Waziri Mkuu Kivuli, KC (ACT Wazalendo) wanaongoza Uchambuzi wa Bajeti Kuu ya Serikali 2025-2026

Waziri Mkuu Kivuli, KC (ACT Wazalendo) wanaongoza Uchambuzi wa Bajeti Kuu ya Serikali 2025-2026

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
5,352
Reaction score
15,876
WhatsApp Image 2025-06-21 at 08.03.46_d16e4193.jpg


View: https://www.youtube.com/live/CSYHcygl-bk
​

UTANGULIZI

Juni 12, 2025 Serikali iliwasilisha Bungeni Bajeti yake ya mwaka 2025/2026.

Hii ni Bajeti ya Tano kusomwa tangu Rais aingie madarakani na Waziri wa Fedha Mheshimiwa Mwigulu Nchemba. Matarajio yetu ilikuwa kuwa sera za bajeti za mwaka huu zingegusa maisha ya mtanzania ya kila siku – ambayo kwa miaka minne iliyopita, wananchi wamelia na kodi lukuki, tozo, ongezeko la gharama za Maisha. Mapendekezo ya Bajeti ya mwaka 2025/26 ni bajeti ya kugharamia masuala ya utawala na kulipa madeni pia bado inaendelea kujali kundi la walalakheri kuliko wanyonge. Inaonekana serikali inatekeleza sera za kuwanufaisha wafanyabiashara wakubwa kwa matarajio kuwa fedha hizi zitarudi kwa wananchi kutokea kwa wafanyabiashara (TRICKLE DOWN ECONOMICS). Sera za uchumi za namna hii haziwezi kamwe kuwaondoa Watanzania kwenye dimbwi la umasikini. Sera zinazofaa ni zile za kuwawezesha wananchi wengi (BOTTOM UP) ambapo sisi ACT Wazalendo tunaziita TAIFA LA WOTE, MASLAHI YA WOTE.

Katika uchambuzi wetu tumetazama kama bajeti imegusa vya kutosha matatizo ya kupanda kwa gharama za maisha kwa kuwa ni jambo moja kubwa zaidi linaloshughulisha Watanzania hivi sasa.

Changamoto nyingine inayokabiliwa wananchi wengi ni hupatikanaji wa huduma bora za afya. Kila kona ya nchi hii watanzania walalamikia upatikanaji wa huduma za afya, ukubwa wa gharama, huduma mbovu, ukosefu wa dawa na vifaa tiba na maeneo mengine hakuna kabisa Miundombinu ya huduma ya afya.

Maeneo megnine ya kutazama bajeti ya serikali inakwenda wapi, tutaangalia hili ili wananchi wajue Kodi zao zinafanya nini. Mchanganuo matumizi ya mapato ya Bajeti ya mwaka 2025/26 unaonyesha kuwa sehemu kubwa ya Bajeti ilitumika kulipa mishahara, kugharamia deni la Serikali, pamoja na matumizi mengine.

Aidha, katika uchambuzi wetu huu, tumeona kwamba mwaka huu ni wa uchaguzi, tumetazama Serikali imetenda na tayari imeanza kutumia fedha za Umma kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi mkuu, Tumetazama na kutoa uelekeo wetu kwa serikali, kwamba Bajeti ni ya Serikali na sio ya CCM na hivyo fedha za wananchi zisitumike kuibeba CCM bali kuupa haki umma uchague watu unaowahitaji.

Vilevile, tumefanya uchambuzi wa kina wa namna Serikali inavyoiga danadana kutekeleza miradi mbalimbali ya barabara, tumeonesha namna ambavyo kila mwka serikali inakuja na ulaghai mpya. Na kwasababu Serikali ya CCM imeshalewa sifa, Waziri wa Fedha hutumia mwanya huo kulaghai Umma kwa kuanza na Kibwagizo “Mama” ili kuwapumbaza wabunge wengine na watanzania, kwahiyo tumeonesha ulaghai waliokuja nao kwenye masuala ya ujenzi wa barabara mwaka huu.

Mwisho, katika uchambuzi huu tumetazama marekebisho ya kodi, tozo, makato ambayo kwa namna moja yameachwa bila kufanyiwa marekebisho au kuanzishwa mapya ambazo zinatoa maumivu kwa wananchi wa kawaida.

Hivyobasi katika uchambuzi huu, ACT Wazalendo tumeangazia kwenye maeneo tisa (9) ambayo yanaonyesha ni dhahiri bajeti ya Serikali haiendi kutoa nafuu kwa Umma, inakwenda kuongeza maumivu na mzigo mabegani mwa watanzania wenye kipato kidogo.

Haya ni maeneo 9 tuliyoyachambua;


Fedha za bajeti ya 2025/26 zitakwenda wapi?

Kwa mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali imepanga kutumia jumla ya fedha Shilingi Trilioni 56.49. Mgawanyo wa matumizi wa fedha za serikali kwa mwaka wa fedha 2025/26 unaonyesha kuwa Shilingi trilioni 38.99 imetengwa kwa ajili ya matumizi ya Mishahara, posho, magari na misafara ya viongozi, Mabango yay a Kumsifu Raisi, chai na Deni la Serikali ambayo ni sawa na asilimia 69.04% Wakati miradi ya barabara, mikopo ya wanafunzi, ujenzi wa vituo vya afya, shule, madawa, maji, pembejeo za kilimo, imetengewa Shilingi Trilioni 17.49 sawa na 30.96%. hii maana yake ni kuwa katika kila shilingi elfu moja ni shilingi 700 inaenda kwenye Mishahara, chai, Deni na posho na shilingi 300 tu ndio inaenda kuhudumia wananchi.

