilizoandaliwa na baadhi ya viongozi wa Chama
na kuwarubuni wajumbe 31 wasiokuwa wanademokrasia na
kunipaka matope ya siasa zao zisizo na hata chembe ya
Demokrasia.
Nasema hivi nikijua wazi kwamba, CHADEMA kama chama
kinaendeshwa kwa katiba na kwa wakati huo huo kikiwa
kinaendeshwa kidikteta na kauli za NDIYO MZEE.
Ninajua wazi kwamba, viongozi wa sasa wa chama changu
wanatofautiana sana na viongozi wa mwanzo wakati CHADEMA
ikianzishwa kwani wanatofautiana kiitikadi, kisera na hata
kimtazamo.
Kwa mfano, mzee Mtei alikuwa akikieneza chama hasa vijijini
miaka ya 95 kwa kutumia magari chakavu na alifanikiwa kwa
kiasi kikubwa kuwashawishi wananchi na wakijua kuwa CHADEMA
si chama cha mjini, na hapa ndipo mwanzo wa CHADEMA kuwa
Chama Tawala kule Tarime hadi sasa. Ila katika uongozi huu
wa kizazi kipya basi kila kitu kinaenda kwa kauli za
Mheshimiwa Mwenyekiti kasema na matumizi mabaya huku
ufisadi ukikitafuna chama kwa matumizi hewa na kwa kigezo
kuwa eti wanajilipa madeni ya Kampeni.
Nililia sana juu ya matumizi ya helkopta katika kampeni
lakini nikaanza kuonekana kuwa mini ni mbaya. Binafsi
sikuona sababu za Chama kutumia helkopta ilhali bado
wanachama wa vijijini hawakijui chama wala sera zake huku
viongozi wa wilaya na mikoa wakishindwa hata kutoa durufu
(photocopy) za viepeperushi vya chama kwa kukosa ruzuku. Hii
si sawa.
SEHEMU YA KWANZA
Sababu za baadhi ya Viongozi wa CHADEMA kuamua kunichafua
kisiasa.
Baadhi ya Kampeni za chini chini dhidi yangu, tarehe 28 na
29 Juni 2008 katika kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika
Dodoma ambacho kiluhudhuriwa na wajumbe 31 kiliridhia mimi
kuondolewa kwenye wadhifa niliokuwa nao ndani ya chama kama
Makamu Mwenyekiti kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na
kutuhumiwa kuwa navujisha siri za chama kwa CCM. Binafsi
kwangu kama mwanasiasa wa kiwango cha juu ni pigo kubwa sana
kisiasa kuchafuliwa na watu 31 tu ndani ya chama.
Ninachokiamini hapa ni kwamba, kutokana na msimamo wangu wa
siku nyingi hata kabla sijawa makamu mwenyekiti CHADEMA,
ndiyo sababu rasmi ya kupigiwa kampeni na baadaye kura za
kutokuwa na imani na mimi kwa taarifa nilizo nazo ni kwamba
anaandaliwa Dr. Slaa kushika nafasi hiyo. Hapa ikumbukwe
kuwa Mke wa Dr. Slaa ni diwani kupitia CCM hivyo kuna
uwezekano wa sera za chama zikavuja kupitia Mama huyu katika
njia mbalimbali.
Ofisi ya Katibu Mkuu (Ofisi ya Slaa) ndiyo ya kwanza
kunituhumu kuwa nawaingilia majukumu yao katika suala zima
la matumizi mabovu ya fedha za ruzuku ya chama. Chama hupata
zaidi ya milioni 60 kila mwezi. Ni fedha nyingi sana
kukijenga chama kama zikipata mipango mizuri na kuachana na
matumizi mabovu kama matumizi ya helkopta kwenye kampeni
kama ilivyotokea kwenye chaguzi zetu pamoja na baadhiya
viongozi kudai kuwa wanajilipa madeni waliokikopesha chama
wakati wa kampeni za 2005.
Mhe. Philemon Ndesamburo Mbunge wa Moshi Mjini inadaiwa kuwa
anakidai chama milioni 100 alizokopesha wakati wa kampeni za
2005.
Mhe. Philemon Ndesamburo Mbunge wa Moshi Mjini inadaiwa kuwa
anakidai chama milioni 100 alizokopesha wakati wa kampeni za
2005, Freeman Mboe ambaye hadi sasa ni Mwenyekiti wa chama
changu katika ngazi ya Taifa naye kwa taarifa nilizo nazo ni
kwamba kila mwezi hulipwa shilingi milioni 10 ili kufidia
fedha anazodai kukikopesha chama ambazo ni zaidi ya milioni
500 katika kampeni hizo hizo na hadi sasa anaendelea kukidai
chama mamilioni ya shilingi.
