Tatizo la mjadala wa lugha hapa Tanzania ni ile polarization ambayo inalenga au kukikuza Kiswahili na kupuuzia mengine, au kukikuza Kiingeraza na kupuuzia Kiswahili. Watu wanaotoa mifano ya nchi za Ulaya, kwa mfano, watakuambia kwamba kule wanatumia lugha yao ya Kidachi. Lakini masharti ya shule ni lazima usome lugha nyingine mbili kikiwemo Kiingereza. Zingatia hapo: Lugha yao kwanza, na lugha nyingine ni lazima.
Isitoshe, wanafunza hizo lugha nyingine kikweli si kubabaishaji. Mjadala wa lugha hapa TZ mara nyingi unasahau kwamba kwa miongo mingi sana, lugha zote mbili Kiingereza na Kiswahili zimefundishwa vibaya mno au hazikufundishwa kabisa pengine. Kuna wakati tulikuwa tunajaza vyuo vya ualimu vijana waliofeli masomo yote, kikiwemo Kiswahili. Watu hao ndiyo walioenda kufundisha baadae katika shule za msingi. Uzoefu wangu ni kwamba hata sekondari walimu wengi hawana ujuzi wa kutosha kufundisha Kiswahili. Achia Kiingereza, Kiswahili tu kwanza hakifundishwi vema.
Nimebahatika kuona mfumo wa elimu huko Marekani pia. Katika vyuo vikuu huko, wanafunzi kwanza lazima wasome madarasa kadha ya Kiingereza (lugha yao), wanajizatiti katika stadi mbalimbali: reading, college writing, etc Sasa turudi kwetu TZ, Kiswahili kilishatupwa baada ya Form IV kwa kiwango ambacho hawajakisoma vizuri. Na Kiingereza, je? Tumewaachia mangwini chuoni maana hawana jingine la kufanya. Halafu tukienda nje Kiingereza kikatugonga, tunasingizia Kiswahili ndiyo kimeleta taabu hiyo.
Nahitimisha, lugha ya kwanza kutiliwa mkazo ni Kiswahili. Wanafunzi wakijifunza Kiswahili vizuri wataweza kuhamishia stadi zao kwenye Kiingereza, Kifaransa, Kiarabu, Kireno, nk. Kwa hakika tunahitaji lugha kama tatu na si mbili tu. Nitoe mfano tu mdogo. Kuna watu wanamaliza vidato na hawajui sentensi ni kitu gani, hawajui jinsi ya kusoma haraka haraka upate pointi, hawajui jinsi ya kuandika muhutasari, nk. Fikiri mwenyewe kama mtu amepata stadi hizo ktk Kiswahili, ni rahisi sana kuhamishia kwenye lugha nyingine.
Mjadala usifinywe kwenye Kiswahili au Kiingereza, bali namna gani tunaweza kupangilia mafunzo yenye kuleta ufanisi na ustadi katika lugha tatu na zaidi.