Waziri Ulega asitisha bunge na kwenda kutizama uharibifu wa miundombinu Morogoro

Waziri Ulega asitisha bunge na kwenda kutizama uharibifu wa miundombinu Morogoro

Sijapewa username bado

JF-Expert Member
Joined
Aug 15, 2024
Posts
1,775
Reaction score
2,891
Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imepanga kutumia kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 30 kwa ajili ya ukarabati wa barabara muhimu za maeneo mbalimbali nchini zilizoharibiwa na mvua.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ametoa taarifa hiyo akiwa mkoani Morogoro alikoenda kwa dharura baada ya mvua kubwa zinazoendelea kunyesha na kuharibu barabara inayounganisha wilaya ya Ifakara – Mlimba kwenda mkoa wa Njombe.

Ulega amesema pamoja na kiasi hicho cha fedha kilichoidhinishwa na Rais kwa ajili ya ujenzi wa dharura, mipango ya serikali ya ujenzi wa kudumu wa barabara na madaraja inaendelea kama ilivyo na haiathiriwi na mipango hii ya dharura.

Ulega aliyelazimika kukatisha kuendelea na vikao vya Bunge vinavyoendelea mkoani Dodoma kwa ajili ya kufanya safari hiyo ya dharura, alifuatana na baadhi ya wahandisi wabobezi nchini kutoka wizarani na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ili wasimamie viwango kwenye ukarabati utakaofanyika.

Kabla ya kuzungumza na wananchi wa Ifakara na viongozi waliokuwepo kwenye eneo la barabara iliyokatika, Ulega alifanya ziara kwa njia ya helikopta akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, kuona athari za mvua kwenye miundombinu ya barabara na madaraja mkoani humo.

Baadhi ya miundombinu ya Morogoro kama madaraja, itafaidika pia na mpango wa serikali wa ujenzi wa madaraja na barabara wa kudumu unaoendelea nchini baada ya miradi yake kuridhiwa na serikali ya Rais Samia.

Baadhi ya barabara za Morogoro zitakazofaidika na mpango huu wa serikali ni Ulanga – Namhanga ambayo imetengewa zaidi ya shilingi bilioni 6.3 na Malinyi mpaka Mto Fulua iliyotengewa shilingi bilioni 12.

Katika taarifa yake kwa Waziri, Malima amesema mkoa wa Morogoro ni mkubwa na maombi yao kwa serikali ni kwamba barabara muhimu zijengwe katika hali ambayo zitaweza kupitika na si lazima ziwe za lami.
 
Back
Top Bottom