Hii kauli ya Bumbuli ni kauli ya kichochezi kabisa ambayo ikiachwa ipite hivi hivi bila uwajibishwaji basi tujiandae kwa madhara makubwa sana kwenye soka letu huko mbele ya safari. Na hata kwenye sekta nyinginezo wanaweza kutokea watu wa hovyo kama hawa wasipochukuliwa hatua mapema. Kitendo cha serikali na TFF kukaa kimya mpaka sasa hivi bila kumchukulia hatua Bumbuli inaonyesha jinsi gani watanzania tusivyo makini. Siku zote madhara makubwa husababishwa na vyanzo vidogo. Hivi ina maana ule mkutano wa TFF, Simba, Yanga na Wizara ulikuwa ni bla bla tu. Kwa mtizamo wangu kwa kuwa Bumbuli ameenda "live" kwenye vyombo vya habari basi TFF na serikali kila mmoja kwa wakati wake wangeuhoji uongozi wa Yanga haraka sana iwapo wamemtuma huyo Bumbuli kutangaza kupingana na maazimio ya kikao maalum kati ya Simba, Yanga, TFF na serikali au ni maoni yake binafsi kama Bumbuli. Kama uongozi wa Yanga ndio uliomtuma kupima kina cha maji basi uadhibiwe wote bila kupepesa na kama ni kiherehere chake aadhibiwe huyo Bumbuli mwenyewe kama ilivyotokea kwa Mwakalebela. Je serikali na TFF zinasubiri tena washabiki wafike uwanjani wakute hakuna mechi ndio wachukue hatua? Je waliokati tiketi na kuahidiwa wazitumie kwenye mchezo wa marudiano watafidiwa na nini? Je sheria itafuatwa kwa ukamilifu na Yanga kushushwa daraja? Je iwapo vurugu zitatokea ni nani atawajibishwa?
Wakati mwingine najiuliza sipati majibu. Hivi mfadhili GSM alipoamua kuweka fedha zake kwenye timu kama Yanga alifikiria nini maana nikitizama naona kama kuna ombwe kubwa sana la uongozi hasa uwepo wa watu kama Bumbuli na Mwakalebela. Wakati mwingine wanafanya watu makini kama wakili Simon naye aonekane kama wao tu. Ni wakati sasa wa wanachama, mashabiki na wapenzi wa Yanga kuungana na kwenda kuwashawishi watu makini, wenye weledi na uchungu na Yanga kama Charles Boniface, Ali Mayai, Sekilojo Chambua, Jonas Tiboroha na wengineo waingie rasmi kwenye uongozi wa Yanga hasa ikizingatiwa sasa hivi Yanga ina ufadhili rasmi wa GSM kwa hiyo pesa ipo ila weledi tu ndio umekosekana. Vinginevyo Yanga itabakia inashabikia tu Simba kutolewa na Kaizer kwenye robo fainali ya CL kwa "aggreagate" ya 4-3 ilihali wao wanakimbia kucheza na hiyo Simba. Na iwapo wanaikimbia Simba kwenye mechi ya ligi vipi wakipangwa na Mamemlodi au Al Haly kwenye CL je nako watakimbia?
Kwa maoni yangu masuala yoyote yanayohusu Simba na Yanga ni masuala ya kitaifa kwani yanahusisha watu wengi hivyo basi serikali inapaswa iingilie kati mapema na kuchukua hatua zinazostahiki bila kuogopa wala kumuonea mtu kwani madhara yoyote yakitokea italaumiwa serikali wakati wasababishaji watakuwa wamekaa sebuleni kwao wametulia. Na tuliona kwenye awamu iliyopita baadhi ya viongozi wa soka waliokiuka maadili ya soka na kujihusisha na jinai walichukuliwa hatua na serikali na wala hata FIFA haikuingilia. Na watu aina ya Bumbuli hao wasipewe nafasi kabisa katika soka letu au hata kwenye sekta nyingine kwani watakuwa wanaleta mitafaruku zaidi badala ya kujenga na kuleta maendeleo.