Sehemu kubwa ya Bajeti ya mwaka 2025/26 inaenda kugharamia maeneo yafuatayo;

Mishahara, na Matumizi mengine ni shilingi trilioni 24.78 sawa na 43.87%

Gharama za kuhudumia Deni la Serikali ni shilingi trilioni 14.20 sawa na 25.13 % ya fedha zote.

Bajeti ya miradi ya maendeleo ni shilingi trilioni 17.49% sawa na 30.96%

Mgawanyo wa bajeti uliopelekwa kwenye matumizi ya Maendeleo ya wananchi ni kiwango kidogo zaidi. Ukiangalia bajeti ya maendeleo, kiwango kinacholenga kuhudumia wananchi ni shilingi trilioni 17.49 tu sawa na 30.96% ya bajeti yote ya Serikali kwa mwaka 2025/26.

Hii ina maana kuwa miradi ya ujenzi wa vituo vya afya, shule, maji, barabara, dawa na vifaatiba, umeme vijijini na mijini haiwezi kutekelezwa kikamilifu kwasababu bajeti iliyotengwa ni kiduchu mno ukilinganishwa na fedha iliyotengwa kwenye matumizi mengine.

Wakati serikali inapanga kukusanya trilioni 40.466 kwa mwaka 2025/26 kwa mchanganuo huu takriban trilioni 38.99% zote ni kwa ajili ya mishahara na Deni la Serikali ni shilingi trilioni 1.47 tu kutoka mapato ya ndani inabaki kwa ajili ya Miradi ya maendeleo, kwa hiyo miradi ya maendeleo itategemea zaidi Fedha za nje au mikopo. Ndio maana tunasema nchi yetu inaendeshwa kwa mikopo, jambo ambalo linateteresha uhuru wetu.

Bajeti haijibu changamoto sugu zinazowakabili wananchi.

Bajeti ya Serikali Kuu kwa mwaka wa fedha 2025/2026 inaendelea kuonesha mwenendo ule ule wa bajeti ya mwaka uliopita yaani bajeti ambayo haijibu changamoto kubwa zinazowakabili wananchi wa kawaida. Zikiwemo gharama kubwa za maisha, ukosefu wa ajira, matatizo ya huduma za afya, elimu na maji.

Elimu: Uhaba wa walimu, madarasa na vitabu.

Tatizo la upungufu wa walimu katika shule za msingi na sekondari za umma linazidi kukua kutokana na jitihada ndogo za Serikali kuajiri. Kwa sasa tuna upungufu wa walimu 279,202 kwa shule za msingi, sekondari na zile za mahitaji maalum.

Bajeti Kuu ya Serikali haijatenga fedha kwa ajili ya kuajiri walimu wapya mwaka huu. Kwahiyo tutaendelea kukuza upungufu na kudondosha ubora wa elimu yetu.

Madarasa: Serikali imetenga shilingi bilioni 58.2 kwa ajili ya kujenga madarasa 6357 huku mahitaji ya madarasa katika nchi yetu ni zaidi ya madarasa 95,000.

Gharama za matibabu

Ukubwa wa gharama za matibabu na kukosekana kwa mfumo mzuri umeendelea kuwaingiza watanzania katika ugumu wa maisha na umaskini.

Mfumo wa kugharamia Afya za wananchi umekuwa wa kitabaka ambao maskini wengi hawawezi kumudu. Mfumo huu unatoa huduma kulingana na uwezo wa mtu badala ya magonjwa yanawakabili wananchi.

Mwaka huu Serikali imesema itatenga bilioni 57.8 kwa kutoza kodi kwenye vileo, vifaa vya urembo na vinywaji baridi. Kwanza, kiasi hiki hakiwezi kusaidia kutoa huduma ya afya kwa wananchi wote nchini. Pia, mfumo wa bima ya afya uliopendekezwa na Serikali sio mfumo endelevu.

ACT Wazalendo tumekuwa tukisisitiza wakati wote kwa kuitaka Serikali kuwekeza fedha ili kugharamia matibabu kwa watu wote nchini bila kuwepo na matabaka (ubaguzi).

Mfumo ambao tumekuwa tukipendekeza ni ule wa Bima ya Afya inayotokana na Mfumo wa Hifadhi ya Jamii. Tunataka mfumo unaomfanya mtu alipe bima kulingana na uwezo wake lakini apate huduma kulingana na mahitaji yake. Hali ya sasa katika upatikanaji wa huduma bora za afya kwa sehemu kubwa umekuwa ukitegemea uwezo wa kifedha wa Mwananchi kununua huduma hiyo badala ya uzito wa ugonjwa.

Bajeti ya mwaka huu inaendelea kuacha watanzania wakifa kwa kushindwa kumudu gharama za matibabu na kushindwa kuzika maiti kwa kutozwa gharama.

