SoC04 Wazo bunifu kwa maendeleo ya baadhi ya Wizara katika Serikali ya Tanzania

SoC04 Wazo bunifu kwa maendeleo ya baadhi ya Wizara katika Serikali ya Tanzania

Tanzania Tuitakayo competition threads

Hilali Sadick Mussa

New Member
Joined
Jun 8, 2024
Posts
1
Reaction score
0
1. Ninalo wazo bunifu,
Ila mwenzenu nahofu,
Wapo wenye nia chafu,
Wanoweza nizulia.

2. Ninaposhusha usuli,
Uhusuo serikali,
Wenye hiba na adili,
Wao wataupindua.

3. Watazua yaso mana,
Ambayo sijayanena,
Hivyo nawaomba sana,
Muje nihahakikishia.

4. Ikiwa tatoa wazo,
Lililokidhi vigezo,
Mtakuwa na uwezo,
Kuweza lifafanua.

5. Au mtababaisha,
Mje kunichonganisha,
Nifungwe jela maisha,
Iteseke familia.

6. Sawa, wazo nitawapa,
Ila msiwe na pupa,
Wote murejee hapa,
Niweze waelezea.

7. Tagusa kila wizara,
nikionesha taswira,
Wizara ziweke dira,
Malengo kuyafikia.

8. Nianze wizara mama,
Ulinzi na usalama,
Jama wangefanya hima,
Mipakani wakatua.

9. Kuna wanaoingia,
Bila kufwata hatua,
Na viti wanagombea,
Hili sijui mwajua?

10. Sambe maeneo gani,
Haya yapo mipakani,
Magharibi na kusini,
Na kaskazini pia.

11. Magharibi natongowa,
Ukanda wote wa ziwa,
Wakongomani hutuwa
Na hata Warundi pia.

12. Na mara wanapofika,
Hujifunza kutamka,
Na madaraka hushika,
Tusiweze wagundua.

13. Pia na kaskazini,
Wapo walio nchini,
Jama kiwatathmini,
Wala si watanzania.

14. Wanazuka toka Kenya,
Tena kwa kupenya penya,
Na shughuli wanafanya,
Tukijua ni raia.

15. Kadhalika na kusini,
Zipo jamii fulani,
Zinazokita nchini,
Raia wakaridhia.

16. Jambo hili sio njema,
Kwa nyanja ya usalama,
Wizara ifanye hima.
Kuweza kulizuia.

17. Kwanza itoe elimu,
Kila mtu afahamu,
Uhamiaji haramu,
Si jambo la kuchekea.

18. Pili iwe mipakani,
Hasa hasa milimani,
Maziwa na baharini,
Na njia za kupitia.

19. Na ifanye mikakati,
Ipitie ithbati,
Wanaovuka mageti,
Iweze kuwakagua.

20. Ulinzi taimarika,
Ikiwa watayashika,
Haya niliyotamka,
Na kazi wakatendea.

21. Nije nako TAMISEMI,
Nisije olwa kichomi,
Ni maoni yangu mimi,
Yapaswa kuzingatia.

22. Hii ni wizara baba,
Ina mengi ilobeba,
Majukumuye si haba,
Na si ya kupuuzia.

23. Moja ya lake jukumu,
Ni kuajiri walimu,
Na kuwapa majukumu,
Kisha kuwasimamia.

24. Afya bila kusahau,
Tamisemi ndo mdau,
Huajiri angalau,
Wizaraye yende poa.

25. Nianze na kada hizo,
mbona kwasasa tatizo,
Au hakuna uwezo,
Nyinyi kuzihudumia?

26. Laiti mngefikiri,
Kuna uhaba si siri,
Haraka mungeajiri,
Wakaenda saidia.

27. Kada hizo ni teule,
Zipewe vipaumbele,
Sivyo tutarudi kule,
Zama tulizotokea.

28. Nchi itakosa mwanga,
Watakithiri wajinga,
Magonjwa pia majanga,
Tutashindwa vizuia.

29. Ajirini watu hawa,
Kazini kukae sawa,
Wajapo wahudumiwa,
Wahudumiwe sawia.

30. Swala la miundombinu,
Nimependa nyendo zenu,
Mmezuia upenu,
Watu pesa kujilia.

31. Vituo vya Afya, shule,
Barabara mpaka kule,
Kwa hili kwenu kongole,
Napaswa kuwapatia.

32. Kuna wizara ya pesa,
Nayo ni kiini hasa,
Cha kufungua furusa,
Nchi ikaendelea.

33. Kwenye Bunge la bajeti,
Hi' wizara ingeketi,
