Mkurugenzi wa Yas Zanzibar, Ndugu Aziz Ali Said akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi uliofanyika jana Zanzibar.
Katika hatua nyingine ya kuimarisha na kuendeleza nafasi yake kama kinara wa mapinduzi ya kidijitali nchini, Kampuni ya Mawasiliano ya Yas imezindua rasmi kampeni ya “Anzia Ulipo” visiwani Zanzibar.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika leo tarehe 10 Juni 2025, Mkurugenzi wa Yas - Zanzibar, Ndugu Aziz Ali Said, amesema kampeni hiyo ni mwendelezo wa dhamira ya Yas kumuwezesha kila Mzanzibari kutimiza ndoto zake kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
“Anzia Ulipo ni zaidi ya kauli mbiu – ni mwaliko kwa kila kijana, kila mfanyabiashara mdogo, kila mbunifu – kuanza pale alipo, kutumia alichonacho, na kufikia anakotamani. Tunaamini kuwa ndoto hazihitaji kusubiri wakati maalum au mazingira spesho; wakati sahihi ni sasa,” amesema Aziz mbele ya wadau, waandishi wa habari na washirika wa maendeleo waliohudhuria uzinduzi huo.
Katika hotuba yake, Aziz amepongeza jinsi ambavyo chapa za Yas na Mixx by Yas zimepokelewa kwa mikono miwili na Wazanzibari, na kuwa tayari zimetambulika kama alama ya matumaini mapya, ubunifu, na fursa visiwani humo.
Ameeleza kuwa Yas imeendelea kuwekeza kwenye miundombinu imara ya kidijitali ikiwemo mtandao wa kasi wa 4G na 5G unaopatikana kote Tanzania Bara na Visiwani, hali inayowezesha sekta muhimu kama elimu, afya, biashara na kilimo kustawi kwa kutumia teknolojia.
“Leo hii tunaona vijana wengi wakianzisha biashara zao mtandaoni, wakitengeneza maudhui ya ubunifu, wakitumia teknolojia kwenye kilimo na hata kubuni mavazi. Haya yote yanawezekana kwa sababu ya miundombinu na huduma zenye tija tulizojenga,” aliongeza.
Kampeni ya Anzia Ulipo inalenga si tu kuhamasisha matumizi ya teknolojia miongoni mwa Watanzania, bali pia kutoa msukumo wa kisaikolojia na kimaendeleo kwa wale wanaohisi hawana mwanzo. Kupitia huduma mahususi za Yas pamoja na bidhaa bunifu, kampeni hii inalenga kuwapa Watanzania silaha sahihi za kubadilisha ndoto kuwa halisi.
Aidha, Aziz alisisitiza kuwa Yas itaendelea kuwa mshirika wa karibu kwa kila Mzanzibari katika safari ya kutafuta mafanikio kupitia nguvu ya kidijitali.