Mtetezi wako yu hai na hatimaye atasimama kukutetea, Mungu ni mwenye haki na hata kuacha kamwe!! Mungu anajua mwanzo na mwisho wa maisha yako, Mungu anakuwazia mawazo ya Amani. Hakupendi huyo lakini Mungu anakupenda sana, hakupendi huyo lakini wazazi wako, kaka na dada zako na rafiki zako wanakupenda.
Usihangaike na kiburi chake, hakuna marefu yasiyokuwa na ncha, na siku zote mbio za sakafuni huishia ukingoni. Huyo hakuwa mume wako, hakufai wala usijute kama kaweza kutamka kwa kinywa chake hakupendi Mshukuru Mungu lazima kuna jambo anakuepusha nalo.
Jitahidi kunyamaza wala usijibizane naye, wala usimlaumu kwa sasa, mimina moyo wako kwa Mungu, tulia jipe muda wa kumtafuta Mungu kwa bidii utapona na utapata neema ya kupita salama katika hilo jaribu.
Hebu ona kama hayo yote ni mapito tu, upo wakati wa furaha unakuja kwako, unajua dhahabu haiwezi kuwa dhahabu mpaka imepita kwenye moto, wewe ni dhahabu, ukitulia sasa nina uhakika utakuwa umejifunza mengi utakuwa msaada kwa watu na utaimarika zaidi kiakili na kiroho pia.
Kataa hiyo roho ya mauti kabisa, huo ni mpango wa adui, fikiria hata ukifa unafikiri yy atapata faida? Hapana kwanza hakupendi, mtoto wako, na ndugu zako ndio wataumia. Haijalishi kakupotezea muda kiasi gani, Mungu ni mwenye haki na anahukumu kwa haki. We msamehe, muachie Mungu ashughulike naye mwenyewe, wakati ukifika atajutia maneno yake....wakati yy anajuta ww umeshapona na unaendelea na maisha yako.
Ngoja niishie hapa dada, lakini ninakuombea, najua unachopitia, najua unavyoumia lkn kwa usalama wa afya na akili yako, lia na Mungu tu, utaona neema ya ajabu.