SoC02 Watanzania tuzijue sheria za nchi yetu

SoC02 Watanzania tuzijue sheria za nchi yetu

Stories of Change - 2022 Competition

Mohan Ksan

New Member
Joined
Jul 29, 2022
Posts
4
Reaction score
1
UTANGULIZI
Imepita takribani miaka sitini tangu Watanzania tupate uhuru mwaka 1961 chini ya baba wa taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere na sasa ni awamu ya sita chini ya rais wa Jamhhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan. Kwanza natoa pongezi kwa Serikali za awamu zote kwa kupambana dhidi ya adui "Ujinga" ambao ndilo lengo hasa la andiko hili. Ujinga ninaokusudia hapa ni juu ya masuala ya Sheria na katiba na siyo kutokujua kusoma na kuandika kama ambavyo imezoeleka katika jamii yetu.

Ujinga ni hali ya mtu, watu au jamii kukosa ufahamu (uelewa) wa jambo fulani. Awali ya yote yatupasa kutambua kwamba asilimia kubwa ya watanzania hawana ufahamu juu ya masuala ya kisheria. Tangu tupate uhuru, wengi tunadhani kwamba kujua katiba na Sheria ni jukumu la viongozi wa serikali, viongozi na watumishi wa Mahakama mfano hakimu na mawakili ilehali si kweli na kutokana na dhana hii potofu tumekua tukijidanganya kupambana vikali dhidi ya Ujinga wa kutojua kusoma na kuandika ilehali tunaongeza Ujinga kwa kutokujua Sheria kwani sheria za nchi yetu ni wajibu wetu sote kuzifahamu.

CHANGAMOTO YA KUTOKUJUA SHERIA NA MADHARA YAKE KATIKA JAMII YA WATANZANIA
Sheria zilizomo kwenye katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimepitishwa na bunge la Jamhhuri ya Muungano wa Tanzania huku Mahakama ikiwa ni muhimili wenye mamlaka ya kuwawajibisha wanaopatikana na hatia ya kuvunja sheria. Changamoto kubwa hapa ni watu kukosa ufahamu katika masuala haya ya kisheria na katiba.

Wanasiasa hususan wa vyama vya upinzanzani mfano CHADEMA wamekua wakiwaeleza Watanzania kuhusu mapungufu yaliyomo kwenye katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwahamasisha kuishinikiza serikali kuanza mchakato wa kuunda katiba mpya. Licha ya kufanya hivyo lakini mwitikio wa Watanzania umekuwa hafifu sana kwani Watanzania wengi hawaijui hata hiyo katiba ya sasa hivyo wanakosa maamuzi yoyote kutokana na kutokujua ubora na mapungufu yaliyomo kwenye katiba iliyopo.

Ukifuatilia chanzo cha migogoro ya kisiasa hapa nchini ni kutokujua sheria za nchi. Wanasiasa wa vyama vya upinzanzani mfano Viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wamekuwa wakilalamika kuonewa na vyombo vya dola hususan polisi. Hapa ni lazima tuelewe kwamba polisi ni chombo kinachosimamiwa na kuendeshwa na watu. Swali la msingi hapa ni je, watu hawa wanaoliongoza jeshi la polisi wanazijua Sheria? Kama itakua ni kweli kuna uonevu na ukandamizaji kwa vyama vya upinzanzani, inawezekana kabisa polisi hawaijui katiba ya nchi hivyo inabidi waelimishwe kwanza kabla ya kulaumiwa.

Serikali kupitia mamlaka yake ya mapato (TRA) imekuwa ikipata changamoto kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kukwepa kulipa Kodi. Juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanywa kunusuru mapato ya serikali lakini jambo la msingi hapa ni kujua kama wafanyabiashara wenyewe wanajuwa kua wana wajibu wa kulipa Kodi, na je wanafahamu kuwa kukwepa kufanya hivyo ni kosa kisheria? Najua wapo ambao hawajui kua kukwepa Kodi ni kosa kisheria hivyo pia ufahamu wa sheria unahitajika mahali hapa.