Pendekezo la ACT Wazalendo ni kutaka mfumo wa hifadhi ya jamii upanuliwe kutoka kwenye kundi dogo la watu wazima milioni 1.8 hadi milioni 18.2 ili kuhakikisha watanzania wote wanakuwa na bima ya afya itakayowezesha kupata matibabu stahiki bila kujali vipato vyao.

Uhaba wa wataalamu wa afya, dawa, vifaa na vifaa tiba.

Vituo vya kutoa huduma za afya vinaendelea kukabiliwana na uhaba wa rasilimali, kama mazingira duni ya kazi, na uhaba wa dawa na vifaa tiba. Uwekezaji wa ujenzi wa vituo vya huduma za afya unapaswa kwenda sambamba na jitihada za kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.

Kwa miaka minne mfululizo bajeti inayotengwa kununua dawa inazidi kushuka. Kutoka shilingi bilioni 218.1 zilizoidhinishwa mwaka 2021/2022 hadi shilingi bilioni 200 mwaka 2024/25 kwa ajili ya kununua, kuhifadhi na kusambaza dawa.

Pia, uhaba wa wataalamu na wahudumu wa afya. Hadi kufikia mwezi Aprili 2025, Sekta ya afya ilikuwa na jumla ya watumishi wa afya wapatao 126,925 ambao ni sawa na asilimia 36 tu ya watumishi 348,923 wanaohitajika katika sekta ya afya.

Bajeti ya mwaka haijaeleza au kutenga fedha ya kuajiri watumishi na wahudumu wa afya, hii ni hali mbaya zaidi.

Kwahiyo, bajeti hii haiendi kuongeza dawa zaidi, vifaa tiba wala kumaliza tatizo la uhaba wa watumishi. Hii ni bajeti ya anasa na kuwa acha wananchi wakiendelea kukosa huduma bora na muhimu.​

Kupanda kwa gharama ya mafuta ya petroli, Diseli na mafuta ya taa

Bei za mafuta ya petroli, Diseli na mafuta ya taa imeendelea kubaki juu kiasi cha kuathiri bei za bidhaa zingine. Bado bei ya mafuta haya haitabiriki kabisa, fedha zinazotumika kuagiza bidhaa hizi ni kubwa sana.

Kwa miaka mitatu ya bajeti kuanzia 2021 hadi 2025 pamekuwepo na tatizo la kupanda kwa gharama za mafuta ya Nishati (Petroli, Diseli na mafuta ya taa).

Serikali inayojali watu wake ilipaswa kufikiria njia bora za kutatua tatizo hili la mafuta. Jambo la kushangaza ni bado Serikali imeng’ang’ania kuweka utitiri wa kodi zaidi ya 22 zenye thamani ya shilingi 1447 katika kila lita moja ya mafuta. Pia, imeondoa ruzuku iliyoweka kama hatua ya kuhami mfumuko wa bei.

Bajeti na Ajira

Serikali ya CCM inaeleza kwamba katika kipindi cha Novemba 2020 hadi Februari 2025, serikali imefanikiwa kuzalisha jumla ya ajira milioni 8 (8,084,204) katika sekta rasmi na sekta isiyo rasmi. Hata hivyo, taarifa hiyo ya bajeti haielezi ni katika sekta zipi hususani ambazo ajira hizo zimezalishwa, ama ni katika kilimo, viwanda au biashara.

Wakati huo huo, taarifa ya taasisi ya kitaifa ya takwimu (NBS, 2024) inaeleza kwamba watu walio katika sekta rasmi [ya umma na binafsi] ni watu milioni 3.7. Ikiwa takwimu hizi za NBS zikionesha ukubwa wa tatizo la ajira, CCM wameamua kuchagua hadaa za kisiasa, kuudanganya umma na kucheza na hisia za wananchi.

ACT Wazalendo tunataka serikali kueleza kwa kina ni namna gani inatarajia kukabiliana na kumaliza tatizo la ajira. Serikali itueleze ina mpango wa kuajiri watu wa ngapi na kuwawezesha wananchi kujihusisha na shughuli za kujiingizia kipato.

Bajeti inapuuza Wakulima na Kilimo.

Kilimo na uchumi wa vijiji (Ufugaji, Uvuvi na shughuli za misitu) ndio shughuli ambazo watanzania wengi wamejiari huko. Taarifa ya hali ya uchumi 2024 inaonesha kuwa asilimia 65 ya Watanzania wameajiriwa katika shughuli za kilimo. Pia imeonesha kilimo kimechangia katika Pato la Taifa asilimia 26.7

Licha ya mchango wa kilimo katika pato la taifa na ajira nchini, uwekezaji wa Serikali katika sekta ya kilimo ni mdogo sana. Mbaya zaidi Serikali inataka kunufaika na kilimo kwa kuweka kodi, ushuru na makato lukuki. Yaani kila shilingi 100 inayopatikana katika taifa hili shilingi 26.7 ni fedha inayotoka kwa wakulima.

Pamoja na mchango huo, kiwango cha ukuaji wa shughuli za kilimo umekuwa wa kusua sua. Kwa mfano kutoka mwaka 2021 kasi ya ukuaji wa sekta hii ilikuwa ni 3.9%, mwaka 2022 kilikuwa kwa 3.3% hadi kufikia 4.5 kwa mwaka 2023. Ni wastani wa ukuaji wa 0.6 kwa mwaka.

