Wizara ya Ardhi
Govt Institution
- May 14, 2024
- 306
- 165
MTWARA
Timu ya wataalamu wa sekta ya ardhi tarehe 23 septemba 2026 ikiongozwa na Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Mtwara, Bw. Frederick Mrema, imefika Mji Mwema kwa ajili ya kufanya uhakiki wa taarifa za upimaji wa viwanja zilizobainika kuwa na tofauti wakati wa zoezi la upandishaji wa taarifa kwenye Mfumo wa e-Ardhi.
Zoezi hilo linalenga kuthibitisha na kusahihisha taarifa za upimaji ili kuhakikisha taarifa za viwanja zitakazowekwa kwenye Mfumo wa e-Ardhi zinakuwa sahihi, kamili na zinazoendana na uhalisia wa eneo husika.
Akiongoza zoezi hilo, Bw. Mrema amesisitiza umuhimu wa wataalamu kufanya uhakiki wa kina wa taarifa za ardhi kabla ya kuziingiza kwenye mfumo, hatua inayolenga kuimarisha usahihi wa kumbukumbu za ardhi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Soma Pia: Wataalamu wa ardhi waendelea kunolewa katika matumizi ya mfumo wa e-ARDHI
Uhakiki huo pia unalenga kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi za viwanja vyao kupitia mfumo wa kidijiti, huku ukisaidia kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na tofauti za taarifa za upimaji.
Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha matumizi ya e-Ardhi katika utoaji wa huduma za ardhi kwa njia ya kidijitali, kwa lengo la kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi, uwazi, usahihi na kwa wakati.