UFALME UKIFITINIKA HAUWEZI KUTENGEMAA
Lakini Mafarisayo waliposikia, walisema, Huyu hatoi pepo, ila kwa Beelzebuli mkuu wa pepo. Basi Yesu akijua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, hufanyika ukiwa; tena mji au nyumba yo yote ikifitinika juu ya nafsi yake, haitasimama (Mathayo 12:24–25).
Kuna siku nilisema, kisa cha Kaini na Habili kina mambo mengi na kinatuachia maswali mengi tu ambayo tukitafakari vizuri tunaweza kuona kwamba tabia hizo zipo hata miongoni mwetu!
Maana kilichomfanya amuue ndugu yake wivu uliomjia baada ya kuona sadaka yake imekataliwa. Wakati ule niliuliza swali hili: Je, baada ya kumuua ndugu yake, sadaka yake ilikubaliwa? Kukataliwa kwa sadaka yake hakukuwa na uhusiano wowote na Habili.
Katika mistari ya leo tunasoma sehemu ya mjadala mrefu katika ya Yesu na Wayahudi, hasa mafarisayo na wengine waliokuwa na vyeo katika dini ya Kiyahudi. Walimwona Yesu anatoa mapepo. Na inaonekana waliona sio jambo la kawaida kabisa! Huenda walijaribu nao pian a wakashindwa! Badala ya kuomba msaada ili wajifunze ni kwa nini walishindwa, walifikia hatua ya kumchafua Yesu ili kwamba hata yeye aonekane kuwa hawezi. Wanachokifanya ni kwamba wanasema hatumii nguvu za Mungu, bali nguvu za Beelzebuli, jina jingine la mfalme wa giza, yaani shetani!
Yesu anawashangaa kwamba wamefika huko! Sipendi kujadili sana habari zao, lakini nataka tujifunze kitu hapa! Mafarisayo na Yesu, kwa namna moja au nyingine walikuwa katika kundi moja la imani! Walimwamini Mungu, hata kama kwa viwango tofauti. Mafarisayo wanapoona Yesu anafanya vizuri zaidi, huku wao wakishindwa, inawapa shida! Sio tu kwamba wanaona wivu, bali ule wivu wao unatunga mimba na utazaa huko mbele!
Yesu anawaambia, ufalme ukiftinika, hautasimama. Utaanguka tu! Tulio wengi ni wapenzi wa mpira, tuseme habari za simba na Yanga ndio habari ya mjini! Mchezaji aliyepambwa kwenye vichwa vya habari sasa ni Mzambia, Chama. Wachezaji wenzake wanajua kuwa kijana anaujua mpira. Hata wapinzania wanalijua hilo, ndio maana wanamtaka katika timu yao. Sasa, itokee kwamba timu ya simba ikiwa inacheza, Chama akawa na mpira, wachezaji wa Simba badala ya kumsapoti na kutafuta vyumba ili awapasie, wao wanakwenda kumkaba na kumpiga mtama! Tufanye ameumizwa! Sijui atatolewa nje? Hata kama atabaki uwanjani, spirit ya timu iko wapi?
Yesu anaonesha kuwa ibilisi na wafuasi wake yuko vizuri kuliko wafuasi wa Mungu! Ibilisi hawezi kujishambulia. Akifanya hivyo, ni strategy kama sio viini macho! Lakini wafuasi wa Mungu, habari iko tofauti. Tusipoona athari ya mengi tuyasemayo na kuyafanya dhidi ya wafanyakazi wenzetu au wakristo wenzetu, tutaendelea kuhatarisha ustawi wa ufalme wa Mungu kupitia huduma na taasisi tunazozihudumu. Mungu atufumbue macho. BWANA AKUBARIKI leo na siku zote. Amen [emoji2399] Gerson Mgaya.
Sent from my SM-A715F using
JamiiForums mobile app