Mimi nilipoonyesha wasiwasi juu ya madeni haya yasiyoisha,
ikaundwa tume ya kampeni za kutokuwa na imani na mimi.
Binafsi sijui kama viongozi wanaojiita makini kama kina Dr.
Slaa na Kabwe Zitto wangeweza kuusimamia ufisadi mkubwa kama
huu ndani ya chama huku wakiwa mstari wa mbele kuwafichua
mafisadi Serikalini.
Au ni kawaida kuwa Mganga hajigangi?
CHADEMA kuna ufisadi wa aina nyingi sana kuanzia uchapaji
bendera hadi manunuzi ya vifaa vya chama!
Katika ofisi ya Vijana nako kunanuka ufisadi kwani ni vijana
wachache sana ambao hupata nafasi ya kwenda nje ilhali
mikoani nako kuna vijana wanaohitaji kujifunza. Ofisi hii
ina watu maalumu wa kwenda kwenye Semina na Matamasha
mbalimbali. Na watu hao hupangwa na John Mnyika.
Pamoja na hayo, Kurugenzi hii inayoendeshwa na John Mnyika
imekuwa ikifanya hesabu za Mbili mara Mbili toa nne.
Nakumbuka matamasha mbalimbali yaliyowahi kuratibiwa na
Kurugenzi hii kwa kutumia fedha za chama yamekuwa hayana
maslahi yoyote kwa chama
.labda kwake mwenyewe kwani
itakumbukwa kwamba Kurugenzi ilizindua mfuko ulioitwa
Tumaini jipya Septemba 16, 2007 katika hafla ya wafanyakazi
vijana na akaunti ya Tumaini Jipya 01810301 NBC
ilifunguliwa.
Jumla ya shilingi milioni 6,176,500 zimekusanywa na shilingi
milioni 6,064,300 zimetumika kwa shughuli mbalimbali za
vijana ikiwemo gharama za hafla yenyewe. Hafla nyingine kama
hiyo ilifanyika Arusha.
Hafla hii ilifanyika tarehe 29 Machi, 2008 The New Polygon
Triangel Arusha na kuhudhuriwa na washiriki 67 mgeni rasmi
akiwa Mhe. Mzee Edwin Mtei. Jumla ya shilingi milioni
2,300,700 zilikusanywa na shilingi milioni 1,885,000.
Zimetumika kwa shughuli mbalimbali za vijana ikiwemo gharama
za hafla yenyewe. Sasa najiuliza, kulikua na mantiki gani ya
kutumia fedha za chama kiasi cha shilingi 6,064,300 na
kukusanya shilingi 6,176,500/=? Ni faida ya shilingi ngapi
ilipatikana kama ameamua kukiingiza chama katika kufanya
biashara ya matamasha?
Jingine, tangu nimekuwa mbunge Chadema na Baadaye Makamu
Mwenyekiti sijawahi kuandaliwa safari za kibunge ama za
kukiwakilisha chama ilhali kuna watu wasio na uwezo kiakili,
kifikra na hata nafasi za uongozi lakini waliandaliwa safari
za nje.
Chama kimefikia hatua ya kuwakilishwa kimataifa na watu
wasio na vigezo kwa ajili ya utawala mbovu! Siandiki haya
kwa kuwa nimeondolewa katika uongozi, hapana! Hizi ni
harakati zangu za muda mrefu juu ya utawala bora. Tazama,
wafuatao wamewahi kusafiri katika mataifa mbalimbali kwa
shughuli mbalimbali kukiwakilisha chama. Mhe. Suzan Lymo
(Mb. Viti maalumu) Cape Towan, Afrika Kusini kwa Mkutano wa
Interparliamentary Union. Susan pia amesafiri kwenda USA kwa
High Level meeting ya HIV/AIDs mwezi June, 2008.
Mhe. Zitto Kabwe, (Mb) alisafiri kwenda Berlin mara mbili
Mhe. Zitto pia alisafiri kwenda Marekeani kwa wiki 3 kwa
mwaliko wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani pamoja na
Wabunge vijana toka dunia nzima ambako walipata nafasi ya
kutembelea majimbo mbalimbali ya Marekani.
Mhe. Mhonga Said (Mb Viti maalum) alisafiri kwenda
Burundi kwa Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu. Mhe. Dr. Slaa
amesafiri kwenda Johannesburg, Windhoek na Manzini Swaziland
kwa vikao vya Kamati na Bunge la SADC. Dr. Slaa ni Makamu
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya InterParliamentary
Cooperation Committee ya Bunge la SADC. Mhe. Maulida Komu
(Mb. Viti Maalumu)
alisafiri kwenda Nairobi na pia Finland. Mhe. Ndesamburo
(Mb) alisafiri kwenda Australia kama Commissioner wa Bunge.
