SoC03 Wazee wote wapewe pensheni kwani walilitumikia taifa

SoC03 Wazee wote wapewe pensheni kwani walilitumikia taifa

Stories of Change - 2023 Competition

October 2pm

Senior Member
Joined
May 2, 2023
Posts
106
Reaction score
282
Kila mtu siku moja atakuwa mzee. Nguvu tulizo nazo hazitadumu daima; kutembea kwa nguvu, kufikiri kwa kasi, macho yetu kuona mbali, vyote; uwezo wake utayoyoma na kupungua kabisa. Huo ndio utakuwa uzee. Tutahitaji msaada wa mkongojo kutembea, msaada wa watu kutusaidia katika yale tuliyokuwa tunayafanya wenyewe. Magonjwa na udhaifu wa uzee utafadhaisha kila mmoja wetu. Tunayohaja ya kuchukua tahadhari na hatua mapema tangu sasa tungali tuna nguvu. Kwani sisi ni wazee wa kesho, na bila ya shaka kesho sio mbali.

Wazee ni hazina kubwa ndani ya jamii. Taifa lisilo na wazee ni taifa lililokosa hekima na maarifa mengi. Kukosa wazee ni kutokujua wapi tumetoka, tulipo na wapi tuendako; naweza kusema ni kukosa uzoefu wa kujiongoza kama taifa. Wazee kutokana na umri mwingi walionao katika kuishi walilitumikia taifa, wana maarifa licha ya kuwa nguvu zao zimeishia katika kulijenga taifa kwa namna moja ama nyingine. Jasho na mawazo yao yamechangia pakubwa jamii na nchi yetu kuwa hivi ilivyo. Walilipa kodi iliyojenga yale yaliyowezekana kwa wakati wao, kama hivi leo nasi tufanyavyo. Ni haki yao kabisa kupewa pensheni ya uzee kwa ajili ya kuwapongeza kwa kazi nzuri waliyoifanya, lakini pia kwaajili ya kuwapunguzia hali ngumu ya maisha katika uzee wao.

“Mpango maalum wa pensheni kwa wazee” utahusisha vipengele viwili katika kuwahudumia wazee;
  1. Kutoa huduma muhimu za kijamii bure kama huduma za afya na usafiri.
  2. Kupewa pesa kidogo ya kujikimu kila mwezi.
1. KUTOA HUDUMA MUHIMU ZA KIJAMII BURE
Kwa ajili ya kupunguza changamoto na ugumu wa maisha kwa wazee, ikiwemo hali zao za afya kudhorota kutokana na uzee, serikali Kupitia mpango huu itoe huduma za afya bure katika hospitali na zahanati. Hii itawasaidia na kuwapunguzia wazee changamoto za afya wazipatazo. Itapunguza pia vifo vya wazee ambavyo kama wangalipatiwa huduma bora za matibabu na madawa basi wangaliendelea kuishi. Pia huduma za usafiri kwa wazee iwe bure au iwe nusu ya nauli ya mtu wa kawaida.

2. KUPEWA PESA KIDOGO YA KUJIKIMU KILA MWEZI
Kila mzee anahaki ya kulipwa pesa kidogo ya kujikimu itayayomsaidia kupunguza makali ya hali ngumu ya maisha. Mahitaji madogomadogo kama chakula, maji, mafuta miongoni mwa mahitaji mengine Kupitia pesa hii wataweza kupata unafuu kidogo. Serikali iweke kiwango sawa(Flat rate) kwa kila mzee nchi nzima. Kwa mfano kila Mzee awe anapewa pensheni Shilingi elfu hamsini(Tsh50,000/=). Hii iwe nje ya zile pensheni kwa wale wazee waliostaafu waliokuwa wanakatwa na mifuko ya hifadhi.
1684671731144.png

