AKILI TATU
JF-Expert Member
- Feb 10, 2016
- 2,659
- 2,827
NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deo Ndejembi amewataka watumishi wa umma nchini kuwajibikaji kikamilifu katika kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa nchini ikiwemo ujenzi wa madarasa, zahanati, vituo vya afya na miundombinu ya barabara na reli, ili fedha inayotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kutekeleza miradi hiyo itumike ipasavyo kuleta maendeleo katika taifa.
Ndejembi ametoa wito huo kwa watumishi wa umma nchini, alipokuwa akizungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi yenye lengo la kutatua changamoto zinazowakabili na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa wilaya hiyo.
“Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa fedha nyingi kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye Halmashauri zote nchini, hivyo ni lazima tuwajibike kikamilifu katika kuisimamia miradi yote ili ikamilike kwa wakati na kuwanufaisha wananchi,” Ndejembi amesisitiza.
Aidha, Ndejembi amewataka watumishi wa umma nchini kuwajibika kwa wananchi kwa kutoa huduma bora ili kuondoa dhana potofu iliyojengeka katika jamii kuwa, watumishi wa umma hawawajibika ipasavyo kama ilivyo katika sekta binafsi.