Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza anuai mpya ya COVID-19 iitwayo EG.5 - iliyopewa jina lisilo rasmi "Eris" huku likishauri kila nchi kuchukua hatua mahsusi za kufuatilia uwepo wake.
Lakini shirika hilo linasema inaleta hatari ndogo kwa afya ya umma, bila ushahidi kwamba husababisha ugonjwa mbaya zaidi kuliko lahaja zingine zinazozunguka kwa sasa.
Lakini shirika hilo linasema inaleta hatari ndogo kwa afya ya umma, bila ushahidi kwamba husababisha ugonjwa mbaya zaidi kuliko lahaja zingine zinazozunguka kwa sasa.
- Tunachokijua
- Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa sasa linafuatilia aina kadhaa za anuai mpya za virusi vya COVID-19, ikijumuisha anuai EG.5 inayotajwa kusambaa katika nchi kadhaa duniani.
Huu ni mfululizo wa kutokea kwa anuai mbalimbali za virusi vya COVID-19, ugonjwa ulioripotiwa kwa mara ya kwanza huko Wuhan, Uchina, mwishoni mwa mwaka 2019 na WHO kisha kutangazwa kuwa janga la Dunia Januari 30, 2020.
Anuai (Variants) zingine zilizowahi kuripotiwa kuwepo ni Alpha, Beta, Gamma, Delta na Omicron (BF.7, XBB, BN.1, BF.11)
Agosti 9, 2023, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema kuwa pamoja na uwepo wa anuai nyingi zinazoendelea kutokea hadi sasa, aina ya EG.5 inaonekekana kuwa hatari zaidi kuliko zingine, inaweza kusababisha ongezeko kubwa la visa vya maambukizi na idadi ya vifo.
Sehemu ya hotuba ya Tedros Adhanom Ghebreyesus inafafanua;
"Hakuna shaka kwamba hatari ya ugonjwa mbaya na vifo ni ya chini sana kuliko ilivyokuwa mwaka mmoja uliopita, kutokana na kuongeza kinga ya idadi ya watu kutokana na chanjo, maambukizi au vyote kwa pamoja, na kutokana na utambuzi wa mapema na huduma bora za kliniki.
Licha ya maboresho haya, WHO inaendelea kutathmini hatari ya COVID-19 kwa afya ya umma duniani.
Virusi hivyo vinaendelea kusambaa katika nchi zote, vinaendelea kuua na vinaendelea kubadilika.
WHO kwa sasa inafuatilia anuai kadhaa ikiwa ni pamoja na EG.5, ambayo leo tunachapisha tathmini.
Hatari inasalia kwa anuai hii kuwa hatari zaidi inayojitokeza ambayo inaweza kusababisha ongezeko la ghafla la visa na vifo."
Sifa za anua mpya ya EG.5
Taarifa za kuibuka kwa anuai hii mpya zinakuja miezi 3 baada ya WHO kutangaza COVID-19 kuwa sio Ugonjwa wa dharura ya afya duniani.
Tathmini ya awali ya kusambaa kwake inaonesha kuwa hadi kufikia Agosti 9, 2023, anuai hii imeripotiwa kugunduliwa kwenye nchi 51 duniani ikiwemo China, Marekani, Korea Kusini na Japan.
Aina hii imetoka kwenye familia kubwa ya Omicron, kundi dogo XBB.1.9.2 ambalo sifa zake za kijenetiki zinafanana na aina XBB.1.5 iliyogunduliwa februari 17, 2023.
Muonekano wa EG.5
Uchunguzi wa awali unabainisha kuwa anuai hii ina hatari ndogo, lakini inasambaa na kukua kwa kasi pamoja na kuwa na uwezo wa kukwepa kinga mwili.
Tabia hizi za upekee zinaifanya iwekwe chini ya uangalizi mkubwa ili kuzuia maambukizi mapya yanayoweza kutokea duniani kwa sasa.
Sehemu ya waraka maalum wa WHO inasema;
"Kwa kuzingatia muundo wake wa kijenetiki, uwezo wake wa kukwepa kinga mwili pamoja na kukua kwa kasi, anuai hii ya EG.5 inaweza kusambaa duniani kote na kuongeza idadi ya visa vya maambukizi"
Baadhi ya majaribio yanapendekeza kuwa anuai hii inaweza kukwepa mifumo yetu ya kinga kwa urahisi zaidi kuliko aina zingine zinazozunguka.
Hata hivyo, dalili za maambukizi yake zinabaki kuwa zilezile kama ilivyo kwa wagonjwa wote wa COVID-19.
Jinsi ya kujilinda na EG.5
Kama ilivyo kwa anuai zingine za COVID-19, hatari kubwa ya ugonjwa inabaki juu zaidi kwa watu wazee au walio na changamoto kubwa za kiafya ikiwemo magonjwa sugu.
Kwa mujibu wa WHO, chanjo inasalia kuwa kinga bora dhidi ya mawimbi ya COVID-19 ya siku zijazo, kwa hivyo bado ni muhimu kama hapo awali kwamba watu wachukue dozi zote ambazo wanastahiki haraka iwezekanavyo
Tathimini ya athari za anuai hii kwenye utendakazi wa chanjo ili kutoa maamuzi kuhusu masasisho ya muundo wa chanjo, kama itaonekana kuna umuhimu wa kufanya hivyo.
Mapendekezo 7 ya kukabiliana na Janga hili
Tangu kutangazwa kuisha kwa dharura ya Ugonjwa huu mnamo Mei 5, 2023, Shirika la Afya Duniani limekuwa likitoa miongozo mbalimbali inayolenga kupunguza, ikiwezekana kufuta kabisa janga hili.
Katika kuhakikisha kuwa Dunia inaendana na matakwa ya sasa, hasa baada ya kugundulika kwa anuai EG.5, WHO imetoa mapendekezo mengine 7 yaliyofafanuliwa hapa;
- Nchi zote zinapaswa kusasisha programu zao za kitaifa za COVID-19 kwa kutumia Mpango Mkakati wa Maandalizi na Majibu ya WHO, ili kuelekea kwenye usimamizi endelevu wa COVID-19.
- Nchi zote zinahimizwa kudumisha ufuatiliaji wa ushirikiano wa COVID-19, ili kugundua mabadiliko makubwa katika virusi, na pia mwelekeo wa ukali wa magonjwa na kinga ya idadi ya watu.
- Nchi zote zinapaswa kuripoti data ya COVID-19 kwa WHO au katika vyanzo huria, hasa kuhusu vifo na magonjwa hatari, mpangilio wa kijeni na data kuhusu ufanisi wa chanjo
- Nchi zote zinapaswa kuendelea kutoa chanjo ya COVID-19, hasa kwa vikundi vilivyo hatarini zaidi, ambavyo vina uwezekano mkubwa wa kulazwa hospitalini au kufa.
- Nchi zote zinapaswa kuendelea kuanzisha, kuunga mkono, na kushirikiana katika utafiti ili kutoa ushahidi wa kuzuia na kudhibiti COVID-19.
- Nchi zote zinapaswa kutoa huduma bora zaidi ya kliniki kwa COVID-19, ikijumuisha ufikiaji wa matibabu yaliyothibitishwa na hatua za kulinda wafanyikazi wa afya na walezi.
- Nchi zote zinapaswa kuendelea kufanya kazi ili kuhakikisha upatikanaji sawa wa chanjo, vipimo na matibabu salama, madhubuti na yenye uhakikisho wa ubora wa COVID-19.