Wasifu wa Abdilatif Abdalla

Wasifu wa Abdilatif Abdalla

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
1545575481454.png


WASIFU WA SHEIKH ABDILATIF ABDALLA
Umetolewa na Prof. David P. B. Massamba tarehe 13 Aprili, 2012, kabla ya kumkaribisha Abdilatif Abdalla kutoa Mhadhara Maalumu (“Nafasi ya Wasanii Katika Ukombozi wa Bara la Afrika”) kwenye Tamasha la Nne la Kitaaluma la Mwalimu Julius Nyerere, lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam 12-13 Aprili, 2012

Labda nianze kwa kusema kwamba matumizi yangu ya neno ‘Sheikh’ kumhusu Abdilatif Abdalla ni stahiki yake. Hii ni kwa sababu kwa wenyeji wengi wa jamii za pwani neno sheikh lina maana kama tatu hivi. Maana ya kwanza ni ‘mtu yeyote aliye na elimu ya dini ya Kiislamu, ambaye aghalabu huwafundisha wenzi wake’. Maana ya pili ni ‘mzee yeyote katika jamii anayeheshimika sana kutokana na busara zake na mashauri ya welekea anayotoa kwa watu wengine’. Maana ya tatu ni ‘jina la kuitana watu wa rika moja walio marafiki na wenye uhusiano wa karibu sana’. Matumizi yangu ya neno Sheikh kuhusu Abdilatif Abdalla yanaangukia katika maana hii ya pili na ya tatu, na nitaeleza kwa nini.

Mimi na Abdilatif Abdalla tumefahamiana kwa takribani miaka arobaini. Hivyo, kwa kiasi fulani ninaweza kusema ninamfahamu kidogo, kuliko pengine wengi wetu hapa. Kwanza namfahamu tukiwa vijana, na kisha namfahamu tukiwa wazee. Kwa wale ambao wangependa kujua, mimi na Abdilatif Abdalla tulianza kazi pamoja mnamo mwezi Julai, 1972 – hapa hapa Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, katika Taasisi ambayo wakati huo ilijulikana kama Chuo cha Uchunguzi wa Lugha ya Kiswahili. Baadaye chuo hicho kikawa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, na sasa ni Taasisi ya Taaluma za Kiswahili.

Naomba sasa nitumie fursa hii kusema yale kidogo sana ninayojua kuhusu Abdilatif Abdalla. Sheikh Abdilatif Abdalla alizaliwa Kuze, Mombasa, tarehe 14 Aprili, 1946. Alianza masomo yake katika shule ya msingi ya Faza (pia ikijulikana kama Rasini), eneo ambalo liko katika upwa wa kaskazini kabisa mwa Kenya, karibu na Lamu. Wakati huo alikuwa akilelewa na babu yake (mjombake mamake), Ahmad Basheikh, ambaye alikuwa mwalimu. Hatimaye babu yake alipata uhamisho kwenda Takaungu, ambako ndiko Abdilatif alikomalizia shule yake ya msingi (wenyewe wanaita KPE = Kenya Primary Education).

Baada ya kumaliza mtihani wa KPE Abdilatif aliambiwa hakufaulu mtihani huo! Nathubutu kusema kwa kutumia yale maneno ya ‘Bwana MUSA’ kwamba huo haukuwa mzimu pekee bali palikuwa panyigwa! Hisia zangu ni kwamba watu walikwishanusanusa harufu ya mtu huyu na kumwona ni mtu ambaye hakuwa katika uelekeo wao. Ninasema hivi kwa sababi sisi tuliyefanya naye kazi hapa tunajua wazi kwamba si mtu ambaye angeshindwa mtihani huo! Pengine hapa yafaa nitoe maelezo kidogo kwa nini nimesema hivyo.

