mkiluvya
JF-Expert Member
- May 23, 2019
- 809
- 729
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeeo ya Makazi William Lukuvi ameagiza kutolewa Hati za umiliki wa ardhi ndani ya wiki pamoja pale mwananchi atakapokuwa amekamilisha taratibu zote za umilikishwaji ardhi.
Aidha, ameagiza wananchi kupatiwa hati zao za ardhi katika halmashauri waliolipia gharama za kupatiwa hati ili kuondoa usumbufu pamoja na gharama kwa mwananchi kufuatilia Hati kwenye Ofisi za Ardhi za mikoa.
Lukuvi alitoa agizo hilo jana wakati akizindua ofisi ya ardhi mkoa wa Tanga katika hafla fupi iliyofanyika jijini Tanga. Uzinduzi wa Ofisi hizo ulihudhuriwa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo, Mkuu wa mkoa wa Tanga Martine Shighela, Kamishna wa Ardhi nchini Nathaniel Nghode, Katibu Tawala mkoa wa Tanga Judica Omari, Wakuu wa wilaya za mkoa wa Tanga pamoja na viongozi wa taasisi mbalimbali za mkoa wa Tanga.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, wizara yake imekamilisha ndoto za Rais John Pombe Magufuli za kuondoa usumbufu kwa wananchi kupata hati za ardhi pamoja kufuata huduma za ardhi umbali mrefu na kutolea mfano kuwa, mwananchi wa mkoa wa Tanga alilazimika kuifuata huduma ya ardhi mkoani Kilimanajaro.
‘’Umekamilisha taratibu zote za kupatiwa Hati hapa Tanga, unaambiwa ukachukue Moshi ilipo ofisi ya Kanda, Rais ameliona hilo maana gharama za ufuatiliaji ni kubwa kuliko hata ghrama ya kulipia hati yenyewe’’ alisema Lukuvi.
Aliwataka Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuhakikisha pale hati za maeneo yao zinapokamilika wamfuate Msajili Msaidizi wa Hati katika ofisi ya ardhi ya mkoa kwa lengo la Msajili huyo wa Hati kwenda kuzikabidhi hati hizo kwa wahusika kwenye halmashauri badala ya wananchi kuzifuta mkoani. Kwa mujibu wa Lukuvi, kumbukumbu zote za ardhi katika mkoa zilizokuwa ofisi za Kanda nazo zimepelekwa mikoa husika na kutolea mfano kumbukumbu za mkoa wa Tanga ambazo awali zilikuwa zikihifadhiwa Dar es salaam na baadaye kuhamishiwa Moshi, Kilimanjaro sasa zimetunzwa Ofisi ya ardhi mkoa wa Tanga.