The Sheriff
JF-Expert Member
- Oct 10, 2019
- 747
- 2,112
Watoto ni waathiriwa wakubwa wa kazi za kulazimishwa/utumikishwaji katika sehemu nyingi duniani. Utumikishwaji ni hali ambapo watu wanalazimishwa kufanya kazi kinyume na matakwa yao, kwa vitisho vya adhabu, vurugu n.k.
Watoto wako katika hatari ya kutumikishwa kwa sababu mara nyingi hawawezi kujilinda au kudai haki zao. Huenda wakalazimika kufanya kazi katika sekta mbalimbali kama vile kwenye kilimo, uchimbaji wa madini, viwandani, pamoja na kazi za nyumbani. Katika baadhi ya matukio, watoto husafirishwa kuvuka mipaka na kulazimishwa kufanya ukahaba au kuingizwa katika unyonyaji mwingine wa kingono.
Hali Ilivyo Duniani
Kwa mujibu wa ripoti ya Makadirio ya Utumwa wa Kisasa Duniani mwaka 2022, jumla ya watoto milioni 3.3 duniani kote wako katika hali ya kutumikishwa.
Ripoti hiyo inasema kuna wasiwasi kwamba hali ya kutumikishwa kwa watoto imefanywa kuwa mbaya zaidi na janga la UVIKO-19. Inakadiriwa watoto milioni 10.4, kwa mfano, wamepoteza angalau mzazi mmoja kutokana na janga hili, kati yao milioni 7 wamekuwa yatima, hivyo kuachwa katika hatari ya kunyanyasika katika mazingira ambayo mifumo ya usaidizi haitoshi.
Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa jumla ya watoto milioni 1.7 wako katika unyonyaji wa kingono, ikiwa ni zaidi ya nusu ya watoto wote wanaotumikishwa. Zaidi ya milioni 1.3, ikiwa ni asilimia 39 ya jumla, wako katika unyonyaji wa kazi ya kulazimishwa. Watoto milioni 0.32 waliosalia katika kazi za kulazimishwa, asilimia 10 ya jumla, wanatumikishwa na serikali.
Kutumikishwa na serikali ni hali ambapo watu binafsi wanalazimishwa kufanya kazi chini ya vitisho vya kuadhibiwa na serikali au mamlaka ya serikali. Aina hii ya kazi mara nyingi hutumiwa kama njia ya kudhibiti au kunyonya vikundi fulani vya watu, kama vile wafungwa, wapinzani wa kisiasa n.k.
Utumikishaji ni ukiukaji wa haki za binadamu chini ya sheria za kimataifa. Utumikishaji ni kinyume cha sheria chini ya sheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na Azimio la Kimataifa la Haki za Kibinadamu na Mkataba wa Kazi ya Kulazimishwa wa Shirika la Kazi la Kimataifa. Pamoja na hayo, utumikishaji wa watoto unaendelea kuwepo katika baadhi ya nchi, hasa zenye migogoro au ukosefu wa utulivu wa kisiasa.
Madhara Yake
Watoto wanaotumikishwa wanapokonywa haki zao za msingi za kibinadamu, ikiwa ni pamoja na haki ya elimu, haki ya afya, haki ya kulindwa na haki ya kujifunza. Watoto hawa hukosa nafasi ya kwenda shule na hivyo kukosa fursa ya kupata elimu na stadi zitakazowasaidia kujenga maisha bora ya baadaye.
Watoto walio katika mazingira ya kutumikishwa mara nyingi hufanya kazi katika mazingira hatari na yasiyo salama, ambayo yanaweza kusababisha magonjwa, kuumia au hata kifo. Kazi ngumu na za mara kwa mara zinaweza pia kuathiri ukuaji wa mwili na akili ya mtoto, na hivyo kumfanya ashindwe kufikia uwezo wake kamili.
Kama ilivyo kwa kila mmoja, watoto nao wanahitaji kufurahia maisha yao. Hata hivyo, ni bahati mbaya kwamba watoto wanaotumikishwa wanapokonywa utoto wao na hukosa nafasi ya kuwa na wenzao wa rika lao, kujifunza michezo na kufurahia utoto wao. Wanapotumikishwa hudhulumiwa na kunyanyaswa kimwili, kijinsia na kiakili na hata kufanyishwa kazi za hatari kwa afya zao.
Ni Kifanyike
Utumikishaji ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na sheria za kimataifa, na ni muhimu kwamba serikali na mashirika mengine yashirikiane kushughulikia tatizo hili. Juhudi za kupambana na kazi za kulazimishwa zijumuishe hatua za kuzuia usafirishaji haramu wa binadamu, kuwalinda waathiriwa na kuwashtaki wahalifu. Ni muhimu pia kushughulikia sababu za msingi zinazosababisha utumikishaji, kama vile umaskini, ukosefu wa elimu, na ukosefu wa usawa wa kijamii.
Mashirika kama vile Shirika la Kazi Duniani (ILO) na UNICEF yanajitahidi kuongeza uelewa kuhusu kazi ya kulazimishwa na kuendeleza mikakati ya kukabiliana na tatizo hili. Kama watu binafsi, tunaweza pia kuwa na jukumu kwa kuunga mkono mashirika haya, kutetea mabadiliko, na kufanya maamuzi sahihi.