Siisemei Yanga, ila naomba kuweka sawa mambo 4. (1) Kuna tofauti baina ya ushirikina na kuamini uchawi. Ushirikina ni kuabudu asiyekuwa Mwenye enzi Mungu, uchawi ni kuamini ama kuogopa nguvu za giza au chochote kisichoeleweka. Timu zetu zinaangukia kwenye hili la pili. Ila haziko peke yao kwenye hilo, kwa hivyo ni ujinga, ushamba na upuuzi kuzibeza timu zetu tu huku tukitukuza wengine wafanyao zaidi ya hayo, kwa sababu tu si Watanzania wala Waafrika. (2) kitendo chochote kinachoipa timu ama mchezaji kujiamini kwenye mchezo wake ni msaada kwa mchezaji na timu hiyo. Muhimu tu kisipingane na ustaarabu, sheria, kanuni na taratibu zetu na za kimpira. (3) Kwa nini wastaarabu wanaolaani ushirikina wa Yanga wasijiulize zaidi mambo rahisi ya msingi: (a) kwa mechi ya Mapinduzi Cup dhidi ya Shaba, je ni kawaida golikipa kubaki na glovu za akiba chini ya goli, hasa ndani ya nyavu? Si vifaa vyote vya akiba vinabaki na wachezaji wa akiba kwenye dawati la ufundi? Marefa ilikuwaje wasilione hilo? (b) Kwa mechi ya Ndanda, ni kawaida golikipa kubaki na chupa ya maji akiwa golini? Na kama ni kwa matumizi yake, kwa nini ayasokomeke nyuma ya nyavu ambako hata kuyafikia ni taabu kwake? (4) Hivi kuondoa glovu ama maji hayo inakuwa ni jambo kubwa kuliko yafuatayo? (a) Michael Jordan alikuwa ni lazima avae kaptura yake ya Chuo Kikuu cha Carlifonia ndani ya bukta ya timu kwenye kila mechi ya Chicago Bulls, jambo lililomlazimisha kuvaa bukta kubwa zaidi kuliko kawaida. Hatimaye bukta hizo kubwa ukawa ndio mtindo wa NBA nzima. (b) kabla ya kila msimu wa Wimbledon, Bjorn Borg aliwacha kunyoa ndevu zake. Akaishia kutwaa taji hilo mfululizo 1976 - 1980. (c) Serena Williams amezoea kuenda na malapa yake ya msalani hadi kwenye uwanja anaochezea mashindano, ni lazima adunde mpira mara 5 kabla ya 'serve' yake ya kwanza na mara 2 kwa 'serve' ya pili. (d)Kolo Toure lazima awe wa mwisho kuingia uwanjani kwenye mechi yoyote. Mechi ya fainali ya Ulaya dhidi ya AC Roma aligoma kuingia mwanzoni mwa kipindi cha pili hadi Gallas aliyekuwa akitibiwa alipoingia. Toure akalimwa kadi ya njano alipoingia baada ya hapo. (e) John Terry kwenye kila mechi huegesha gari yake mahali hapohapo, anatumia vikinga ugoko hivyohivyo kwa miaka 10 mfululizo mpaka vilipopotea kwenye mechi ya ugenini dhidi ya Barcelona. (f) laurent Blanc alikuwa akibusu upara wa golikipa wake Barthez kabla ya kila mechi ya Kombe la Dunia 1998. (g) wakati mmoja Pele alimvulia jezi shabiki mmoja baada ya mechi. Mechi zilizofuata kiwango chake kikaonekana kupungua, mpaka alipomwomba rafiki yake kuifuatilia jezi hiyo. Baada ya hapo mambo yakajipa tena, ingawa kuna habari kwamba jezi aliyorejeshewa haikuwa ileile. (h) Kipa Sergio Goycochea wa Argentina alikuwa akikojoa kiwanjani kila ulipofikia wakati wa penalti tanotano. Akaitoa Yugoslavia kwenye robo fainali ya Kombe la Dunia 1990, akaitoa na Italia kwenye nusu fainali. Wakazitoa Columbia na Brazil kwenye kombe la Marekani Kusini 1993. (i) Rais wa klabu ya Piza alikuwa akimwaga chumvi kabla ya kila mechi ya mashindano kiwanjani kwao, dhidi ya watani wao wakubwa wa Cesena alimwaga kilo 26 nzima. Na kadhalika. Na kadhalika. Kwa nini iwe nongwa kufanyika hapa kwetu tu, tena madogo kuliko hayo? Acheni hizo!