Habari za Zanzibar
JF-Expert Member
- Dec 18, 2024
- 651
- 433
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo, tarehe 15 Oktoba 2026 jijini Dar es Salaam, amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wamiliki wa Viwanda ya Uturuki (MÜSİAD), ukiongozwa na Makamu wa Rais wake, Bw. Selim Başdemir.
Mazungumzo hayo yamelenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kufikia lengo la biashara ya Dola za Marekani bilioni moja lililowekwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais Recep Tayyip Erdoğan wakati wa Ziara ya Kitaifa ya Rais Samia nchini Uturuki mwaka 2024.
Waziri Kombo amepongeza ziara ya ujumbe huo na kueleza kuwa ushirikiano na MÜSİAD utachangia kufanikisha lengo hilo kupitia uwekezaji katika sekta za kipaumbele, zikiwemo viwanda, kilimo, nishati, miundombinu na utalii. Aidha, amekaribisha kampuni wanachama wa MÜSİAD kuwekeza katika uzalishaji wa chakula cha mifugo, uongezaji thamani wa mazao ya kilimo, viwanda vya bidhaa za afya na vifaa vya ujenzi. Kwa upande wake, ujumbe wa MÜSİAD umeonesha utayari wa kuanzisha miradi ya uwekezaji nchini na kuhamasisha wanachama wake kushirikiana na sekta binafsi ya Tanzania.
MÜSİAD ni moja ya jumuiya kubwa za wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda nchini Uturuki, yenye wanachama zaidi ya 14,000 wanaowakilisha takribani kampuni 60,000 na kuchangia ajira kwa watu milioni mbili. Ushirikiano wake na Tanzania unatarajiwa kufungua fursa mpya za biashara, uwekezaji na ajira, pamoja na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.