Baadhi ya mazao yanayotarajiwa kuzalisha malighafi za viwanda uzalishaji wake umeporomoka kwa kiwango cha kutisha. Kwa mfano mazao ya Pamba na katani uzalishaji na mauzo ya nje ya zao hili yameshuka kwa asilimia 1.4, 9 na 16.2 mtawalia kwa mujibu wa Taarifa ya hali ya Uchumi iliyosomwa na Serikali bungeni tarehe 13 Juni 2025.

Sababu kubwa imeelezwa ni tija ndogo, teknolojia duni, ukosefu wa masoko na uhaba wa viwanda vya kusindika mazao ya kilimo (agroprocessing industries).

Hata hivyo, tumeona Serikali imetenga shilingi trilioni 1.2 sawa na asilimia 2.1 ya bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2025/26. Hii ni chini zaidi ya kiwango kilichokubalika cha asilimia 10 ya bajeti ya Serikali. Hii ina maana kuwa wakulima wanachangia shilingi 26.7 kati ya 100 wanazozalisha lakini wanachorejeshewa kwa ajili ya uwekezaji ni shilingi 2.1bya bajeti kuu ya Serikali.

Ni wazi kuwa Serikali ya CCM inawapuuza na kuwabeza wakulima wa nchi hii. Tunashuhudia kushuka kwa bei za mazao, wakulima kukosa mbolea za ruzuku, wakulima wananyang’anywa ardhi zao na kuwekewa utitiri wa kodi kwa kile kinachozalishwa.

Kukosekana kwa mfumo wa kodi unaoeleweka na usiotetereka katika kuisimamia sekta ya Kilimo inarudisha nyuma maendeleo ya wakulima. Kilio cha kuporomoka kwa bei ya mazao, wakulima kutoona tija ya jasho lao ni kutokana na Serikali kutoweka mkazo na kuipuuza sekta ya kilimo.

Kama kawaida, bajeti hii imeendelea kuwapuuza wakulima wa taifa hili na kuwafanya waendelee kuishi Maisha dhalili.


Kuongezeka kwa kasi Deni la Taifa ni hatari

Hadi kufikia Aprili 2025 deni la Serikali limefikia shilingi trilioni 107.70 ikilinganishwa na shilingi trilioni 91.7Machi mwaka 2024. Hili ni ongezeko la shilingi trilioni 16. sawa na 17.23% kutoka mwaka wa Fedha uliopita. Ambapo Deni la Nje ni Trilioni 72.94 na Deni la Ndani ni Trilioni 34.76

Kasi ya ukuaji wa Deni la Serikali ya awamu wa Sita chini ya Rais Samia kwa miaka minne imekuwa kubwa sana. Ongezeko hili halijawahi kutokea tangu nchi yetu ipate uhuru. Amekopa kiasi cha shilingi trilioni 52.73 Tangu alipoingia madarakani.

Mwenendo huu wa Deni la Serikali unatishia maendeleo ya watu, uwezo wa nchi kujihudumia na kusababisha ukuaji wa uchumi unaoendeshwa na deni (debt driven growth).

Waziri ameliambia Bunge kuwa eti Deni la Serikali ni Himilivu lakini takwimu zinamkataa, Ilipotufikisha serikali fisadi ya CCM ni kwamba Uwiano wa Deni kwa Pato la Taifa ni 40.3 kwa asilimia 55, hii ni kuonesha kuwa Kama taifa tunakaribia mstari Mwekundu wa hatari ya kukopesheka. Madhara makubwa ya ukopaji huu holela ni kuongeza gharama za kulipa deni kama tunavyoona kwenye bajeti ya mwaka huu.

Athari za ukubwa wa deni la Serikali linaangukia kwenye mabega ya wananchi wanyonge. Wananchi wanaongezewa kodi, ushuru na makato katika huduma muhimu kama vile umeme, elimu, afya, maji na kodi kwenye mazao ya kilimo ili kulipa madeni haya.

Mathalani mwaka huu 2024/25 Serikali imepanga kukusanya shilingi trilioni 40.46 kati ya fedha hizo shilingi trilioni 14.20 zitaenda kulipia deni la Serikali. Nchi inatumia sehemu kubwa ya makusanyo yake kwenda kuhudumia deni badala ya kutoa huduma kwa wananchi walalahoi.

Waziri wa Fedha amekiri kwamba ongezeko la deni linatokana na kushuka kwa thamani ya shilingi lakini ameshindwa kutoa njia za kulinda thamani ya shilingi, shilingi ya Tanzania ni Miongoni mwa shilingi inayofanya vibaya sana dhidi ya Dola kwa mwaka huu 2025. Ni wazi kuwa jitihada za makusudi kabosa zinahitajika ili kupandisha thamani ya shilingi yetu.

Katika miaka minne ya Baraza tumekuwa tukionyesha njia madhubuti za kupandisha thamani ya shilingi yetu. Tulieleza njia za kuimarisha shilingi kwa namna tatu.

Kwanza, kuongeza uwezo wetu wa kuuza bidhaa nje

Kuongeza mauzo ya bidhaa za kilimo nje ikiwemo kuongeza thamani ya mazao.

Kuweka nguvu kubwa kwenye mradi wa Mchuchuma na Liganga ili kuzalisha bidhaa za chuma kwa matumizi ya ndani na nje. Hii itasaidia kuokoa fedha za kigeni zaidi ya Dola za kimarekani Bilioni1.2 ambazo tunatumia kuagiza chuma kutoka nje kwa mujibu wa taarifa za Serikali.

