Kumzungumzia Bernard Morisson mzee wa ndevu za karantini inahitaji tafakuri sana kwani jamaa kila siku anakuja na jipya.
1. Tuanze na Morison mwenyewe. Huyu jamaa vituko vyake tu kwa muda wa takribani miezi sita aliyoishi nchini inatosha kuandika kitabu/vitabu au hata kuandaa filamu. Huyu jamaa mara leo kaipeleka Yanga TFF kuishataki juu ya mkataba wake, mara katoroka kambini kamtishia mlinzi na kisu, mara kagomea tiketi ya kwenda Mwanza, mara kaomba msamaha, mara kapanda boda boda baada ya kutolewa uwanjani ampishe Sibomana, mara kaonekana mchangani anacheza ndondo ili mradi tafarani. Kwa haraka haraka hivi vituko tena kwa mchezaji wa kulipwa toka nje ya nchi nadhani kwa Tanzania huyu ndio kavunja rekodi na itachukua miaka mingi sana kuja tokea mchezaji toka nje kuja kuvunja hii rekodi ya vituko. Lakini hili liwe funzo kubwa sana kwa timu zetu zinapoamua kusajili wachezaji wa kulipwa ziwe kwanza zinatafuta kwanza ripoti za wachezaji husika za ndani na nje ya uwanja na nidhamu zao kabla ya usajili. Pia zisiwe zinawapima tu afya ya mwili bali ziongeze kipengela cha afya ya akili kabla ya kuwapa mikataba.
2. TFF nao wanapaswa kulaumiwa kwenye sakata la Morison na Yanga. Hivi ni kwanini mpaka leo mchezaji akihojiwa na waandishi wa habari anasema kuwa mkataba wake umeisha kwa hiyo anasubiri tu TFF wampe mwongozo ili ajue mweleko wake. Hivi kesi rahisi tu hii ya kusema aidha Morison ana mkataba na Yanga au hana inachukua masaa mangapi kuitolea hukumu? Je TFF itaifidia vipi hasara inayoipata Yanga kutokana na mchezaji kutokuwepo kwenye timu iwapo kweli mchezaji ana mkataba halali na Yanga? N a je vipi kwa Morison naye atafidiwa vipi kuendelea kuingia gharama za kuendelea kubaki hapa Tanzania wakati kwao ni Ghana iwapo itathibitika kuwa mchezaji hana mkataba na Yanga. TFF wamalize hili sakata haraka kila mmoja apewe haki yake. Iwapo ni Yanga apewe haki yake na fidia juu vivyo hivyo ikiwa ni Morison.
3. Vyombo vya habari na waandishi wa habari. Nilitegemea hawa ndio wangetupa usahihi wa tabia za Morison lakini wameshindwa kabisa badala yake wengine walichukua njia rahisi ya kwenda kumhoji akiwa kambini Yanga kinyume na taratibu. Na kwa hili naulumu sana uongozi wa Yanga kwa kutokuchukua hatua yoyote na hata kulalamika tu kwa chombo habari husika/au mwandishi husika kwa mchezaji wao kuhojiwa akiwa kambini. Na je walinzi wa kambi walikuwa wapi?. Nilitegemea vyombo vya habari/waandishi wa habari kwenda Afrika Kusini, Kongo na hata Ghana kufukunyua habari za Morison halafu waje na kabrasha lake tuweze kumjua kwa undani huyu binadamu. Penginepo kuanzia hapo tungekuwa tunafanya shuguli nyingine wala tusingekuwa tunapoteza muda kumzungumzia Morison baada ya kupata taarifa zake na kumfahamu kwa kina yeye ni mtu wa namna gani. Huwa tunaona waandishi wa habari na hata vyombo vya habari vya hapa nchini huwa vinatueletea habari toka mbali huko hata Brazil, France, USA, n.k. lakini kwa hili la Morison hapo Afrika Kusini, Kongo na Ghana vimeshindwa kabisa.
4. Uongozi wa Yanga. Huu mimi nitaulumu moja kwa moja kwa sababu ya kushindwa kutimiza wajibu wake. Sidhani kama ni rahisi tu Morison asajiliwe Yanga halafu aanze kuwapanda kichwani kama anavyoupanda mpira bila ya kuona madhaifu ya hao viongozi. Haiwezekani kwa vituko vyote vile vya kiwango cha lami alivyofanya Morison kabla ya mechi na Kagera Sugar halafu akapandishwa ndege kwenda Mwanza halafu akasafirishwa kwenda Kagera. Je uongozi ulikuwa unaleta picha gani kwa wachezaji wengine wa Yanga? Je Dr. Msola na Mwakalebela kama kweli wana jicho la tatu waliona tofauti gani kwa wachezaji wa Yanga pale Morison alipokuwa uwanjani na pale alipotelewa wakati wa mechi ya Simba na Yanga inaendelea? Mbaya zaidi mpaka leo zaidi ya wiki tangu Morison akatae kukaa kwenye benchi baada ya kufanyiwa "sub" hakuna kiongozi mwenye uwezo wa kumpa adhabu au hata kumuonya kuanzia kwa Dr. Msolla mpaka hata kwa wasemaji wa timu. Kila anayeulizwa anarusha mpira; wakiulizwa wasemaji wanarusha mpira kwenye benchi la ufundi, wakiulizwa benchi la ufundi wanatupa mpira kwa viongozi, wakiulizwa viongozi wanatupa mpira tena kwenye benchi la ufundi.
5.GSM. Hawa wameisadia sana Yanga nawapa hongera sana. Lakini linapokuja suala usajili wa wachezaji wakishamaliza makubaliano basi kuwe na utaratibu mchezaji aende kusaini mkataba kwa viongozi wa timu na mchezaji binafsi ajulishwe kuwa viongozi wa Yanga ndio mabosi wake toka siku anasaini mkataba na ndio atakuwa anawajibika kwao pamoja na benchi nzima la ufundi. Lakini kitendo cha kumleta mchezaji mmeshamalizana huko unakuja unambwaga kwenye timu ndio matokeo nidhamu mbovu za Morison anaacha kupanda mpira anaanza kuwapanda kichwani viongozi pamoja na benchi lote la ufundi na hakuna wa kumchukulia hatua. Kila mmoja anamuogopa kuanzia viongozi mpaka kocha hawajui wafanye nini matokeo yake wanabaki wanarushiana mpira nani wa kumwajibisha Morison. Hivi vituko alivyofanya Morison angefanya Yondani au Ngasa hata robo yake nini kingetokea kama sio kushukiwa kama mwewe kuanzia benchi la ufundi, wasemaji mpaka viongozi. Kwa sasa hata viongozi wa Yanga wakitamani vipi kumuadhibu Morison au hata kumtimua hawawezi mpaka wasilikilizie GSM anaamua vipi. Na yote hii ni kutokana na utaratibu mbovu wa usajili. Kwa hili ni muda muafaka sasa kwa viongozi wa Yanga wakae chini na GSM ili waweke vizuri taratibu za usajili ambazo zitamfanya kila mchezaji pamoja na kuwajibika kwa mfadhili lakini wawe na wajibu kwa viongozi na benchi la ufundi kwa ujumla wake.
Lakini pamoja na vituko vyote Morison kwangu atabaki kuwa bonge la mchezaji. Mpira anaujua sana lakini nidhamu yake mbovu ndio inamuhaharibia sana. Madhara ya kuwa na mchezaji wa aina yake kwenye timu ni kule kushusha sana morali ya wachezaji wenzake ndani ya timu.