Wazee Wana Haki na Wanastahili Kuwezeshwa Kutumia Fursa za Kidigitali

Wazee Wana Haki na Wanastahili Kuwezeshwa Kutumia Fursa za Kidigitali

The Sheriff

JF-Expert Member
Joined
Oct 10, 2019
Posts
747
Reaction score
2,112
Wazee na Digitali.jpg


Leo hii vijana wengi wana-enjoy urahisi wa maisha unaoletwa na teknolojia ya digitali kama vile kufanya manunuzi mtandaoni, malipo ya kidigitali na ufikiaji wa taarifa kwa urahisi mtandaoni. Lakini wazee wengi wasio na ujuzi wa digitali wameachwa nyuma.

Hata hivyo, kuna umuhimu wa wazee kuwezeshwa kutumia teknolojia ya digitali ipasavyo. Hii siyo tu itawasaidia kwa afya na ustawi wao wenyewe, bali pia kuwasiliana na wanafamilia wao, kupata taarifa tofauti na ushauri pamoja na kuwasaidia kwa ujumla kuondokana na upweke na hisia za kutengwa. Wazee wanaweza kutumia zana za kidigitali kuwasiliana na marafiki na familia endapo hawawezi tena kuwatembelea.

Wazee wanapitia changamoto nyingi kama vile matatizo ya kutoona vizuri au wakati mwingine kutoona kabisa, usikivu na upweke. Upweke unaweza kuwa na athari mbaya kisaikolojia na kimwili kwa wazee.

Upweke unaweza kusababishwa na kushindwa kutembea, kupungua kwa uwezo wa kuwasiliana au kukosa watu wa kuzungumza nao kutokana na kuongezeka kwa matatizo na shughuli za maisha ya kila siku.

Hata hivyo, kuwasaidia na kuwawezesha wazee kutumia fursa za kidigitali kunaweza kuwasaidia kuondokana na upweke na hisia za kutengwa na jamii, kuboresha afya zao na kuboresha maisha yao. Kwa mfano, wanaweza kupata vikundi vya usaidizi mtandaoni vya watu wanaopitia hali kama zao.

Kuna dhana potofu kwamba wazee hawawezi kujifunza matumizi ya majukwaa ya kidigitali/mitandao ya kijamii. Lakini, ukweli ni kuwa wazee wana uwezo wa kujifunza ujuzi mpya. Tunapaswa kuwahamasisha wanafamilia kufundisha wazee kutumia teknolojia hii.

Pia, taasisi mbalimbali pia zinaweza kuanzisha programu za mafunzo au warsha kwa wazee kujifunza kutumia majukwaa ya kidijitali ili waweze kujitegemea na hatimaye kufurahia manufaa ya uwepo wa teknolojia.

Hata hivyo, ni muhimu kutafuta njia za kuwawezesha wazee katika ushiriki huru wa kijamii kupitia mtandao, lakini pia ni muhimu zaidi kuwalinda na kuwawezesha kujilinda dhidi ya hatari wanazoweza kukumbana nazo, kama vile ulaghai wa mtandaoni n.k.

Ufahamu/ujuzi wa matumizi ya digitali umekuwa sehemu muhimu ya kushiriki kikamilifu katika jamii. Ikiwa ufikiaji wa teknolojia kwa wazee utakosekana, hii inamaanisha kuwa tunawafungia nje ya jamii, na hivyo kuzidisha kutengwa na upweke kwa wazee wetu.

Kwa hakika, wapo wazee wanaoonesha kutopendezwa na teknolojia. Lakini hii inaweza tu kuwa ni hofu inayotokana na ukosefu wa ujuzi. Hivyo, mafunzo sahihi yanaweza kusaidia kuzima hofu hizo na kuleta manufaa.

Ujumuishaji wa kidigitali ni jambo litakaloendelea kuwa muhimu kwani teknolojia inazidi kubadilika, na kila uvumbuzi mpya huja na changamoto zake.

Ikiwa leo ni Oktoba 1, ambayo ni Siku ya Wazee Duniani, mimi kama mmoja wa watu ambao nimebarikiwa kuwa na wazee kadhaa katika familia, nimeona ni vyema tukumbushane mawili matatu kuhusu masuala yanayowahusu wazee wetu.

Tusiwaache wazee wetu nyuma!
 
Back
Top Bottom