Serikali iharakishe Mradi wa kusindika Gesi asilia wa Lindi (LNG) na kuufungamanisha na Mradi wa kuanzisha kiwanda Kikubwa cha kuzalisha Mbolea. Hii itasaidia kuokoa Fedha za Kigeni tunazotumia kuagiza Mbolea kutoka nje, ambapo mwaka 2024 tulitumia Dola za Kimarekani Milioni 345.4. sawa na shilingi Billion 900.6

Kuboresha miundombinu na vivutio vya sekta ya utalii ili kuongeza idadi ya watalii maradufu ya idadi ya sasa.

Kuongeza ufanisi katika Bandari zetu ili kufaidika na Uchumi wa jiografia kwa kuongeza idadi ya mizigo inayopita na kutoka nchi jirani maradufu ya tunayohudumia sasa. Sasa hivi mapato ya Fedha za kigeni tunayoyapata kwa huduma za usafirishaji (transit trade).

Pili, kupunguza uagizaji wa bidhaa za nje;

Magari yote ya Serikali yaanze kutumia Gesi asilia (CNG) ili kupunguza kutumia fedha nyingi za kigeni kuagiza bidhaa za mafuta. Pendekezo hili pia litapelekea kupunguza matumizi ya Serikali kwa takribani shilingi bilioni 500 kwa mwaka.

Hivyo basi, Bohari zote za Serikali (GPSA) zifungwe mitambo ya kujazia gesi asilia (CNG) mara moja.

Vile vile, tunashuhudia ubadhirifu na upotevu mkubwa wa fedha unaofanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi bila kuchukuliwa hatua za kiuwajibikaji. Badala yake viongozi wanaendelea kulitafuna taifa kwa kujinunua magari ya kifahari, kujiongezea posho, safari za nje na mishahara.

Katika uchambuzi wetu wa ripoti ya CAG mwaka huu tulionesha ubadhirifu wa fedha za umma katika utekelezaji wa miradi na majukumu mbalimbali ya wizara, taasisi za Serikali na Mashirika ya umma. Jumla ya hoja zenye thamani ya shilingi trilioni 2.56 zilihusishwa na ubadhirifu.

Tatu, Serikali ifanye marekebisho ya sheria mbalimbali za kodi zinazohusisha Kampuni za kimataifa (MNCs) ili kuzuia kumomonyoa wigo wa kodi (Base Erosion and Profit Shifting) kunakofanywa na kampuni hizi. Hili linawezekana kwa Serikali kuchukua hatua ya kupitia mikataba ya kikodi (double taxation treaties) ambayo Tanzania iliingia na nchi nyingine duniani.

Mwisho, Waziri anajua mikopo si njia sahihi, kutokana na ukweli kuwa inatuweka kwenye utegemezi wa kibajeti na kusua sua kwa utekelezaji wa malengo ya taifa. Kujifaharisha katika Bunge na umma kwamba tunaelekea kuzuri ni kutaka kusafisha makosa yanayofanywa na serikali ya CCM ambayo wananchi hawatakiwi kukuyakubali.

Ufinyu wa bajeti na ucheleweshaji wa utekelezaji wa Miradi ya Ujenzi wa Barabara.

Katika mwaka wa fedha 2025/26 serikali imeendelea kutenga bajeti kiduchu kwa ajili ya Ujenzi wa Barabara mpya, ukarabati na matengenezo. Serikali imetenga shilingi trilioni 2.1 kwa ajili ya miradi ya maendeleo. TANROADS imetengewa shilingi bilioni 986.3 kwa ajili ya matengezo na ukarabati wa Barabara kuu na za Mikoa.

Hata hivyo, kati ya fedha hizo trilioni 1.02 zimetengwa kwa jili ya kulipa madai ya wakandarasi ikilinganisha na mahitaji na malimbikizo ambayo ni takribani shilingi trilioni 4.6 kwa mujibu wa ripoti ya CAG 2023/24. kushindwa kwa Serikali kulipa madeni ya wakandarasi na watoa huduma kunachangia kudorora kwa kasi ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa Barabara.

Aidha, Serikali iliahidi kwa kishindo mwaka 2023 kuwa itajenga barabara saba (7) zenye urefu wa kilomita 2035 kwa utaratibu wa Wakandarasu kusanifu, kufanaya manunuzi, kujenga na kugharamia miradi hiyo (EPC+F) zenye thamani ya Tsh trilioni 3.775, kupitia TANROADS.

Wananchi tuliahidiwa ujenzi wa barabara hizo ungeanza punde na zingekamilika kwa pamoja ndani ya miaka 5. Tumeshangaa kuona mwaka huu serikali imegeuka na kuja na kauli zingine kwamba sasa itajenga kwa utaratibu wa Sanifu na Jenga.

Kauli hii ya Serikali Bungeni inaibua maswali mengi yanayohitaji majibu. Serikali iliwezaje kuingia mikataba na wakandarasi ambao hawana uwezo wa kujenga Barabara hizo? Je, Serikali haikufanya ufuatiliaji wa uwezo wa wakandarasi hao (due diligence)?

Maswali haya yanaonyesha kuwa ni wazi Serikali iliwalaghai watanzania na kuwapa matumaini bandia wananchi wa maeneo haya ambao hawana barabara zinazopitika tangu uhuru.

