Hili ndilo tatizo kubwa tulilonalo - sio CCM, si CDM wala si CUF.
Katika mfumo wa vyama vingi, suala la muungano na hata idadi ya serikali, lisingepaswa kuwa ni suala la sera ya chama cha siasa. Hayo ni mambo ya msingi ambayo yanahitaji mustakabli na maridhiano ya kitaifa bila kujali wenye vyama na wasio na vyama wala ni chama gani cha siasa kipo madarakani. Tukiendelea kuacha jambo hili likawa ni sera ya vyama nchi yetu itayumba sana.
Leo CCM ipo madarakani inataka nchi iwe na serikali mbili na hawaamini katika muungano wa hiari, kesho CDM ikiwa madarakani itataka tuwe na serikali tatu, wanaamini katika muungano wa hiari, keshokutwa wakiingia CUF watataka muungano wa mkataba, wanaamini katika muungano/mkataba wa hiari.
Kama wazalendo, tunapswa kuweka sera na maslahi ya vyama ama makundi yetu kando linapokuja suala la msingi la kitaifa, hasa KATIBA. Warioba mwishoni mwa hotuba yake alisema maneno mazuri sana namna tume yake ilivyofikia maamuzi wakati wa kutengeneza rasimu ya katiba. Alisema wajumbe wa tume walikuwa na misimamo yao ambayo mingine ilikuwa inakinzana. Lakini waliweza kuweka misimamo hiyo kando na kutanguliza maslahi ya taifa. Alisema, wajumbe wote walikubaliana na kila kifungu katika rasimu ya katiba. Na la muhimu sana ni kuwa, katika kufikia maamuzi yao, hakuna hata mara moja ambapo walifanya maamuzi kwa kupiga kura. Hili ni la muhimu sana kuzingatiwa katika bunge hili la katiba. Kulikuwa na mjadala wa kura ya siri au ya dhahiri - haukuisha! Wabunge/wajumbe wajaribu kutafuta muafaka wa kitaifa badala ya kufikiria sera za vyama vyao.
Tume ya Warioba imefanya kazi nzuri sana. Bunge la katiba lisiharibu kazi hiyo nzuri. Hata kama rasimu itafanyiwa marekebisho makubwa, lakini cha muhimu iwe ni kwa maslahi ya taifa/watanzania na si vyama vya siasa. Kwa sehemu kubwa, wajumbe wa Zanzibar ndio wenye nafasi kubwa ya kuamua muelekeo.