Ikafanya mikakati,
Hotuba kuzipitia.

34. Ingalibaini kitu,
Kwenye hilo Bunge letu,
Hotuba zilizo butu,
Zote ingezitambua.

35. Butu kwa makadirio,
Yenye mengi makisio,
Yaso na uhitajio,
Wala tija kwa raia.

36. Ingachambua chambua,
Yaso mana ikatoa,
Wizara lojiwekea,
Ipate kujipigia.

37. Makisio ya kuhodhi,
Toka wizara baadhi,
Ngepembua ingekidhi,
Pesa ilojiwekea.

38. Bado nasitofahamu,
Kwa wizara ya elimu,
Ina yepi majukumu?
Tamisemi ishachukua.

39. Mi naona ingefutwa,
Pesa zake zikaletwa,
Kwayo Tamisemi kutwa,
Inayoisaidia.

40. Na wizara ya madini,
Ingefanya tathmini,
Wawekezaji nchini,
Vipi wanasaidia?

41. Katika kukuza pato,
Na kuondoa msoto,
Ambao ni changamoto,
Nchi inazopitia.

42. Sekta hiyo ni nyeti,
Ingewekwa mikakati,
Madini kuyadhibiti,
Bure yasije potea.

43. Chochoroni sipitishwe,
Yachimbwe yathibitishwe,
Na kisha yaidhinishwe,
Ndipo waweze yatoa.

44. Mikataba ya madini,
Inayofanywa nchini,
Ingewekwa hadharani,
Raia wakatambua.

45. Isiwe madini yetu,
Yanatafunwa na watu,
Pasi na kujali kitu,
Wala kujali raia.

46. Na wizara ya kilimo,
Nanyi pia humu mumo,
Siridhi chenu kipimo,
Bado sijafurahia.

47. Jama mungehakikisha,
Wilaya zinozalisha,
Trekta mungekopesha,
Watu wakajilimia.

48. Ikiwa kuzikomesha,
Kutabana kimaisha,
Wilaya zingekosha,
Kwa bei ilo murua.

49. Na zile jamii duni,
Mngefanya tathmini,
Mbolea zikawa chini,
Nao wakazinunua.

50. Pia katika masoko,
Wajuzwe mtiririko,
Wapi zao lilimwako,
Na wapi wende uzia.

51. Ziboreshwe barabara,
Kilimo kiwe imara,
Wasije pata hasara,
Shamba mazao kufia.

52. Hapo tutaona tija,
Na itatia faraja,
Raia hawatongoja,
Shambani wataingia.

53. Watalima kitaraji,
Wataja pata mitaji,
Wakakuze yao miji,
Na watunze familia.

54. Kuna na wizara hii,
Wizara ya utalii,
Mambo yake yako wii,
Mawimbi inapasua,

55. Wizara imeanzisha,
Chaneli inoonesha,
Ya Tanzania maisha,
Navyo vivutio pia.

56. Kwa hili nawapongeza,
Japo tawaambiliza,
Lugha mngeziongeza,
Tukazidi wavutia.

57. Kadhalika na Nishati,
Siwezi iacha eti,
Hii ni wizara nyeti,
Sote twaitegemea.

58. Inaendesha mitambo,
Sanjari na yetu mambo,
Ya kutafutia tumbo,
Tukiwa tumetulia.

59. Tabu ni shirika lake,
Linafanya tuteseke,
Daima tuwe wapweke,
Mambo kombo kutwendea.

60. Nina langu lalamiko,
Iweje kwa Tanesko,
Kutwa afanye vituko,
Bila nyinyi kukemea.

61. Akate Kate umeme,
Ajione mfalme,
Raia atuandame,
Hali anatukosea.

62. Wanakosea si siri,
Wangetupasha habari,
Watu wakawa tayari,
Mbadala kuandaa.

63. Mengi ya hiyo wizara,
Sio siri yanakera,
Vipi gesi ya Mtwara,
Tusifaidi raia?

64. Gesi ni kizaa zaa,
Kutupa mmekataa,
Tunapokata mkaa,
Bado mnatukemea.

65. Ingekwepo mbadala,
Gesi umeme na sola,
Msingeona pahala,
Misitu tukivamia.

66. Tamati natia koma,
Itoshe niliyosema,
Wizara zingeyapima,
Kazi zikayatendea.

67. Haki tungalifaidi,
Kwa maelfu idadi,
Na tungestaafidi,
Nchi yetu Tanzania.

******** MWISHO*******

Jina la Mtunzi: Hilali Sadick Mussa
Jina la Utunzi: Malenga Mfawidhi
 
Upvote 0
Back
Top Bottom