Tunamtaka Waziri wa Fedha atoe ufafanuzi wa utaratibu huu mpya kwa kutuhakikishia kuwa haitokuwa kichaka cha kuiba fedha za wananchi kwa kukwepa utaratibu wa zabuni uliopo kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande mwingine, bajeti ya serikali haiendi kujibu kilio cha kusua sua kwa miradi kutokana na kutoongeza bajeti ya mirdi ya maendeleo. Ripoti ya CAG imeonesha jumla ya miradi 136 yenye thamani ya Shilingi Trilioni 1.34 imesuasua huku baadhi ya miradi ikiathiriwa kwa kucheleweshwa hadi asilimia 92. Hii inaonyesha udhaifu mkubwa wa usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Hali hii inatia hasira kali kuona kwa taifa maskini kama Tanzania, ambalo linapaswa kuhakikisha kila shilingi inayotengwa kwa maendeleo ya wananchi badala yake inaishia kupotea kwenye matumbo ya wachache.

Aidha, CAG ameonesha utekelekezwaji wa miradi wenye mamilioni ya fedha. Katika sekta za barabara, afya, maji na miundombinu, ripoti inaonyesha miradi mingi imetelekezwa, ikiwemo miradi 22 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 505.63 ambayo ilitelekezwa kwa sababu ya ukosefu wa fedha na mipango duni.​

Ni muhimu kwa serikali kutenga fedha za kutosha na kutoa


Serikali haijasikia Kilio cha Wastaafu kuhusu Kikokotoo cha Mafao (Pensheni)

Suala la kikokotoo cha Wastaafu kinaendelea kuwa kitanzi kwa watumishi wanaomaliza muda wao. Watumishi kama Polisi, waalimu, watumishi wa afya na watendaji wengine wa serikali na serikta binafsi wanaendelea kuwa na kilio kisichokua na majibu kutoka kwa Serikali.

Serikali haijafanya marekebisho ya kikokotoo cha wastaafu kinacholalamikiwa cha 40 na 35 kwa wafanyakazi wa wanaochangia mifuko ya PSSSF na NSSSF mtawalia.

Hatua hii inapelekea wafanyakazi na watumishi kupata malipo yao ya mkupuo kwa kupunjwa. Serikali ya CCM bado inaendelea kutumia kanuni zilizopitishwa mwaka 2022 zinazompunguzia mstaafu mafao yake kwa kuwalaghai kuwa itawasidia walakini inaendelea kuwakandamiza kupitia vipengele vinne.

Kipengele cha kwanza ni hiyo asilimia ambayo inapunguza mafao kwa wastani wa asilimia 60

Kipengele kingine, kigawo (Kikiokotoo) cha 1/580 badala ya kutumia 1/540 kinampunguzia mfanyakazi zaidi ya asilimia 7.

Utaratibu wa kutumia wastani wa mishahara mitatu ya juu badala ya kutumia mshahara wa mwisho inaporomosha mafao ya mstaafu kwa asilimia 7.2

Kupunguzwa miaka ya kuhudumiwa na pensheni kutoka miaka 15-5 hadi miaka 12.5 inapoteza maana ya pensheni na kuwajaza hofu wastaafu.

Pili hatua hii inaendeleza ubaguzi miongoni mwa wafanyakazi. Kuwabagua wafanyakazi kutoka sekta binafsi wanaohudumiwa na NSSSF ni kufanya makosa yanayojirudia.

Mfumo wa hifadhi ya jamii husaidia kulinda maisha ya watu na kutoa uhakika wa kuishi vizuri unapokutwa na majanga au kupoteza uwezo wa kufanya kazi kwa namna yoyote ile. Hatupaswi kuwaadhibu wazee wetu kwa kukubali kanuni hizi kandamizi zinazoenda kuwapunja mafao yao na kufupisha muda wa kuwahudumia na kuwakadiria kifo mapema zaidi.

Aidha, tunaendelea kupinga uamuzi wowote wa serikali kung'ang'ania shilingi za wafanyakazi kwa kuwaingizia kwenye mchezo wa "lesser devil“

Tunaitaka serikali kurejesha kanuni za kabla ya 2018 ambazo zinatoa mafao ya malipo ya mkupuo kwa 50% kikokotoo kuwa ni 1/540, umri wa kuishi baada ya kustaafu kuwa muda wote atakaoishi.

Vilevile, Waziri amelieleza Bunge kupitia hotuba ya Bajeti kuwa Serikali haijamaliza kulipa deni la waliokua wafanyakazi kabla ya mwaka 1999 na kwamba katika Trilioni 4.46 wanazodaiwa na PSSSF wamelipa Trilioni 2.18 tu, madai haya yanaifanya PSSSF kukosa uwezo wa kuwalipa haraka wastaafu na kuwekeza kwenye shughuli zitakazosaidia kukua kwa mfuko huo.

Badala ya Kupanga kulipa Bilioni 630, ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kulipa fedha zote kwa mkupuo kupitia mfumo wa hati fungani kwa madeni ya kabla ya mwaka 1999.


