Kutoka barazani mwa Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula
1hr ago·
Kwa mujibu wa Shahidi wa ACP Ramadhan Kingai (pichani), Freeman Mbowe alimuahidi Luteni Dennis Urio kuwa wakifanikisha kuchukua nchi [kwa njia ya mapinduzi] yeye Mbowe angempa nafasi kubwa.
Hata hivyo, aliyekuwa Mgombea wa Kiti cha Urais kupitia CHADEMA alikuwa Tundu Lissu. Hivyo kama CHADEMA ingeshinda, Lissu ndio angelikuwa Rais wala siyo Mbowe. Hapa kuna maswali kadhaa:
1. Kama Tundu Lissu ndiye ambaye angelikuwa Rais endapo CHADEMA wangelishinda Urais, Mbowe angewezaje kuahidi kutoa nafasi kubwa kwa watu wengine?
2. Inaonekana Mbowe [kama ushahidi wa ACP Kingai unavyodai] alikuwa tayari kupindua hata Serikali ya Tundu Lissu ili atimize ahadi yake?
3. Kuna kujikanganya kidogo katika mtiririko wa ushahidi: (a) Kuna kauli 'kuelekea Uchagauzi Mkuu'; (b) Kuna mazingira yanayoonyesha kuwa ACP Kingai alipanda cheo na kuushughulikia jambo hilo Novemba 2020, baada ya Uchagauzi Mkuu. Wakili wa Serikali hamuongozi vizuri Shahidi huyo kujibu maswali yaliyojificha, hivyo majibu yake bado yanaacha maswali mengi!
4. Kwa mantiki ya hoja ya 3 hapo juu, ni lini hasa Mbowe et al walipanga kufanya ugaidi wao? Je, ni kabla ya Uchaguzi Mkuu, kuelekea Uchaguzi Mkuu au baada ya Uchaguzi Mkuu?
5. Wakili wa Jamhuri anayemhoji Shahidi ACP Kingai hakuonekana kutilia sana maanani kipengere cha 'lini' katika hojaji yake. Hatujui kama ni makusudi, mkakati, au kupitiwa.
6. Je, hayo mambo yalikuwa kabla ya Uchaguzi Mkuu au kuelekea Uchaguzi Mkuu, Mbowe alikuwa amejua kuwa CHADEMA kitashindwa Uchaguzi Mkuu?
7. Inakuwaje Mwenyekiti wa Chama kikubwa cha upinzani nchini apange njama nzito kama hizo peke yake na Askari Jeshi mmoja wa kukodi huku Chama chake hakijui?
8. Ni Kiongozi gani wa Chama alijua mpango wa Mbowe au ni kikao gani cha Chama kilijadili kwa siri mpango huo na kilifanyika wapi na kiliwahusisha viongozi gani?
Kesi ya Mbowe na wenzake inavuta hisia za watu wengi. Mambo ndio kwanza yameanza katika Kesi hiyo ambayo ingawa haijatamkwa hivyo, lakini kwa mujibu ushahidi wa ACP Kingai, ilipaswa kuwa ni 'Kesi ya Uhaini'! Kwa kadiri ushahidi utakavyoendelea kutolewa, tutashuhudia mengi sana katika Kesi hii ya kusisimua! Endelea kutega sikio Mahakamani!
Uchambuzi wa Askofu ni mantiki (logic) ya mantiki (Reasoning of a Reason)!
Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!
Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula