Nimesoma kwa makini sana waraka alioandika mtu anayejiita mchambuzi kuhusu lile analodai kama ufisadi kwenye sekta ya Sukari. Katika maelezo yake, mtu huyu mbali na kuwataja viongozi wakuu wa serikali katika porojo lake hilo, hakuainisha ushahidi wowote unaoweza kuthibitisha hoja alizozitoa.
Lakini kikubwa nilichokiona hapa, mtu huyu hana uelewa hata kidogo wa sekta ya sukari nchini, historia yake, na kukua kwake mpaka kufikia hapa leo hii. Mtu yeyote makini akisoma porojo hii atagundua mara moja kuwa hii ni stori ya uongo, uzushi, na imejaa uzandiki wenye lengo la kumchonganisha Mheshimiwa Rais na watendaji wake wakuu ndani ya serikali, wananchi, na wawekezaji kwa nia ya kuua uchumi wa nchi. Lakini pia mtu huyu akijua fika anaandika habari za uongo tena kwa Mheshimiwa Rais, ameshindwa hata kutaja jina lake halisi, basi angalau angewataja waliomtuma.
Sasa hebu nianze kwa kumchambua mwandishi anayejiita mchambuzi katika hoja alizoziongelea. Hoja zake zimegusa maeneo yafuatayo; ulanguzi katika bei ya sukari, ufisadi uliopo katika bidhaa hiyo, kundi dogo la wazalishaji lisilo rasmi linalodhibiti upatikanaji wa bidhaa hiyo nchini, na utolewaji wa vibali vya sukari nchini.
Nirudi nyuma kidogo nimfahamishe mtu huyu kwa faida yake na kwa faida ya waliomtuma kwamba nchi yetu imetoka katika athari kubwa ya uhaba wa sukari kabla serikali haijaamua kubinafsisha viwanda vya sukari nchini. Ni dhahiri kwamba wazo la serikali la kubinafsisha viwanda hivyo na kuwaruhusu wawekezaji kuwekeza katika sekta hiyo ngumu nchini limeikomboa nchi yetu kutoka uzalishaji mdogo usiotosheleza mahitaji ya nchi na mpaka kufikia leo nakisi ya uzalishaji imebaki kidogo sana.
Ni miaka michache tu iliyopita, serikali ilikuwa ikitoa vibali vya kuagiza sukari kutoka nje ya nchi kwa zaidi ya tani 150,000 kila mwaka ili kufidia nakisi ya uzalishaji wa bidhaa hiyo nchini, lakini leo hii nakisi hiyo imepungua kutoka tani 150,000 mpaka tani 20,000 tu kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji nchini. Haya ni mafanikio makubwa na ya kujivunia yanayotokana na sera na dira ya serikali katika sekta hii muhimu.
Kumthibitishia mchambuzi huyu, toka nchi yetu ilipopata uhuru, si yeye wala hao wafanyabiashara anaowasemea walithubutu kuwa na ujasiri wa kuwekeza katika sekta hiyo ngumu sana nchini. Wengi wao wanataka utajiri wa haraka haraka kujipatia vibali vya uagizaji wa sukari kutoka nje ya nchi jambo ambalo linadhoofisha uchumi wa Tanzania na kuifanya kuwa tegemezi katika bidhaa hiyo.
Mchambuzi anadai eti kuna ulanguzi katika bei ya sukari. Katika maelezo yake anadai kwamba ulanguzi huu unafanyika kwa njia mbili; ya kwanza ni kuamua ni kiasi gani sukari izalishwe lakini pili ni kupandisha bei kwa kudhibiti kiwango cha supply na demand. Ambacho hakielewi mchambuzi huyu ni kwamba uzalishaji wa sukari nchini unapangwa na kudhibitiwa na serikali ukizingatia uwezo wa viwanda vyote katika kuzalisha bidhaa hiyo ili kukidhi azma ya serikali ya nchi kujitosheleza katika uzalishaji wa bidhaa hiyo miaka michache ijayo.
Sijui kama mtu huyu anatambua takwimu za uzalishaji nchini. Kwa sababu, Ikiwa viwanda vimeongeza uzalishaji mpaka kufikia nakisi ya tani 20,000 tu kwa mwaka kutoka tani 150,000, huyu mtu anapata wapi ujasiri wa kusema kwamba viwanda vinaamua kuzalisha sukari kidogo kwa lengo la kupandisha bei? Mantiki ya hoja yake hii iko wapi? Kwa kumsaidia mchambuzi huyu, aende Bodi ya Sukari ili apewe takwimu za ongezeko la uzalishaji sukari kila mwaka kwa kila kiwanda. Kwa mujibu wa takwimu hizo, uzalishaji unaongezeka kwa kasi kila mwaka. Kwa hiyo hoja kwamba wazalishaji wa sukari wanapanga kiwango cha uzalishaji wa sukari kwa lengo la kupandisha bei ni uzushi na uongo uliopitiliza mipaka.