Familia nyingi nchini Tanzania zimejawa na unyanyasaji na uonevu. Mume kumpiga mkewe imekuwa kawaida kwa baadhi ya jamii. Unakuta familia yenye kumiliki rasilimali muhimu kama vile nyumba, mashamba na viwanja, bahati mbaya mume na mke wakitengana basi mwanamke haambulii chochote. Zipo jamii ambazo mwanamke hapewi haki ya kumiliki rasilimali yoyote. Uzuri ni kwamba sheria ziko wazi sana bila kupendelea jinsia yoyote, hivyo ufahamu wa sheria ni changamoto katika jamii kama hizi.

Raia wengi hawajui haki na wajibu wao katika jamii, wanaharakati mbalimbali nchini Tanzania na duniani kote wamekua wakitetea sana haki za wanyonge kama vile raia wanapoonewa na vyombo vya dola na wafanyakazi kuonewa na waajiri wao, lakini je hivi hawa watu wanaotetewa wanaweza kujitetea wenyewe, na pia wanajua kupigania haki zao wenyewe kisheria? Mtu yeyote akijiuliza maswali haya ataona kabisa kuna umuhimu mkubwa kwa raia wote kuzijua Sheria.

Makosa ya jinai kama vile wizi na ubakaji yamekithiri sana nchini. Kesi zimekua nyingi kwenye Mahakama mbalimbali lakini jambo la kushangaza watuhumiwa wengi wakipewa nafasi ya kujitetea wanadai wamefanya makosa hayo kwa bahati mbaya ama kwa kutokujua kua ni kosa kisheria. Hali hii inadhihirisha wazi kua elimu ya Sheria inahitajika kwa watu hawa.

UMUHIMU WA KUJUA SHERIA KATIKA JAMII YA WATANZANIA
Kuna umuhimu mkubwa sana kwa raia wa Tanzania kujua Sheria za nchi. Kwanza, kuwajengea raia uwezo wa kusimamia na kulinda haki zao kisheria. Raia wa kitanzania endapo wakizijua sheria, wataweza kusimamia haki zao pale watakapokua wanaonewa badala ya kusubiria wanaharakati waanze kupaza sauti kwa niaba yao. Vilevile husaidia raia wa kitanzania kujua wajibu wao. Wajibu wa raia wa Tanzania umeelezwa pia kwenye katiba ya Jamhhuri ya Muungano wa Tanzania.

Watanzania wakijua wajibu wao watafanya kazi kwa bidii, wafanyabiashara watalipa kodi bila shuruti na waajiri watalipa mishahara kwa wakati. Pia ufahamu wa sheria utapunguza vitendo vya uonevu na unyanyasaji. Kwa jamii za watu wanaofahamu Sheria za nchi vizuri ni vigumu kuonewa au kunyanyaswa lakini vilevile hawawezi kunyanyasa na kuonea watu wengine.

Vilevile kufahamu sheria kutawawezesha raia kulinda na kufuata sheria za nchi ya Tanzania na hurahisisha upatikanaji wa suluhisho la migogoro mbalimbali katika jamii na pia hujenga jamii bora ya raia wanaozifahamu sheria za nchi yao na kuwarahishia kuzifuata na kuzitii sheria hizo.

HITIMISHO
Kwa kumalizia naomba nitoe wito kwanza kwa kila raia wa Tanzania anaejua kusoma, aitafute katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuanza kujifunza sheria kwa kuzisoma, pili kwa serikali ya Jamhhuri ya Muungano wa Tanzania kuona umuhimu wa kuwa na raia wanaozifahamu sheria za nchi yao na ikibidi wafikiri namna ya kuanzisha somo la "Katiba na Sheria" litakalokua likifundishwa katika shule zote, kuanzia msingi mpaka vyuo vikuu. Hakuna maana endapo mwanafunzi wa sekondari anafundishwa Sheria za Newton (Newton's laws) na kanuni za Archimedes (Archimedes'principles) halafu asifundishwe sheria za nchi yake. Mwisho kabisa nitoe wito kwa vyombo vya habari kama vile redio, televisheni na magazeti kuanza kuelimisha na kuuhabarisha umma wa watanzania umuhimu wa kujifunza na kuzijua Sheria za nchi yao.

Kwa mawasiliano; 0684125580
 
Upvote 0
Back
Top Bottom