1. Nimesoma andiko la Prof. Anna Tibaijuka juu ya hali tete Mkoa wa Kagera tunapojikuta tuko mwisho kwa vigezo vya kiuchumi hususan GDP.
2. Ningeomba atupe namba ya mkoa katika quality of life/happiness index kutokana na household survey. Ni kwa kutazama vyote viwili ndio tunaweza kusema kama tupoteze imani kabisa au tupendekeze mikakati ya kutupandisha chati katika kipindi cha miaka 5 hadi 10.
3. Huko nyuma nimeshandika sababu ambazo zinaelezea kuanguka kwa uchumi wa Mkoa wa West Lake/ Kagera katika miaka 60 kutoka wa 2 hadi wa 26; kama mtu ambaye ameona haya yote yakitokea.
4. Sababu ya kwanza ni demographic na nategemea Prof. aielezee hii point. Kupiga hatua katika elimu bila kukua kwa viwanda au estate agriculture kuweza kuwaajiri wasomi wake huko kumesabaisha brain drain ya watu wetu walio kwenye productive age kuajiriwa nje ya mkoa wetu na kwa hiyo kuchangia kuendeleza mikoa mingine ya Tanzania.
Tumeacha watoto na wazee ambao mchango wao katika uzalishaji ni haba wakibaki kulima mashamba ya migomba na mibuni iliyopandwa miaka 100 iliyopia. Wachache walio na uwezo wa kuzalisha wamezembea kuhamia mahala ambako wangejiongeza kiuzalishaji na kuendekeza land fragmentation; mojawapo ya sababu ikiwa kuishi kwa invisible earnings kutoka kwenye mishahara ya jamaa zao walioko nje ya mkoa.
5. Sababu nyingine ni historical disruptions za
(a) vita ya Tanzania na Uganda au na Idi Amin. Wengi huiona kama athari katika miaka ya 1978 mpaka 1980;
wanasahau kwamba uhusiano na Uganda ulififia kwa miaka zaidi ya 10 kuanzia 1971. Mathalan uwekezaji wa Serikali/NAFCO katika shamba la Ngano Kibanda,Murongo,lililokuwa mechanised ukiwa na matrekta hadi combine harvestor, ulisitishwa kwa kuhofia Amin asipate target ya kupiga mabomu. Prof. atafiti agundue kwa nini Serikali haikuendelea nao baada ya vita.
(b) Pili,ni Vita ya Kiuchumi ya Sokoine ambapo tofauti na mikoa mingine, wafanyabiashara wote muhimu katika mkoa waliswekwa ndani, na malori zaidi ya 400 yalikamatwa na kuteketea Kaitaba Stadium. Prof. na wasomi wengine watupe kiwango cha economic disruption iliyotokana na vita hiyo na fidia ambayo haikutolewa. Sheria maalumu kutaifisha malori yasiyozidi miaka 5 ambayo ilihusu Kagera tu ilikuwa ya kibaguzi na fidia ilikuwa kiduchu,ambayo kutokana na inflation,hawakuweza kununua lori nyingine. Nilishangaa sifa alizopewa Nsa Kaisi miaka ya karibuni, bila watu kukumbuka ukatili(sadism) alioufanyia mkoa wa Kagera.Serikali na CCM walipaswa kutengeneza Marshall Plan ya kuwekeza katika mkoa kuurudisha kwenye maendeleo iliyokuwa nayo.
(c) Mathalan,mwaka 1967 serikali ilipotaifisha mabenki na Viwanda, kampuni ya West Lake Bus Service iliyokuwa na mabasi ya routes zote mkoani ilifilisiwa na wamiliki wa Kihindi na kukomba hela yote na kumwacha Mzee Daniel K Rwiza, mtu aliyedhamini watu kujenga nyumba za bati Karagwe, kubaki masikini. Shida zote za usafiri mkoani tangu hapo mpaka miaka ya 1990s zinaanzia hapo,na ziliathiri mkoa sana.
Nadhani nimempa Prof. Anna na wapenda maendeleo wa Mkoa wa Kagera nafasi ya kuanzia. Sijataja athari za kuhujumu BCU,kuleta Mamlaka ya Kahawa na kuanzisha BCU(1990) Ltd na KDCU bila mali za Union zote kupatikana nyingine zikichukuliwa na RTC na CCM kuchukua kiwanja cha Union ambako kumejengwa makao makuu ya CCM ambayo ni gofu ambalo halikwisha na halitaisha.
Wakati yote hayo yanatokea viwanda vinajengwa Mbeya,Mwanza, Moshi,Arusha tulikuwa na viongozi wazawa. Nani tumlaumu?