Wafuatao walisafiri kichama; Mhe. Mhonga Said (Mb Viti
Maalum), Maulida Komu (Mb Viti Maalum), Suzan Kiwanga
(Afisa Msaifizi Idara ya Uchaguzi na Kampeni) na John Mnyika
Mkurugenzi wa Idara ya Vijana) walisafiri kwenda Norway na
Sweden. Anthony Komu (Mkurugenzi wa Fedha na Utawala)
alisafiri kwenda Norway kwa mwaliko wa Centre Party, Mhe.
Balozi Ngaiza (Mjumbe wa heshma wa kamati kuu wa kuteuliwa
na Mwenyekiti), John Mnyika (Mkurugenzi katika Ofisi ya
Vijana), John Mrema (Afisa katika Kurugenzi ya Halmashauri
na Bunge), walisafiri kwenda Windhoek Namibia kwa Mkutano wa
Dua, na Mhe. Kimesera (Katibu Mtendaji wa kuteuliwa na
Mwenyekiti), Suzan Lymo (Mb) Viti maalum, na John Mrema
walisafiri kwenda Kampala, Uganda kwa Mkutano wa Dua.
Ndugu Regia Mtema (Afisa katika Kurugenzi ya Vijana)
alisafiri kwenda Malawi kwa Mkutano wa NIMD.
Mama Naomi Kaihula (Mkurugenzi katika Idara ya Wanawake) na
Regia Mtema walisafiri kwenda Finland kwa mwaliko wa Shirika
la Demo Finland. Johna Mrema, Msafiri Mtemelwa na Happiness
Mwaipopo (Sina hakika kama ni Mwanachama) walisafiri kwenda
London/Uingereza kwa mwaliko wa Conservative Party/WFD
wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Mhe. Benson Kigaila
(Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo) alienda Zimbabwe
katika uchaguzi uliofanyika 27 June, 2008 kupita Ofisi ya
Msajili wa Vyama.
Suala la ukabila ni jambo ambalo halihitaji kupingwa kwani
asilimia karibu 85 ya viongozi wa CHADEMA wametoka katika
mikoa ya Kilimanjaro na Arusha pamoja na kwamba baada ya
mimi kulishupalia jambo hili wameanza kubadilisha majina.
Wapo wanachama kama mimi ambao nao wakipewa nafasi za
uongozi ndani ya chama hiki watafanya vizuri zaidi ya hawa
na wengine ambao ni Jobless! Pengine niweke wazi hapa kuwa,
mimi ni kiongozi shupavu nisiye kuwa na hata chembe ya woga
katika kuteta na kusimamia haki za mwanachama wa CHADEMA
tena nisiyependa siasa za kisanii.
Ukweli huu ndio uliowafanya kina Mbowe, Slaa kuwa mstari wa
mbele katika kupiga kampeni na baadaye kura ya kutokuwa na
Imani na mimi. Binafsi naamini katika chama cha siasa mtu
muhimu ni Mwanachama na si Mwenyekiti au Katibu. Hapa mimi
siandiki maneneo haya kukufanya udhani kuwa nataka kuwa
kinganganizi kwenye wadhifa niliovuliwa, la hasha bali
napenda upate picha halilisi ya uendeshwaji wa Siasa ya
CHADEMA na kisha uweze kugundua uhalisia wa mgogoro ulivyo.
Viongozi wa CHADEMA Makao Makuu wameningoa kutoka katika
wadhifa niliokuwa nao kwa sababu zao binafsi na si sababu za
chama kama chama, na wanajitahidi kuzunguka mikoani kwa siri
kuendelea kunichafua kisiasa kuwa sifai. Kweli sifai kwa
wafuja ruzuku ya chama, kweli sifai kwa mafisadi ndani ya
chama ila nafaa kukiendesha chama katika ngazi ya taifa
katika nafasi yoyote na siku zote.
Nafaa kwa sababu nimefukuzwa kwa kusema ukweli hivyo
nikageuka mwiba kati kati ya majipu, nikatolewa. Ndiyo,
nafaa kwa sababu siko tayari kufanya kazi na watu waliozoea
kukaa ofisini kama mafaili! Nafaa kwa sababu mimi ni
mpambanaji, kamanda shujaa niliye tayari kuwajibishwa kwa
ajili ya kuwatetea WANADEMOKRASIA hususan WANACHADEMA nchi
nzima.
Kuliendesha Taifa kama Tanzania hakuhitaji siasa za kisanii,
fitina, na chuki. Kinachotakiwa ni nani abadilike alete
mabadiliko katika siasa ili aweze kukabidhiwa dola na alete
mabadiliko. Wananchi wamechoshwa na siasa zetu ndio maana
wanaziita siasa za kisanii. Wanahitaji mabadiliko. CHADEMA
maana yake ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo, lakini huku
wanakoelekea tayari uongozi wa Mbowe na Slaa wameiondosha
Demokrasia kwa kunitoa katika wadhifa wa umakamu Mwenyekiti
kwa kupiga kampeni ndogo ya wajumbe 31 tu! Tena huku
wakinituhumu kuwa navujisha siri za chama!!. Dhahama kama
hii siwezi kuivumilia hata kidogo na ni wazi kuwa hata
wanachama wetu hawajafurahishwa na jambo hili.