(mzee akiwa katika makazi duni. Picha kwa msaada wa google)
Kwa namna gani mpango huu utaweza kufanya kazi?
Bila shaka mpango huu utahusisha gharama nyingi za fedha, na ili mpango huu ufanye kazi kwa ufanisi ni lazima mipango kabambe na mikakati imara iwekwe. Napendekeza mbinu zifuatazo zitumike:
  1. Kiundwe kitambulisho cha mlipakodi cha kidigitali; Ambacho serikali itahakikisha kila mtanzania mwenye umri wa kulipa kodi anakuwa nacho. Kitambulisho hiki kiwe hivi; a) Kitambulisho hicho kiwe na kumbukumbu namba ya malipo(Control number), kila mtu awe na kumbukumbu namba ya malipo ya mlipakodi ambayo ataitumia kulipia kodi. Mtu akinunua au akiuza bidhaa au huduma iunganishwe moja kwa moja na kumbukumbu namba yake ya malipo ambapo itaunganishwa na mifumo ya ulipaji wa kodi. b)Kitambulisho kiwe na mfumo kama akaunti binafsi ya mtu ambapo atatumia nywila(neno la siri) kufanyia huduma za kikodi, kuangalia kumbukumbu na historia ya kila kodi alizotoa. c) Kitambulisho hiki cha kidigitali kimsaidie mlipa kodi kufanya shughuli zake kwa njia ya simu, laptop au kompyuta. Pia pawe na mfumo wa kutumia mitandao ya simu na kibenki katika utumiaji wa kitambulisho hiki.
  2. Sheria iundwe kuwa; kila atakayelipa kodi kwa miaka isiyopungua thelasini na tano(35) atanufaika na mpango huu; kwa kupata huduma muhimu za kijamii bure pamoja na pensheni ya kila mwezi. Hii itahamasisha watu kulipa kodi.
  3. Mifumo ya ulipaji kodi iboreshwe kwa namna ambayo ukusanyaji wa kodi utakuwa rafiki, rahisi, nafuu na yenye uadilifu. Kama ifuatavyo; i) Sheria kali zitungwe zitakazowabana watumishi wa mamlaka ya mapato ili kuwafanya wawe waadilifu. ii) Serikali iboreshe mifumo ya ukusanyaji kodi iwe kidigitali ili kuondoa usumbufu na rushwa. iii) Pasiwe na mlolongo mrefu katika usajili wa biashara na ulipaji wa kodi. iv) Serikali iajiri maafisa wa mapato ngazi ya kata au kila kijiji ambao kazi yao itakuwa kutoa elimu, kuratibu na kusaidia jamii katika masuala ya kikodi.
  4. Kila mzee apewe kadi maalumu ya kupewa huduma. Kadi hiyo wapewe wazee waliolijenga taifa kwa kulipa kodi kwa miaka isiyopungua thelasini na tano. Uzee isiwe kigezo pekee bali kigezo kiwe mzee aliyewajibika kujenga nchi yake kwa kulipa kodi. Uthibitisho uwe ile kadi maalumu ya kidigitali ya mlipakodi.
  5. Adhabu ya rushwa ingozwe makali kudhibiti ukiritimba.
  6. Serikali ipunguze kodi ya mafuta kwa asilimia fulani kwaajili ya kuwafanya wamiliki wa vyombo vya usafiri kusafirisha wazee aidha bure au kwa nusu nauli ukilinganisha na mtu wa kawaida.
  7. Kila kanda kijengwe kituo maalumu cha wazee wasiojiweza au wasio na watu wa kuwaangalia.
    1684672373912.png
    (Kituo cha kulelea wazee nchini uingereza, Age UK services. Picha kwa msaada wa google)
  8. Elimu ya umuhimu wa kulipa kodi itolewe; ilenge kuwapa wananchi uelewa na utambuzi, ziundwe propaganda na matamasha yatakayohamasisha jamii kulipa kodi, Watu waone ni fahari kulipa kodi. Pia elimu ilenge kutisha na kuogopesha mtu au watu wasiolipa kodi jinsi watakavyowajibishwa na sheria na adhabu kali.
Kwa nini mpango huu ni muhimu?
Mpango huu ni muhimu kutokana na sababu zifuatazo;
  1. Itapunguza na kuondoa hali ngumu ya maisha kwa wazee. Kwani wazee watapata mahitaji yao ya msingi kama chakula, maji, mboga, sabuni pamoja na kusafiri kwa urahisi kwenda kupata huduma za afya.
  2. Itachochea watu kulipa kodi na kusababisha maendeleo ya nchi. Watu wengi hasa vijana watahamasika kulipa kodi kutokana na kuona moja ya umuhimu wa kodi hizo ni kipindi watakapokuwa wazee achilia mbali maendeleo ya miundombinu na huduma za kijamii.
  3. Itaongeza umri wa kuishi kwa watanzania. Wazee wengi hufa mapema kutokana na ugumu wa maisha na kukosa huduma bora za afya. Mpango huu utasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza umri wa kuishi. Kwa sasa umri wa kuishi ni miaka 66.
  4. Itapunguza utegemezi wa Wazee kwa vijana wao. Wazee wakipewa pesa za kujikimu pamoja na huduma bure itapunguza utegemezi kwa vijana na wajukuu wao. Hii itachochea maendeleo.
Mwisho, kama yatafanyika haya basi kauli ya wazee ni hazina itakuwa yenye thamani kubwa, Sio kuwatelekeza.
 
Upvote 7
Upande wa Tanzania Bara, Zanzibar Mpango huu naona wameanza kuufanyia Kazi. Serikali inawalipa kila mwezi wazee Tsh 20,000/= za kujikimu. Ni mwanzo Mzuri
 
Back
Top Bottom