Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
WASIFU WA JULIUS NYERERE: MWALIMU NYERERE NDANI YA OFISI YA TANU ISIYOKUWA NA SAMANI 1954
Nasoma siku za mwanzo za TANU kabla Mwalimu hajajiuzulu kazi ya ualimu.
Waandishi wa kitabu wanasema Nyerere alikuwa rais wa TANU na alikuwa anatumikia nafasi tatu.
Nafasi ya kwanza Mwalimu alikuwa mpiga chapa wa ofisi ya TANU, nafasi ya pili alikuwa muhudumu ndani ya ofisi na nafasi ya tatu alikuwa mpelekaji na mchukuaji barua posta na kwengineko ofisi yake ikiwa ndani ya chumba kimoja cha ofisi kilichokuwa hakina samani kwenye mtaa ambao barabara yake ilikuwa ya vumbi.
TANU ilikuwa haina fedha na yeye alikuwa anajishauri kama hela alizokuwanazo mfukoni anunue stempu za kutuma barua akose nauli ya kurudi Pugu au akapande basi barua zisitumwe majimboni ambako alikuwa anajitahidi kuwasiliana na watendaji katika ofisi changa za TANU.
Waandishi wanaeleza hali ngumu iliyokuwa inamkabili Mwalimu na TANU kwa ujumla.
Hali hii kwa hakika ikiwa kweli ilimukata Nyerere ni hali hii ya kusikitisha na kutia majonzi.
Waandishi wanasema hali hii ngumu ilikuja kuondolewa na Oscar Kambona alipojiunga na TANU September, 1954.
Kambona alifanya kazi kubwa ya kuiingiza wanachama TANU na ingawa hawasemi kuwa michango ya wanachama ndiyo iliyoitoa TANU kwenye dhiki ukisoma katikati ya mistari hii ndiyo picha inayojitokeza.
Kwa mtu anaeijua historia ya TANU ambayo wengi wanaifahamu TANU ya Abdul na Ally Sykes, Dossa Aziz na John Rupia maswali mengi yatakuja kichwani.
Kinakachojitokeza hapa ni kuwa waandishi hawaijui vizuri historia ya Nyerere na TANU katika miaka ile ya mwanzo.
Ningependa hapa kueleza historia ya Ali Msham na Julius Nyerere kusadikisha ukweli kuwa ofisi ya TANU ilikuwa haina samani za hadhi ya Rais wa TANU.
Mtoto wa Ali Msham, Abdulrahman anasema siku moja baba yake alipita ofisini kwa Nyerere pale New Street na akakuta ofisi iko taaban na hili lilimsikitisha sana baba yake.
Ali Msham alikuwa na kiwanda chake cha kutengeneza samani Mtaa ule ule wa Kariakoo ilipokuwa ofisi ya TANU lakini kwa mbele kuelekea Mtaa wa Kibambawe.
Ali Msham akachonga samani mpya na akanunua saa ya ukutani na alipokamilisha haya akamwalika Nyerere na viongozi wengine wa TANU, Sheikh Suleiman Takadir, Zuberi Mtemvu na John Rupia wafike kwenye tawi lake la TANU alilofungua nyumbani kwake Mtaa wa Jaribu Magomeni Mapipa amkabidhi Mwalimu samani za ofisi yake pamoja na saa ya ukutani.
Hapo chini ipo picha ya sherehe siku Ali Msham na wanachama wa tawi lake la TANU walipomkabidhi Rais wa TANU Julius Nyerere samani na kuanzia siku ile ofisi ya Mwalimu ikawa ofisi ya kupendeza.
Baada ya kueleza historia hii ya Ali Msham ningependa sasa kueleza namna Nyerere alivyokuwa akiadhimishwa na wale waliokuwa karibu na yeye katika siku zile za mwanzo na kisa hiki ni wakati bado anafundisha Pugu, hajaacha kazi.
Aisha ‘’Daisy’’ Sykes binti ya Abdul Sykes akiwa msichana mdogo wa miaka saba anakumbuka siku zile Nyerere alipokuwa anakuja nyumbani kwao.
Daisy anaeleza kwa kusema:
‘’...aliyeshika nafasi ya juu kabisa katika fikra zangu nikiwa mtoto alikuwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na ni kupitia kwake ndipo tukapata kujua kwa mara ya kwanza kuwa kuna kabila linaitwa, ‘’Wazanaki.’’
Kila alipokuwa anakuja nyumbani kwetu kuja kwake kulikuwa jambo maalum kulikosababisha minong’ono watu wakizungumza kwa sauti za chini wakipeana taarifa kuwa, ‘’Nyerere anakuja au keshafika.”
Kwangu mimi hii ilikuwa ishara ya kutimiza kazi yangu kwani siku zote nilikuwa nikiambiwa kutengeneza kifungua kinywa cha chai na mayai kila alipokuja nyumbani akitokea Shule ya Mt. Francis, Pugu alipokuwa akisomesha.’’
Chini hapo kuna picha ya Aisha ''Dasiy'' Sykes kama laivyo hivi sasa.
Nyerere Rais wa TANU anapita kwa Abdul Sykes asubuhi akitokea Pugu mwisho wa juma anakunywa chai ya mkate, siagi na mayai kisha anaelekea ofisini kwake ofisi ya TANU na baada ya kumaliza kazi Nyerere huyu huyu aliyekunywa chai nzito nyumbani kwa Mama Daisy anakabiliwa na safari ya miguu kurudi Pugu kwa kuwa hana fedha za nauli.
Kuna picha hapo chini ya Mama Daisy na mumewe Abdul Sykes.
Haya ndiyo ninayokutananayo katika Wasifu wa Julius Nyerere.
Kwa miaka mingi sana hakuna aliyekuwa anajua historia ya Ali Msham wala ya Abdul Sykes katika TANU wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika na pia hakuna aliyekuwa anajua michango ya wahisani wengi wa TANU na katika maisha ya kiongozi wao Julius Nyerere.
Ali Msham wa kwanza kulia na Julius Nyerere huyo kakaa kwenye meza siku ya kukabidhiwa samani ka ajili ya ofisi yake ya TANU New Street.