Waliohusika kuifilisi ATCL wasakwe- Waziri
2008-12-19 11:30:02
Na Mashaka Mgeta
Serikali imeitaka Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Ndege Nchini (ATCL), kuwabaini wahusika katika kadhia ya kulifilisi Shirika la Ndege Nchini (ATCL), ili wawajibishwe.
Hatua hiyo, ilitangazwa jana na Waziri wa Miundombinu, Dk. Shukuru Kawambwa, alipozungumza katika mkutano wa majumuisho, baada ya kufanya ziara ya kukagua miradi ya ujenzi wa barabara za jijini Dar es Salaam.
``Niliwapa Bodi siku saba kunipa maelezo yenye kueleza sababu zilizofanya shirika hilo kufika hapo lililopo...watakaobainika kulifikisha katika hatua hiyo, watawajibishwa,`` alisema.
Dk. Kawambwa alisema katika mapendekezo yake, Bodi ya ATCL inapaswa kuainisha njia bora zitakazotumika kuwalipa mishahara wafanyakazi wake, katika kipindi ambacho haifanyi biashara.
Hivi karibuni, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), iliinyang`anya ATCL cheti cha uendeshaji wa safari za anga, kutokana na kutokidhi masharti yanayobainishwa katika sekta hiyo.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, David Mattaka, aliwaambia waandishi wa habari kuwa, sehemu kubwa ya mapungufu 482 yaliyobainika katika ATCL, yalisharekebishwa, bila kuwekwa katika kumbukumbu rasmi za maandishi.
Kwa mujibu wa Mattaka, licha ya kutokuwepo kwa kumbukumbu hiyo, ATCL ilikuwa inajiendesha kwa kufuata sheria za anga zinazotambulika kimataifa.
Lakini, akizungumza jana, Dk. Kawambwa, alisema kasoro zilizobainika katika ukaguzi uliofanywa dhidi ya ATCL, zinapaswa kufanyiwa kazi, ili kuliepusha shirika hilo na kadhia kama iliyotokea.
``Hatuwezi kuendeleza hulka ya kuwaone aibu watu wanaolitia Taifa hasara kubwa na kusababisha walio wengi kuendelea kuteseka,`` alisema.
Alitoa mfano wa kasoro hizo kuwa ni pamoja na mafunzo ya marubani yanayopaswa kufanyika mara kwa mara na matengenezo ya ndege za shirika hilo.
Hata hivyo, alisema serikali imelazimika kuingilia kati mchakato wa kurekebisha kasoro hizo, ili kuifanya ATCL irejee katika utoaji wa huduma zake kama ilivyokuwa awali.
``Hili ni shirika letu wenyewe, ni mali yetu sisi hivyo tutahakikisha kasoro zinafanyiwa kazi, na kurejeshwa kwa cheti chake mapema iwezekanavyo`` alisema.
Alisema katika kufuatilia suala hilo, wizara yake imeshafanya mazungumzo na ATCL na TCAA, ambapo imebainika kuwa mchakato wa kushughulikia kasoro zilizojitokeza unaendelea vizuri.
Kwa mujibu wa Dk. Kawambwa, ATCL inahitaji kiasi cha Dola 273,000 za Marekani ili kushughulikia matatizo yanayoikabili na kufikia hatua ya kujiendesha kibiashara.
Awali, Ofisa Uhusiano wa Umma wa TCAA, Abel Ngapemba, alisema hatua ya Umoja wa Mashirika a Ndege Duniani (IATA), kuizuia ATCL kufanya biashara, haitakuwa na athari kubwa kwa shirika hilo.
Aliliambia gazeti hili jana kuwa tamko la IATA lililokaririwa jana na baadhi ya vyombo vya habari, halihusu washirika wa kibiashara wasiokuwa wanachama wake.
Kuhusu hatua iliyofikiwa katika ukaguzi wa marekebisho yaliyowasilishwa na ATCL ili kupata cheti cha kutoa huduma ya usafiri wa anga, Ngapemba alisema suala hilo linashughulikiwa kwa umakini.
Hata hivyo, hakuwa tayari kusema ikiwa TCAA itafanikiwa kukamilisha zoezi hilo ndani ya siku kumi za kazi, ikiwa ni kuanzia Desemba 11, mwaka huu kama alivyobainisha Mattaka.
Ngapenda alisisitiza kuwa njia pekee kwa ATCL ni kufanikisha utunzaji wa kumbukumbu za kimaandishi kuhusu utekelezaji wa masharti ya usafiri wa anga.
My Take:
Hii inanikumbusha hadithi mojawapo ya Sungura. Sijui alijibadili namna gani na kumshawishi mtoto ampikie lile jogoo kubwa badala ya yeye mwenyewe kugeuzwa kitoweo kama alivyoagiza baba! Ati Waziri amewaagiza bodi watafute waliohusika na kulifikisha ATCL hapa.... Unawauliza wezi nani kaiba!?