TFF haitambui kufunguliwa Yanga
*Yakataa kupokea faini hadi kamati ikutane
*El-Maamry asema amemaliza kazi yake
Na Suleiman Mbuguni
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limesema halitapokea faini ya dola 20,000 kutoka kwa uongozi wa Yanga, hadi hapo Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo itakapokutana Septemba mwaka huu.
Yanga ilipigwa faini ya dola 20,000 na Kamati ya Nidhamu ya TFF inayoongozwa na mwanasheria Said El-Maamry, baada ya kukata rufani kupinga adhabu ya kufungiwa miaka miwili kucheza michuano ya kimataifa iliyotolewa na Kamati ya Utendaji ya TFF, baada kugoma kupeleka timu kucheza na Simba mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu michuano ya Kagame.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TFF, Fredrick Mwakalebela alisema Sekretarieti ya shirikisho hilo tayari imepokea rasmi uamuzi wa Kamati ya Nidhamu iliyokutana mwishoni mwa wiki, lakini suala hilo litapelekwa kwenye Kamati ya Utendaji kwa kuwa ndiyo iliyoifungia Yanga.
Katibu huyo alisema yeye hawezi kutoa uamuzi wowote juu ya faini ya Yanga na hata kama klabu hiyo ingepeleka faini jana asingeipokea hadi atakapopata mwongozo kutoka Kamati ya Utendaji.
Habari kutoka ndani ya Yanga zilieleza kuwa uongozi wa klabu hiyo, jana ulipanga kupeleka faini hiyo, lakini ikashindikana kutokana na kutokuwa na barua ya TFF ya kuwajulisha juu ya faini hiyo.
Habari hizo zilidai kuwa uongozi huo unasubiri barua hiyo, ingawa habari kutoka TFF zilieleza tayari Yanga imefahamishwa juu ya uamuzi wa Kamati ya Nidhamu kupelekwa kwenye Kamati ya Utendaji.
Alipoulizwa El-Maamry kuhusiana na uamuzi huo wa TFF, alisema tayari kamati yake ilishatoa uamuzi kuhusiana na suala la Yanga, hivyo kama TFF haitaki kupokea faini ni jukumu lao.
Alisema katika uamuzi wao waliipiga faini, waliwapa onyo viongozi wa Yanga na kuitaka klabu hiyo iombe radhi, hivyo kimsingi jukumu lao wamelimaliza na kama TFF itaamua vinginevyo ni wao wenyewe