Imeandikwa na Shadrack Sagati;
Tarehe: 1st October 2009
Habari Leo
WAZIRI Mkuu Mstaafu Jaji , Joseph Warioba, amesema, Katibu wa Uchumi na Fedha wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Amos Makala, ni mbaguzi na amemtaka aache tabia hiyo.
Warioba amesema, Makala anaendeleza makundi katika chama hicho na anajipendekeza kwa Rais Kikwete.
Amemtaka Makala atambue kuwa yeye ni kiongozi wa chama kitaifa hivyo asifikiri umri wake mdogo unaweza kumpa kinga ya kutoa kauli zisizo za busara.
Sisi tulipewa madaraka tukiwa wadogo na ukishakuwa kiongozi ni lazima uwe na busara hivyo umri mdogo sio sababu.
Warioba amesema, kauli za Makala zinadhihirisha asivyowathamini wana CCM ambao hawakumuunga mkono Rais, Jakaya Kikwete, wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais kupitia chama hicho.
Kiongozi huyo alisema jana kuwa, kauli ya Makala kwamba yeye (Warioba) alikuwa anamuunga mkono Dk Salim inaonyesha kiongozi huyo alivyodhamiria kuendeleza makundi na kuleta mpasuko ndani ya chama.
Warioba amesema, kauli ya Makala pia ina maana kwamba,wana CCM ambao hawakumuunga mkono Rais Kikwete wakati wa mchakato huo hawana nafasi ya kutoa maoni yao kuhusu uendeshaji wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Amesema, ni hatari kama Makala haoni matatizo yaliyopo, na amemtuhumu kuwa kiongozi huyo wa CCM anajipendekeza kwa Rais Kikwete aonekane ni mtetezi wake.
Huyu ni mwanamtandao kwa hiyo haheshimu mwana CCM mwingine ambaye hakumuunga mkono Rais Kikwete
wana mtandao ni tatizo na ndio wanaoendeleza mpasuko katika chama chetu, amesema Warioba.
Makala ni kiongozi wangu ndani ya chama kwa nafasi yake namheshimu lakini anaonekana ni mbaguzi wa wana CCM
huyu kwa nafasi yake hapaswi kuendeleza malumbano ya mtandao wakati sisi tunataka mtandao uondoke. amesema kiongozi huyo ambaye amewahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, Tanzania.
Warioba amesema, Makala alipaswa kujibu hoja alizozitoa kuhusu matatizo yaliyopo kwenye jamii kama ya udini, matabaka, ukabila na chama kukumbatia utajiri na si kumtukana kwamba ni mchochezi na ni mfuasi wa Dk Salim Ahmed Salim.
Amesema, wakati anazungumza juzi na wanahabari, hakuishambulia Serikali wala Rais Jakaya Kikwete, ila alielezea mambo anayoona ni tatizo na yanaweza hatarisha umoja wa kitaifa.
Makala badala ya kujibu hoja hizo, alichofanya ni kunitukana kuwa mimi ni mchonganishi
nataka Makala aniambie ninaposema kuna udini ni uongo? Ninaposema kuna tabaka la matajiri na masikini ni uongo?
Nilitaka ajibu hoja hizo na sio akwepe na kukimbilia kunishambulia kuwa nalaumu kwa vile nilimuunga mkono Dk Salim (Salim Ahmed) wakati wa mchakato, alisema Warioba.
Alikiri kuwa wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM alikuwa anamuunga mkono Dk Salim, lakini baada ya Rais Kikwete kushinda alishiriki kumfanyia kampeni mgombea wa CCM.
Mimi sio mtendaji ni mshauri tu. Ninaposema umoja wetu uko hatarini unataka nifanye nini zaidi ya kusema?" amesema wakati anajibu tuhuma kwamba amekuwa akisema tu bila kutoa suluhisho.
Ninaposema tumeanza kukumbatia udini, utajiri, ukabila, unataka nifanye nini zaidi ya kusema na watendaji walioko madarakani ndio wanapaswa kutafuta njia ya kuondoa tatizo, alisema kiongozi huyo.
Amesema, wakati anatoa maoni yake alikuwa anawaeleza watanzania wote na wala si wana CCM tu hivyo amemtaka kamtaka Makala aache kuwa mbaguzi, na azifanyie kazi hoja ambazo aliziainisha kwenye mazungumzo yake.
Sijui anamchukia Dk Salim maana hii si mara ya kwanza kusema, kuna wakati Butiku (Joseph) alitoa maoni yake huyu Makala akasema analaumu kwa vile ni mfuasi wa Dk Salim, alisema.
Makala katika taarifa yake alimlaumu Jaji Warioba kuwa ni sehemu ya matatizo yanayoendelea nchini kwa kuwa analaumu bila kuonyesha njia ya kuyatatua.