Guys Check new development of this story tunaweza kuchangia. Hawa jamaa hawako serious na maisha ya watu !!!
Polisi wahusishwa mauaji ya dereva wa Naibu Waziri
na Happiness Katabazi
JESHI la Polisi nchini linawashikilia watu wanne wakiwemo askari polisi wawili kwa tuhuma za mauaji ya aliyekuwa dereva wa Naibu Waziri wa iliyokuwa Wizara ya Usalama wa Raia, Tumaini Mbaga.
Vyanzo vya habari vya uhakika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi viliiambia Tanzania Daima kwa nyakati tofauti kuwa, wengine wanaoshikiliwa kuhusiana na tuhuma hizo ni raia wawili ambao hawakuweza kuthibitisha iwapo ni watumishi wa serikali ama la.
Habari hizo zinaeleza kuwa, watu hao walikamatwa mapema wiki hii na wanaendelea kushikiliwa na jeshi hilo kwa siri.
"Jeshi limewakamata watu hao mapema wiki hii na linaendelea kuwashikilia kwa mahojiano zaidi, lakini hata hivyo baadhi ya maofisa waandamizi wa jeshi letu wanajitahidi kuendesha jambo hili kwa siri," kilisema chanzo chetu cha habari.
Habari hizo zilieleza kuwa chanzo cha mauaji ya dereva huyo ni wivu wa baadhi ya polisi ambao inadaiwa walikuwa wakichukizwa na aliyekuwa Naibu Waziri wa wizara hiyo, Mohamed Aboud, kuendeshwa na dereva ambaye si polisi.
"Inasemekana baadhi ya madereva wa polisi walikuwa wakikerwa na dereva raia kumwendesha naibu waziri wakati madereva wa Jeshi la Polisi wapo," kilieleza chanzo hicho.
Taarifa za kukamatwa kwa watu hao zililifikia gazeti hili mwanzoni mwa wiki hii na tayari habari zimeanza kuenea mitaani.
Chanzo hicho cha habari kilieleza watuhumiwa hao ambao awali walikuwa wakihifadhiwa katika mahabusu ya jeshi hilo iliyopo eneo la Stakishali - Ukonga, lakini sasa wamehamishwa na haijafahamika wako mahabusu gani.
"Mpaka jana watuhumiwa hao walikwishahamishwa kutoka mahabusu hiyo, lakini hatujui ni wapi wamehamishiwa. Wamekuwa wakihojiwa na kikosi maalumu kilicho chini ya Ofisi ya Rais (Task Force), kikosi hiki kinaundwa na vyombo vya ulinzi na usalama kutoka JWTZ, Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa," kilieleza chanzo hicho.
Habari zaidi zinaeleza kuwa askari wanaotuhumiwa katika tukio hilo ni watatu, lakini mmoja alifanikiwa kutoroka baada ya kupata taarifa ya kufichuka kwa siri hiyo.
Miongoni mwa askari waliokamatwa, mmoja anatoka Kituo cha Polisi Msimbazi na mwingine anatoka kitengo cha Upelelezi, Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Mbali na askari hao, pia wapo raia wawili, mmoja wao ni mwanamke ambaye ni raia kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), anayeishi Yombo, jijini Dar es Salaam.
Jana gazeti hili lilifanya juhudi za kuzungumza na Mkuu wa Jeshi hilo, IGP Said Mwema, ili kupata ufafanuzi, lakini halikuweza kuzungumza naye, baada ya simu yake ya kiganjani kupokewa na msaidizi wake, ambaye alieleza kuwa IGP alikuwa kwenye majukumu mengine ya kitaifa nje ya Dar es Salaam.
Aidha, gazeti hili lilifanya jitihada za kuzungumza na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, ambaye baada ya kupatikana hakuwa tayari kuthibitisha au kukataa, zaidi ya kulitaka gazeti hili kuwasiliana na Kamishna wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana kwa ajili ya kupata taarifa za tukio hilo.
Hata hivyo, Kamanda Tibaigana hakuweza kupatikana baada ya simu yake ya mkononi kupokewa na mlinzi wake ambaye aliieleza Tanzania Daima kuwa kamanda huyo alikuwa kwenye kikao ambacho hakufahamu kitamalizika muda gani.
Mwishoni mwa Januari mwaka huu, polisi waliokota mwili wa dereva huyo ukiwa umetenganishwa na kichwa, eneo la Kwembe, ukiwa umeharibika vibaya, ikiwa ni takriban wiki mbili tangu alipotoweka.