Wakati tukisherehekea miaka 60 ya uhuru wa nchi yetu bado Tanzania ina viwanda vinne tu vya sukari vinavyozalisha bidhaa hiyo nchini. Hii ni ishara tosha kwamba eneo hili ni gumu kuwekeza na inahitaji ujasiri na uzalendo wa kutosha kujitoa mhanga katika sekta hii. Vinginevyo kama huko kungekuwa na faida hiyo anayoisema mtu huyu , tayari tungekuwa na wawekezaji lukuki kwenye kilimo na viwanda hivi. Ila kama ni kuagiza tu kutoka nje ya nchi, basi kila mtu anaweza kufanya hivyo japo madhara yake ni makubwa katika kudhoofisha uchumi wa nchi yetu na hilo ndio lengo la mtu huyu na wale waliomtuma.
Sukari ni bidhaa inayotokana na mfumo wa uzalishaji kiwandani. Duniani kote, malighafi (production inputs) za uzalishaji sukari zinafahamika. Hivyo basi Bei ya sukari inatokana na gharama za uzalishaji na sio vinginevyo. Ni mwaka huu huu tumeshuhudia bei ya mafuta ya dizeli ikipanda kutoka shilingi 1,650/= kwa lita mpaka shilingi 2,450/=. Hili ni ongezeko la zaidi ya asilmia 48%. Bei ya pembejeo zote za kilimo, kuanzia mbolea, madawa ya kuua wadudu n.k, zimepanda kwa zaidi ya 100%. Hapo sijazungumzia upatikanaji wa umeme na bei yake.
Mtu huyu anathibisha uelewa wake mdogo katika sekta hii pale anapowaita wazalishaji wa sukari kama kundi dogo lisilo rasmi. Cha kwanza ni muhimu aelewe kwamba waliojiotoa mhanga kuingia katika sekta hii ni wachache mno japo na yeye kama kweli ana uchungu na uzalendo wa nchi hii, ajiunge kwa kufungua kiwanda na kulima miwa ili kuzalisha sukari lakini sio kupiga porojo mitandaoni. Lakini pili, wazalishaji wana umoja wao rasmi na uliosajiliwa kisheria na serikali unaojulikana kama (Tanzania Sugar Producers Association – TSPA) na una viongozi wake rasmi kwa utaratibu waliojiwekea.
Turudi kidogo kwenya uongo wa mtu huyu kuhusu vibali vya kuingiza sukari nchini. Ikumbukwe kuwa hapo awali zoezi za uingizwaji sukari ya nakisi lilikuwa mikononi mwa wafanyabiashara. Lakini kwa kukosa uaminifu walianza kuleta sukari nchini kiholela zaidi ya kiwango kilichohitajika kwa wakati huo, kitu ambacho kilikuwa ni hatari kwa ustawi wa viwanda vya ndani. Pili, waliingiza sukari ya viwandani kwa ajili ya matumizi ya binadamu, kitu ambacho ni hatari kwa afya za wananchi. Hivyo serikali iliamua kulikabidhi jukumu hili kwa wazalishaji wa ndani ikiwa na malengo makuu yafuatayo; kwanza ni ukweli kwamba wamiliki wa viwanda, wamefaya uwekezaji mkubwa katika viwanda hivyo, kwa hiyo haitakuwa rahisi wao kujihujumu wenyewe lakini pia watapata fursa ya kuongeza uzalishaji ili kuziba pengo hilo. Pili ni ukweli kwamba kwa kuzingatia maslahi ya wafanyabishara kujitajirisha haraka haraka, ilikuwa ni muhimu kwa serikali kudhibiti uingizaji wa sukari yenye madhara kwa binaadamu. Tatu, ni kutoa fursa ya viwanda hivi kukua ili kukuza uchumi wa ndani, kuongeza ajira ambapo mpaka sasa hivi sekta ya sukari imeajiri moja kwa moja zaidi ya watu laki moja, lakini pia kutimiza lengo la serikali kutaka Tanzania ijitosheleze katika uzalishaji wa sukari ifikapo mwaka 2025.
Nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutambua mchango wa wawekezaji katika kuifanya Tanzania ipige hatua kubwa za maendeleo ya kiuchumi na kutengeneza ajira za kutosha. Katika kipindi chake kifupi cha uongozi, Mheshimiwa Rais, ameonesha dira kwa kuhamasisha na kusimamia uwekezaji nchini. Tunapaswa kumpongeza sana na kumuunga mkono katika dhamira yake hii kubwa kwa maendeleo ya nchi yetu.
Lakini nitoe angalizo; watu wa aina ya huyu mchambuzi wanaotumiwa vibaya na watu wachache kwa maslahi binafsi, wasivumiliwe hata kidogo wala kuachwa kuendelea kuivuruga nchi yetu kwa kuandika maneno ya uchochezi na uongo wenye lengo la kupotosha na kuvuruga misingi endelevu ya uchumi wetu. Aina ya vitendo kama hivi vinaweza kukatisha tamaa wawekezaji wa ndani na nje.
Kwa kumalizia, naishauri serikali kuwa makini na watu wa aina hii ambao wana nia mbaya ya kumchonganisha Mpendwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan na viongozi wakuu wa serikali kwa kuzungumza maneno ya uongo na uchonganishi lakini pia kumchonganisha Mheshimiwa Rais na wawekezaji kwa maslahi yake binafsi. Viongozi wa serikali yetu waachwe wafanye kazi zao za maendeleo ya nchi kwa maslahi mapana ya taifa letu.
Mungu ibariki Afrika. Mungu ibariki Tanzania.