esther mashiker
JF-Expert Member
- May 29, 2018
- 616
- 552
CHAMA cha Saidia Wazee Tanzania (SAWATA) kimempongeza Rais John Magufuli kwa ushupavu, alioonesha wa kuamua kutekeleza ujenzi wa Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Mto Rufi ji wa Julius Nyerere Hydropower Project (JNHPP), ambao ujenzi wake kwa sasa umefi kia asilimia 10.
Mradi huo wa kuzalisha megawati 2,115, unaotekelezwa kwa fedha za ndani, una thamani ya Sh trilioni 6.5 na hadi sasa Sh trilioni 1.2 zimeshalipwa kwa mkandarasi, sawa na asilimia 18 ya fedha zote. Utakamilika Juni 2022.
Wakitoa shukrani zao jana jijini Dar es Salaam kwa Shirika Umeme Tanzania (TANESCO), ambao ni waratibu wa mkutano baina ya pande hizo wa kuwaelimisha wazee hao umuhimu wa mradi huo, Katibu Tawi la SAWATA Uwanja wa Taifa, Rozina Mkapa alisema uthubutu wa Rais Magufuli ndio uliowezesha uwepo wa mradi huo.
Mkapa alisema ni tamaa ya wazee kutembelea miradi yote ni kujionea kazi nzuri iliyofanywa na serikali, kwani mradi huo ni ndoto za Mwalimu Julius Nyerere na serikali ya sasa iliona ni busara kuutekeleza kwa faida ya Watanzania. “Tunatoa shukrani zetu kwa Rais Magufuli kwa ushupavu wa kutekeleza ndoto za Nyerere kwenye mradi huu wa kuzalisha umeme kwani una manufaa makubwa ndani ya jamii,” alisema Mkapa.
Alisema lengo la chama hicho, ambacho wanachama wake ni wazee wastaafu ni kutoa fursa za kujadili mambo mbalimbali ya shughuli za kiuchumi, kubuni njia za kupunguza ukali wa maisha uzeeni na kubuni miradi na kuiendeleza.
Akizungumzia hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa mradi huo, Mratibu wa Mradi wa JNHPP, Stephen Manda alisema hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 10, na kwamba mkandarasi wa mradi Kampuni ya Arab ya Misri wameshapewa malipo ya awali ambayo ni Sh trilioni 1.2. Malipo yote ni Sh trilioni 6.5. “Mradi ulizinduliwa Juni mwaka jana, tunashukuru na kuomba Mungu hadi ifikapo Julai 2022 tuweze kukamilisha mradi huu, kwani tutapata uhakika wa kupata umeme megawati 2,115,” alisema Manda.
Alisema mradi huo una faida lukuki na ambazo ni kuzuia mafuriko mkoani Morogoro na Pwani, kutokana na maji kuwa mengi kwenye Mto Rufiji, kufua umeme na kuondoa mgawo wake nchini na tatu ni kuhifadhi mazingira. “Kumekuwa na adha ya mafuriko mkoani Morogoro na Rufiji, hivyo uwepo wa mradi huo utasaidia kupunguza adha hiyo na kuleta faida nchini, kwa kuwa kutakuwa na uhakika wa kupata umeme, lakini tunashangaa kuna baadhi wanaupinga,” alisema Manda.
Alisema mradi ukikamilika, utasaidia kupunguza bei ya umeme na utakuwa ni rahisi kupatikana kwa matumizi mbalimbali, ikiwemo ya viwanda na kutakuwa na umeme wa ziada ambao utauzwa nje ya nchi. Mradi huo unasimamiwa na Watanzania wenyewe, ambapo mshauri anatoka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na utakuwa na kilometa za mraba 914 na vivutio mbalimbali.
Akizungumzia utekelezaji wake, Manda alisema maandalizi ya awali yameshafanyika ambayo ni uwekaji wa miundombinu yote muhimu kama vile umeme, mawasiliano ya simu, maji na makazi kwa ajili ya mkandarasi na wanasiomamia wanaofanya kazi katika mradi huo.
Alisema utafiti wa ujenzi wa bwawa hilo, ulianza miaka mingi na mwaka 2017 mchakato ulianza rasmi. Februari mwaka jana tathmini zilianza na hatua za awali za ujenzi. Manda alisema walitegemea hadi sasa mradi uwe umefika asilimia 16.8 za ujenzi.
Lakini hadi sasa wapo asilimia 10 kwa sababu kwenye ujenzi wako mbele na kwenye manunuzi utekelezaji wake unasuasua, kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo baadhi ya vifaa kuagizwa nje ya nchi.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Demitruce Dashina alisema lengo la mradi huo ni kuendeleza viwanda nchini na kukuza shughuli za kiuchumi.
Dashina alisema ushiriki wa wazee hao katika mradi huo, utaleta mchango mkubwa ndani ya jamii jinsi ya kutekeleza miradi. Aliomba wazee hao wasaidie kuelimisha jamii umuhimu wake na kuacha kuupinga. “Tunawaambia haya ili na nyie mtusaidie kutoa elimu kwa wengine kufahamu manufaa ya mradi na kuacha upotoshaji,” alieleza.