1. Kumpata mwenza bahati, siku hizi ni adimu,
Nakupongeza kwa dhati, machangu sikuhujumu,
Shika sana lake shati, peke yake ndo adhimu,
Hongera na Mungu akujalie uvumilivu na upendo.
2. Maisha kama safari, uchumba kituo kimoja,
Mwanzo hauna shubiri, wambea najikongoja,
Chai yenye sukari, maisha yenye faraja,
Hongera na Mungu akujalie uvumilivu na upendo.
3. Uvumilivu muhimu, mapenzi geuka ndimu,
Kila siku si karamu, waweza ishiwa hamu,
Tabia mfano wa bomu, tahadhari ufahamu
Hongera na Mungu akujalie uvumilivu na upendo.
Ndoa zingine maziwa, huishi wewe kunyonywa,
Miaka inavyozidia, wazidi kudanganywa,
Hata kile kilojaa, huishia kumumunywa,
Ndoa zingine kunyonywa, na huku unadanganywa.
Kwa dini au sheria, harusi yenu hufanywa,
Ahadi mtazitoa, mkatae kusengenywa,
Na mafunzo mtapewa, na wazazi mkakanywa,
Ndoa zingine kunyonywa, na huku unadanganywa.
Ukweli hujifichua, wakati mnap0ofinywa,
Maslahi kupungua, kila pembe mnaminywa,
Hali zinapotitia, watu rahisi kugawanywa,
Ndoa zingine kunyonywa, na huku unadanganywa.
Ndugu na hao jamaa, ya uongo hutawanywa,
Hubakia kuvizia, yatangazwa yasiyofanywa,
Na mitego husambaa, wategwe wasiokanywa,
Ndoa zingine kunyonywa, na huku unadanganywa.
Hodari walioamua, milele kutokugawanywa,
Kisha wakajititimua, wasiwe watu wa kunywa,
Fedha kudundulizia, waache tena kunyonywa,
Ndoa zingine kunyonywa, na huku unadanganywa.
Kuwekeza wakitua, vinginevyo wakatonywa,
Mke anapoamua, hataki tena kunyonywa,
Mbele akavichukua, huku mume anasonywa,
Ndoa zingine kunyonywa, na huku unadanganywa.
Mme chumvi hudaiwa, na chake kikamenywa,
Bahili mke akawa, sio wa kumumunywa,
Mme nguvu hulegea, asitake kutekenywa,
Ndoa zingine kunyonywa, na huku unadanganywa.
Ndoa jambo maridhia, ila pasiwe kunyonywa,
Nikahi kitu murua, mtu asiposengenywa,
Nyumba hujititimua, na watu msipogawanywa,
Ndoa zingine kunyonywa, na huku unadanganywa