BigTall
JF-Expert Member
- Mar 9, 2022
- 706
- 1,716
Mnamo Agosti 12, 2024, aliyekuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro, alifika eneo la Tegeta Wazo kufuatia malalamiko ya wananchi waliodai kuwa Uwanja wa Panga, uliokuwa ukitumika kwa shughuli za michezo na kijamii, ulikuwa umeanza kuchimbiwa mashimo ya msingi bila ushirikishwaji wa jamii husika.
Waziri alikutana na wananchi wa eneo hilo na kuafiki hoja zao, akieleza kuwa kilichokuwa kinafanyika kilikuwa kinyume na utaratibu. Aidha, alisema kuwa alikuwa ametumwa na Rais kufuatilia suala hilo.
Katika mazungumzo yake mbele ya kamera, Waziri alitoa saa 72 kwa wahusika waliokuwa wakichimba msingi waliodai kuwa walikuwa wakijenga shule, aliwataka kusitisha shughuli hizo, kusawazisha eneo lililochimbwa na kuurejesha uwanja katika hali yake ya awali ili uendelee kutumika kama ulivyokuwa.
Hata hivyo, baada ya agizo hilo, eneo hilo lilibaki na mashimo kwa zaidi ya miezi mitano bila maelekezo ya Waziri kutekelezwa. Baadaye, ilionekana mkandarasi akirejea na kuendelea na ujenzi kwa kasi huku eneo hilo likiwa chini ya ulinzi maalum wakati wote ambao ujenzi ulikuwa ukiendelea.
Kwa sasa, eneo lote la uwanja limejengwa. Vijana waliokuwa wakilitumia kwa mazoezi na michezo sasa wanahangaika kutafuta sehemu mbadala. Badala ya kuwaona uwanjani, mara nyingi unawakuta wakikaa vijiweni wakipiga soga au wakijihusisha na shughuli zisizo na tija katika muda ambao hapo awali walikuwa wakifanya mazoezi.
Wizara ya Michezo na TAMISEMI wako wapi?
Hizi ni taasisi muhimu zenye wajibu wa kulinda na kuendeleza maeneo ya michezo na shughuli za kijamii. Hata hivyo, zinaonekana kuwa kimya wakati maeneo mengi ya wazi, ikiwemo viwanja vya michezo na vile vilivyokuwa vikitumika kwa shughuli za kijamii, vinaendelea kubadilishiwa matumizi bila kuwepo kwa maeneo mbadala kwa jamii.
Mfano mwingine
Kwa sasa, viwanja kama Biafra (Kinondoni), Sahara (Mabibo-Ubungo) na Uwanja wa Kiwalani Hospitali, miongoni mwa vingine, tayari vimeanza kutumika kwa shughuli tofauti bila ushirikishwaji wa wananchi. Hata kama viwanja hivyo vinamilikiwa na taasisi mbalimbali, vimekuwa sehemu muhimu ya historia na ustawi wa jamii. Kwa hiyo, mabadiliko yoyote ya matumizi yanapaswa kufanyika kwa uwazi na kwa kushirikisha wananchi.
Natoa wito kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) kufuatilia michakato ya kubadili matumizi ya viwanja vya wazi pamoja na viwanja vya michezo ili kuhakikisha sheria na taratibu zinafuatwa.
Vilevile, wito wangu mwingi kwa Serikali kuweka mkakati wa wazi wa kulinda maeneo ya wazi, hususan viwanja vya michezo, ambavyo vina mchango mkubwa katika maendeleo ya kijamii, afya na malezi ya vijana.
Aidha, natoa wito kwa wadau wote wenye umiliki wa viwanja ambavyo kwa muda mrefu vimekuwa vikitumika kwa shughuli muhimu za kijamii ikiwemo viwanja vinavyomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwamba kabla ya kufanya maamuzi ya kuviendeleza kwa matumizi mengine, ni muhimu kuzingatia maslahi ya umma na kushirikisha jamii inayovitumia ili kuepuka migogoro ya kijamii.
Pia soma ~ Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspar Mmuya apiga marufuku uvamizi wa maeneo ya wazi