diana chumbikino
JF-Expert Member
- May 29, 2018
- 428
- 368
WASANII wa fani tofauti na waandishi wa habari Alhamisi wiki hii watafanya ziara kutembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa SGR unaotekelezwa na Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC). Mratibu wa safari hiyo, msanii wa lamu Steve Mengele 'Nyerere' ameupongeza uongozi wa TRC kwa kutambua mchango wa wasanii katika jamii na kuwapa fursa.
Nyerere amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa kufanikisha safari hiyo itayojumuisha waimbaji wa muziki wa bendi, bongo eva, taarabu, singeli, waigizaji wa lamu, bongo movie, komedi, wachezaji wa zamani wa mpira wa miguu na waandishi wa habari wa vyombo wakiwemo wa mitandao ya kijamii.
Wasanii na waandishi wa habari wameelezwa jijini Dar es Salaam kuwa, safari hiyo itaanza saa moja asubuhi kwa treni ya TRC kutoka eneo la Kamata jijini Dar es Salaam na kupitia maeneo yote ambayo mradi huo unatekelezwa. Wakati wa safari wahandisi wa reli watakuwa wakitoa maelezo kuhusu ujenzi wa mradi huo mkubwa.
Nyerere pia amewaeleza wasanii kuwa, kuna mikopo inayotolewa kwa wasanii kupitia Halmashauri za mkoa wa Dar es Salaam kutekeleza sera ya Serikali inayoziagiza mamlaka hizo kutenga asilimia 10 ya mapato yao ya ndani kwa ajili ya mikopo ya vijana, walemavu na wanawake. “Mkuu wa Mkoa Paul Makonda anakaribisha maombi ya mkopo kwa wote wanaohitaji mikopo aliyohaidi wakati wa mkutano wa wasanii wa maigizo waimbaji wa muziki wa bendi, bongo eva, taarab, singeli, waigizaji wa lamu, bongo movie, komedi , wachezaji wa zamani wa mpira wa miguu na waandishi wa habari nchini kuweza kupata mkopo huo utakaowezesha kufanya kazi kwa weledi na kukuza kipato kwa tasnia zote nchini.” amesema Nyerere.
Kaimu Mkuu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano TRC Jamila Mbarouk amesema safari hiyo ni fursa kwa wasanii na waandishi wa habari kwenda kuona mradi wa ujenzi wa SGR unavyotekelezwa. Mbarouk amesema Safari hiyo itasaidia kutangaza utalii uliopo ndani hasa kuwepo kwa treni hiyo ya umeme ikiwa na uwezo wa kubeba mizigo ya tani elfu 10 huku spidi yake ikiwa ni kilomita 160 kwa saa.
“Shirika la reli (TRC) limewapa kipaumbele wasanii ,wacheza mpira, ma MC ,waimbaji, wachekeshaji, waigizaji wa lamu na wengine ambao wanaweza kuwa mabalozi wazuri katika kuutangazia umma kuhusu mradi huo wa treni mpya ya umeme itakayotoka Dar es Salaam -Morogoro hadi Dodoma ” amesema Mbarouk. Amesema, reli hiyo inajengwa kwa fedha za Watanzania kutokana na kodi. Ametoa mwito kwa wafanyabiashara kulipa kodi kwani mradi huo ukikamilika utasaidia kukuza uchumi pia kwa wafanyabiashara kwa kusarisha bidhaa zao na mizigo kwa haraka zaidi.