Marekebisho ya Kodi, Tozo na Makato

Katika bajeti ya mwaka huu Serikali imeanzisha Kodi, tozo, ada na makato ambayo zinaenda kuua fursa, uwezo wa kunufaika na maumivu kwa wananchi wanaojitafuta. Baadhi ya kodi zilizoanzishwa ambazo zinaenda kuongeza maumivu kwa wananchi ni kama zifuatazo;

Tozo ya shilingi 10 kwa kila Lita ya mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya taa

Tozo hii inaongeza ugumu wa gharama za maisha kwa wananchi, Petroli na Dizeli ndio zinazosukuma sehemu kubwa ya maisha ya wananchi, tozo hii itaongeza sana gharama za usafiri.

Tozo ya 500 kwa kila tiketi inayotolewa na mtoa huduma za usafirishaji kwa njia ya Treni.

Serikali badala ya kushajiisha na kuhimiza matumizi ya treni kwa kuhakikisha inakua na bei ya chini, na kutengeneza faida ambayo itasaidia umma wa watanzania, inzidi kuweka ugumu. Tozo hii itaongeza bei ya usafiri huu unaochipua kwa kasi.

Ushuru wa bidhaa kwenye bidhaa kwenye huduma za mawasiliano ya kielekroniki kutoka 17-17.5

Ushuru huu utaongeza makato kwa wananchi wachini wanaofanya malipo kwa njia ya mtandao, Ushuru huu unaongeza sana mzigo zaidi licha ya makato makubwa yaliyopo sasa bado Serikali inaendelea kuminya wananchi kwa kuwaongezea ushuru.

Ada kwa wapambaji wa keki 10,000

Waneni (MCs) 40,000

Wapigapicha 10,000

Wapambaji katika sherehe/ matukio10,000

Serikali imeanzisha ada kwa wajasiriamali wadogo kwa kuanzisha ada zitakazozalisa usumbufu na ukatisha tamaa kwa biashara zinzazochipua.

Kuondoa tozo ya kuingiza Klinka kwenye Tozo ya 10% kutoka nje.

Kuondoa tozo hii kunatarajiwa kupunguza gharama za uzalishaji na kushusha bei, uzoefu unaonesha tangu bei ya Saruji ilipoanza kupanda haikuwahi kushuka. Kuondolewa tozo hii kunaondoa ulazima wa wazalishaji wa Sruji kutumia rasilimali za ndani kuzalisha bidhaa hiyo, bidhaa kama Jasi (Gypsum ore), Chokaa, Makaa ya Mawe na Chuma gafi (Iron ore) vya ndani vitakosa soko la uhakika.

Kupunguza tozo ya ushuru wa huduma kutoka 0.3 hadi 0.25

Kupunguzwa kwa tozo hii kunapunguzia halmashauri vyanzo vya mapato, serikali kupitia mamlaka za serikali za mitaa imeshindwa kukusanya kikamilifu asilimia 0.3 na badala yake imelipunguza.

Kupunguza ada ya ushuru wa hoteli kutoka 10% hadi 2%

Ushuru wa hoteli ni miongoni mwa vyanzo muhimu vya halmashauri, kupunguzwa kwa chanzo hiki kutazorotesha uwezo wa halmashauri kupata mapato.

Kuanzisha tozo ya 0.1 ya thamani ya soko la madini.

Uanzishwaji wa tozo katika masoko ya madini kutapelekea wauzaji wengi kutorosha madini au kuyauza nje ya soko, serikali inapaswa kuweka vivutio vya madini kuuzwa ndani na sio kuongeza mzigo unaosukuma wauzaji na wachimbaji kuuza nje au kutorosha kwa kutafuta unafuu.

Kutoza ushuru wa forodha 25% badala ya 10% kwa matairi ya Pikipiki.

Uendeshaji wa pikipiki umekua sehemu kubwa ya ajira kwa vijana, sehemu kubwa ya matairi haya inazalishwa nje, na kiasi kidogo kinachozalishwa ndani hakitoshi, kuongeza ushuru wa forodha kwenye bidhaa hii ni kumtwika mzigo bodaboda ambae atalazimika kununua tairi kwa bei ghali zaidi. Tairi ya Pikipiki kwa sasa ni shilingi 60,000 baada ya tarehe 01 Julai bei ya tairi itakua 62,000

Hata hivyo Serikali inayorundika Tozo, Ushuru, kodi na ada mbalimbali hasa kwa wananchi wenye kipato cha chini haijafanya mabadiliko yoyote kwenye mzigo waliouweka mwaka jana na miaka ya nyuma.

Bado, Tozo ya shilingi 1000 kwenye kila mfuko wa saruji wa 50 Ipo!, bado tozo ya Asilimia 2 kwa wachimbaji wadogo Ipo!, Bado Makato ya 15% kwa yanayokatwa kwa wanufaika wa bodi ya Mikopo Yapo!, bado makato ya fedha za kutolea ya asilimia 50 Yapo!

Chama Cha Mapinduzi CCM kinaendelea kufukarisha wananchi wa kawaida na kutajirisha matajiri wachache wenye mitaji Mikubwa. Kodi na tozo zote zinalenga kuwapatia faida zaidi matajiri na makampuni makubwa na kuwanyonya wananchi walalahoi, Masikini wan chi hii. CCM haina tena uwezo wa kukabiliana na ugumu wa maisha ya wananchi, inategemea kuwanyonya wananchi ili iendelee kusalia madarakani. Wananchi sasa wanapaswa kuwakataa na kusema sasa Basi inatosha Kuendelea kuikumbatia CCM ni kukumbatia Umasikini. Wabunge wa CCM hawajali tena wananchi bali hofu za ubunge wao.