Tuanze kwa kujiuliza: huyu Abdilatif Abdalla ni nani? Ni mtu gani huyu? Ana mwelekeo gani? Ni mwanasiasa au ni mwana si hasa? Ni mpenda haki au ni mvuruga haki? Maswali haya yote ni mazito na magumu, na si rahisi kuyajibu kwa ukamilifu. Mtu angeweza kuandika tasnifu nzima ya Udaktari wa Falsafa akijaribu kuyajibu na asiyamalize! Lakini kwa hakika kuna kitu kimoja kinachojitokeza wazi kabisa katika haiba ya Abdilatif Abdalla; nacho ni uadilifu wa kutaka haki itendeke na ukinzani dhidi ya dhuluma na uonevu. Hebu niyagusie kidogo mambo haya.

Kwa sababu ya ujasiri wake, tangu akiwa mdogo kabisa Abdilatif alikerwa na kuchukizwa na utawala wa kikoloni, utawala wa mabavu na uonevu. Kwa watu wengine, katika udogo aliokuwa nao Abdilatif wakati huo, wala wasingeweza kuona na kuuchukia ukoloni kwa kiwango hicho. Na kwa hakika tunafahamu wazi kwamba kuna baadhi ya watu, wengine wakubwa kabisa na ambao tungetegemea wayapige vita maovu aliyoyaona Abdilatif katika uchanga huo, lakini badala yake wao nao wametokea kuyafanya hayohayo. Mfano wa wazi kabisa ni viongozi wetu wengi wa Afrika tulionao hii leo.

Abdilatif alikerwa zaidi alipogundua kwamba viongozi wa nchi yake walioshirikiana sana na wananchi kwa nguvu zao zote katika mapambano yao dhidi ya mkoloni na wakamfukuza, baadaye waliwageuka wananchi wao, wakawatadia na kuwafanya yaleyale ambayo wakoloni walikuwa wakiwafanyia.

Kutokana na machungu hayo baadhi ya Wakenya wakajiunga pamoja na kuanzisha chama cha siasa cha upinzani kilichojulikana kama KPU (Kenya Peoples Union). Sheikh Abdilatif Abdalla alijiunga na chama hicho cha KPU akiwa na umri wa miaka 19 tu. Akiwa mmoja kati ya wanaharakati vijana katika chama hicho baada ya muda kidogo alianza kutoa maoni yake katika maandishi.

Ama kwa hakika Sheikh Abdilatif Abdalla anakiri yeye mwenyewe kwamba alivutiwa sana na mawazo na mtazamo wa kaka yake, Sheikh Abdilahi Nassir, ambaye alikuwa mwanzilishi mmojawapo wa chama cha KANU, chama ambacho baadaye aliona kuwa kilikuwa kimepoteza uelekeo. Sheikh Abdilahi Nassir ndiye aliyemjenga na kumkomaza Abdilatif kisiasa, kwenye miaka ya mwanzoni mwa 1960.

Sheikh Abdilahi Nassir alikuwa akimpa vitabu vya kisiasa na kumhimiza avisome na kuvielewa. Kwa mujibu wa maelezo ya Abdilatif mwenyewe, aliwahi kupewa kitabu kilichoandikwa na Fidel Castro kilichojulikana kama History Will Absolve Me. Hiki kilikuwa kitabu cha utetezi wa Fidel Castro mahakamani, alipokuwa amekabiliwa na mashtaka ya kesi ya uhaini ya kujaribu kupindua serikali ya Kuba iliyokuwa ikiongozwa na Batista.

Abdilatif anasema kaka yake alimhimiza sana akisome na kukielewa kitabu hicho. Kitabu hicho kilichochea sana mawazo na fikra zake juu ya siasa, hasa siasa za Kenya ya wakati huo. Na hapa sasa ndipo lile swali muhimu linapofika mahala pake: je ni kweli kwamba mtu ambaye alikuwa hajiwezi kiakili hadi afeli mitihani ya shule ya KPE angeweza kuwa huyu tunayemwona katika haya tunayoyasikia? Jibu tunalijua.
 
Back
Top Bottom