Suley2019
JF-Expert Member
- Oct 7, 2019
- 2,203
- 5,610
SERIKALI imesema ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2023, imeonyesha nchi inapoteza Sh. trilioni tano hadi sita kila mwaka kutokana na upatikanaji hafifu wa huduma za maji safi na salama pamoja na usafi wa mazingira.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akizindua mpango mkakati wa maji wa miaka mitano kati ya mwaka (2023 – 2028), pamoja na maadhimisho ya miaka 40 ya shirika linalojihusisha na usafi wa maji na mazingira la WaterAid.
Alisema kiasi hicho cha fedha ni kikubwa na ni sawa na asilia 3.2 ya Pato Ghafi la Taifa (GDP), na hivyo kuitaka wizara ya maji kushirikiana na wadau wa sekta binafsi na kuandaa mikakati ambayo itaokoa kiasi hicho cha fedha kupotea.
“Wizara ya maji ishirikiane na wadau wengine katika kuwezesha wilaya au miji kuandaa programu za uwekezaji katika sekta ya maji zilizofanyiwa uchambuzi wa kina na zinazojumuisha maji, usafi wa mazingira na usafi binafsi, ili kuweka bayana ni wapi rasilimali na juhudi za wadau zinapaswa kuwekezwa,” alisema Majaliwa.