ACT Wazalendo, tunaitaka Serikali chakavu ya CCM kuondoa maramoja Tozo zote kandamizi zinazozuia biashara ndogo kuchipua, wachimbaji wadogo kunufaika, viwanda vya ndani na rasilimali za ndani kutumika katika uzalishaji na tozo zote kandamizi.

Bajeti ya Uchaguzi isitumike kwa Uchafuzi

Serikali imetenga takribani shilingi trilioni 1 kwa ajili ya uchaguzi mkuu, ambapo mpaka sasa imetumia shilingi bilioni 741.5 na kiasi cha shilingi bilioni 378.2 kinaelezwa kutengwa kwa ajili ya kuwezesha mchakato wa uchaguzi kwa mwaka 2025.

Tunachukua fursa hii kueleza kwamba fedha hizi zilizotengwa na zinazotumika kwa ajili ya uchaguzi ni fedha zetu sisi wananchi wa Tanzania. Fedha hizi si za CCM, wala chama chochote kile, hizi fedha za uchaguzi ni fedha za wananchi!

Tumeshuhudia namna gani shilingi bilioni 254.82 zilizotumika kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Kitongoji zilivyoteketea na kutumika kuwezesha uporaji wa haki na demokrasia. Uporaji wa haki na kutokuzingatiwa kwa matakwa ya wananchi kuendelea kuwepo tangu uchaguzi wa 2019 na 2020.

Kwa mwaka mwengine tena tunaenda kwenye uchaguzi tukiwa hatuna matumaini makubwa ya haki na msingi ya demokrasia kuzingatiwa. Tumeamua kuingia kwenye uchaguzi tukiwa na ari ya mapambano; mapambano yetu ni kulinda thamani ya kura na kuhakikisha ustawi wa wananchi.

ACT Wazalendo tunasisitiza kwamba, hatutaki fedha zetu zitumike kuumiza wananchi; hatutaki fedha hii itumike kupora maamuzi ya wananchi, tunataka uchaguzi huru na wa haki abapo vyama vyote vitapata haki na uwanja sawa wa kueleza wananchi nini cha kufanya bila bughudha.

Tunasisitiza na kueleza kwamba haya yanayoitwa mabadiliko ya sheria ya Tume ya Uchaguzi hayaridhishi na hayatoi nuru na mwanga wowote wa kuchochea mabadiliko ya kweli yatakayo hakikisha kufanyika kwa uchaguzi wa haki, kweli na wenye kuaminika.

Hivyo, ACT Wazalendo tunasisitiza madai yetu sita kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025:

Makamishna wa tume huru ya Taifa ya Uchaguzi wapatikane kwa ushindani, tume iitishe mchakato wa usaili sasa kama inavyotamkwa na sheria

Wakurugenzi wa halmashauri wasiwe wasimamizi wa majimbo, Tume iajiri watumishi wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi.

Mawakala wafanye shughuli zao bila bughudha na wasizuiwe

Wagombea wote wasienguliwe, wananchi wapewe nafasi ya mwisho kuamua viongozi wanaowataka.

Pasiwe na Kura Feki, Fedha zetu kama nchi zisitumike kuchapisha na kupitisha kura feki vituoni.

Vyombo vya ulinzi na Usalama visiingilie mchakato wa Uchaguzi.

ACT Wazalendo tunatoa angalizo na onyo kali kwa serikali kutokujihusisha na matendo yanayolenga kupora na kukiuka haki zetu katika uchaguzi huu. Tunasema, Tume ya Uchaguzi sio mali ya CCM na fedha za umma hazipaswi kutumika kuibeba CCM bali kutenda haki iliyokusudiwa.

Tunawahimiza Watanzania kutumia makasiriko na manung’uniko yao dhidi ya CCM kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga na kulinda kura. ACT Wazalendo tumejidhatiti safari kuongoza Mapambano ya kulinda demokrasia na kukabiliana na uhuni wote wa CCM na wadau wake. Tunawaomba wananchi wote tuungane na tuoneshe mshikamano katika kuondokana na ufedhuli wote wa serikali ya CCM ambayo inatudumaza kiuchumi, itafubaza kijamii na inatuchakaza kisiasa.

Tuungane Kuukataa Uhuni! Tuungane Kupiga na Kulinda Kura!


HITIMISHO

Kwa ujumla, Bajeti ya mwaka 2025/26 itapelekea maisha ya mwananchi wa kawaida kuwa magumu zaidi kwa sababu gharama za maisha zitaendelea kupanda na kipato kupungua. Sera za Bajeti zimeshindwa kutazama Bajeti kama Sera (policy instrument) na badala yake imekuwa nyenzo tu ya kukusanya mapato na kuyatumia.

Chama cha ACT Wazalendo kimetekeleza wajibu wake kwa kuonesha matundu na anguko kwenye mfumo wa Bajeti ya mwaka 2025/26 na kuonesha namna bora inayoweza kuleta unafuu wa Maisha ya mtanzania. Ni dhahiri kuwa Watanzania wa kawaida haijawapa unafuu wa maisha na badala yake imeongeza machungu.


​
 
Back
Top Bottom