Wakuu,
Naomba nitofautiane na maelezo mengi yaliyotolewa na wenzangu, kuhusu hii dhana ya kuwa Watanzania wanaongea sana kuliko Wakenya na Waganda. Dhana hii ni ya zamani sana na ilisikika ikisemwa na wenzetu wa Kenya hususan askari polisi wao.
Askari polisi wa Kenya, wakati huo walikuwa wanapenda sana kuhongwa na dau la hongo yao kwa kawaida ilikuwa Shilingi 20/- (ishirini). Makosa makubwa yaliyokuwa yakiviziwa nao yalikuwa ya uvunjwaji wa sheria za uendeshaji magari barabarani na ya wale waliokuwa wakienda haja ndogo kando kando ya barabara au vichochoroni.
Hii ilikwenda mpaka watu wakawa wanatembea na noti za shilingi 20/- mifukoni au wanazipachika kabisa katika leseni zao. Sasa wenyewe kwa wenyewe wa Kenya, walikwisha zoeana. Wakikamatwa tu, kama ni yule wakukojoa anatoa pesa mara moja na shauri linakwisha. Kama ni dereva, akiulizwa leseni yake akimpa polisi. polisi anaifungua, anatoa ile shilingi 20/- iliyopkunjiwa humo ndani ya leseni, mashauri yanajiishia.
Sasa basi, inapokuja zamu ya kukamatwa mtu wa Tanzania, awe aliyekuwa na kosa la kukojoa au dereva, anakuwa na maelezo mengi sana ya kujitetea. Nao hao polisi wa Kenya wanakuwa hawana muda wa kusikiliza utetezi. Wanachotaka ni kuiona noti ya shilingi 20/- inatolewa. Wakaja na huu msemo, "hii mitu ya Tanganyika ina midomo mireefu sana." Na maanake ni kwamba, "unasema sana, bila kitendo (cha kutoa hongo)." Unapoteza muda. Kwa kukusikiliza wewe, yeye angeshakusanya shilingi ishirini, ishirini zaidi ya moja.
Hali hii imeifikisha dhana hii hapa tulipo, "tunasema sana kuliko tunavyotenda." Dhana hii si suala la uchangamfu, ukabila au kujua sana lugha ya Kiswahili. Tumeburuzwa sana na TANU/CCM na tunaendelea kuburuzwa hadi hii leo. Tunafanya nini katika kuirekebisha au kuiondoa kabisa hali hiyo zaidi ya kusema sema tu?
TANU/CCM imetufikisha kwenye mikasa yote hii, sijui Richmond, BoT, EPA na mingine mingi sana tuijuayo na tusioijua. Tunafanya nini zaidi ya kusema sema tu? Mpaka sasa tumepewa sifa nyingine mpya. "Watanzania wagumu wa kuelewa na wepesi wa kusahau."