Mimi nilipokuwa kwenye ngazi hiyo ndipo fedha zilipoanza
kupelekwa mikoani kwa viwango halali, ndipo ukarabati wa
Makao Makuu ulifanyika. Niweke wazi hapa kuwa, jambo
lililonifanya niandike jarida hili si kuwashawishi Freeman
Mbowe na Slaa kunirudisha kwenye nafasi waliyonitoa kwa
matusi, la hasha! Lengo ni kuweka wazi kwa wanachama wajue
aina ya uongozi uliopo Makao Makuu ya Chama. Kama ni suala
la mimi kurudi katika nafasi hiyo ni mimi mwenyewe nikiamua
na kwa kutumia Demokrasia.
Ikumbukwe kuwa, Freeman ndiye aliyesema kuwa hataki kufanya
kazi na mimi na kutokana na UMANGIMEZA na Kauli za NDIYO
MZEE akapata kuungwa mkono na wajumbe 31 tu! Baada tu ya
mimi kutangazwa kuwa nimetolewa kwenye wadhifa niliokuwa nao
nilipata simu nyingi sana za wanachama na hata baadhi ya
watendaji Makao Makuu wakiniambia kuwa kama Mbowe hayuko
tayari kufanya kazi na mimi, wao bado wananihitaji katika
Uongozi Taifa.
Kuna mila ya kichagga kuwa, katika eneo la kazi/biashara,
ukimuona anayekusababisha ukose maslahi Fulani unatakiwa
kumuondoa kwa gharama yoyote! Na hili ndilo lililojiri
kwangu na mwenyekiti wangu.
Aluta Continue
..
Wangwe Chacha Zakayo,
Mbunge wa Tarime-CHADEMA
KAULI YANGU KWA MSOMAJI
Awali ya yote, nasikitika sana kwa maamuzi yaliyofikiwa na
wajumbe 31 kule Dodoma aidha, kwa hasira, chuki au majungu
na kuamua kuniondoa katika wadhifa niliokuwa nao wa Makamu
Mwenyekiti Tanzania Bara wakitumia kivuli cha Katiba ya
Chama.
Pili nimezidi kuumia zaidi pale nilipotuhumiwa kuwa eti
navujisha siri za Chama kwa CCM! Niliwapa siku Arobaini (40)
kuwaza kuthibitisha juu ya tuhuma hizo lakini wameshindwa
hadi leo! Inamaanisha kuwa walitumia tuhuma hizo ili kunitoa
kati yao ili nisiendelee kutetea ahadi za wanachama wa
CHADEMA na nisiendelee kupinga ubadhirifu wa fedha za chama.
Pengine kutokana na hasira, chuki na majungu hayo hayo
wakaamua kuzidi kunichafualia jina katika mkutano
uliofanyika Tanga kwa kunisema kuwa mimi ni mhuni. Hapa
sintakuwa na huruma wala urafiki na yeyote aliye mstari wa
mbele kunichafua kisiasa nitahakikisha nawafungulia mashtaka
na waweze kuthibitisha tuhuma hizo. Mpendwa msomaji, pamoja
na hayo ni vyema ukumbuke kuwa, uongozi wa CHADEMA Taifa
umeshindwa kukieneza chama hadi vijijini. Ni kwa ajili ya
majungu haya haya!.
Kimsingi, tusiposhikamana kwa sauti moja, lengo moja na kwa
msimamo, ni dhahiri kuwa chama cha mapinduzi kitaendelea
kushika Dola hadi Ukamilifu wa Dahari! Chama kisipokuwa
madhubuti hakitaweza kushika Dola hakiwezi kuaminika na
Wananchi. CHADEMA tufike mahali tugeuke, tujue tuna lengo la
kuiongoza Tanzania na si vinginevyo. Badala ya kulewa katika
kuwafichua mafisadi. Tumejisahau!.
Naamini kuwa, nguvu za umma ndiyo nguvu inayoweza kuleta
mabadiliko ya kweli.Naamini kuwa, katika chama chochote cha
siasa, mwanachama ndiye bora kuliko Kiongozi.Naamini kuwa
msingi bora wa chama hujengwa na watu makini.
Naamini pia baada ya kusoma Jarida hili ukiwa kama
mwanachama au Mwanademokrasia utaungana nami katika kupiga
vita UFISADI ndani ya CHADEMA
