Kuna kila dalili kuwa utitiri wa viongozi wa kisiasa wanaotimka kwenda kugombea ubunge huku wakiacha nyazifa zao nzito walizopewa na Rais huenda wamechoka kutumikishwa na kupelekeshwa na vyeo vya dezo vilivyojaa manyanyaso, mateso, fitna, ubabe na sintofahamu.
Sote tunajua Rais hakutaka waende kwenye ubunge, akapiga mkwara mzito, akawasimanga kuwa ni walafi wa madaraka, lakini hilo halikufua dafu, bado wameendelea kutimka kama hawana akili nzuri kuusaka ubunge huku wengi wao wakiwa hawana nafasi yoyote ya kupenya kwenye kura za maoni, na hata wakipenya bado huenda wakakatwa na Rais, maana tayari wameonyesha dharau na wamekosa utii.
Kwa wadadisi wanaona, wateule hao wametumia hii kama fursa ya kumkwepa Rais aliyekuwa anawapa vyeo vya dezo kama mtego ili kuwatumikisha kwa faida yake binafsi. Hawataki tena kufanya kazi ndani ya hii serikali kwa vyeo vya kupewa. Wamechoka!
Watu wamesepa zao.
Mzee abakie na mandondosha yake?