Nimefanikiwa kufika mara kadhaa katika Zahanati hiyo na kugundua mambo ambayo ni vizuri nikishea na Wana JF inaweza kuwa na faida kwa Jamii kwa maana ya mamlaka husika kuchukua hatua ili kusaidia wanaopata huduma n ahata wanaotoa huduma hapo:-
Zahanati hiyo ina Daktari mmoja, Muuguzi mmoja na Daktari wa Maabara mmoja inafanya kazi siku na saa za kazi tu.
Mnamo Desemba 9, 2024 nilifika eneo hilo na kukuta kina mama wakisubiri huduma ya Kliniki ya Watoto, pia kulikuwa na Mzee mmoja ambaye alikuwa na jeraha usoni.
Siku hiyo hakukuwa na huduma kwa vile ilikuwa Sikukuu, alipigiwa simu Muuguzi hakupokea, baada ya saa kadhaa akaja Daktari wa Maabara akawakuta wahitaji hao ambao walipouliza kama wanaweza kupata msaada akasema kuwa siku hiyo ni mapumziko huduma hadi kesho yake.
Desemba 14, 2024 nilirudi kwa mara nyingine katika Zahanati hiyo na kukuta mama mjamzito akiwa chumba cha Leba anasubiri kujifungua.
Daktari aliyekuwepo alimuona Mwanamke huyo baadaye akaaga kuwa anaelekea Mnadani, nilifanikiwa kuingia humo ndani na kuzungumza na Mwanamke huyo.
MAZINGIRA
Pamoja na kwamba Zahanati hii imejengwa kwa takriban miaka 20 iliyopita, mazingira ya sasa ni duni mnoo.
Kuna uchakavu wa vifaa tiba vingi ikiwemo mpira wanaolalia Wajawazito wakienda Kliniki.
Mazingira ya chumba cha kujifungulia yanahuzunisha sana, kitanda kimoja tu, endapo kuna wamama zaidi ya mmoja wanatakiwa kujifungua kwa wakati mmoja wanafanyaje?
Mfano kuna muda nikiwa nje ya chumba hicho, mwanamke aliyekuwa anasubiri kujifungua alikuwa akigugumia maumivu nilimsikia na nilihisi anahitaji msaada, nikamsikia anatapika nikaingia kumsaidia huku nikimwita ndugu yake aje kumpa msaada wa karibu.
WAHUDUMU
Zahanati hii ina wahudumu wachache, kwa mfano mama mjamzito niliyemkuta Desemba 14, 2024 alikuwa akihudumiwa na Daktari huku nesi hakuwepo.
Mbali na kutoa huduma hiyo, Daktari pia alikuwa na mishe zake, hivyo hakuweza kukaa hapo muda wote kusubiria hadi mama huyo ajifungue, alimuacha na yeye akaendelea na mambo yake kwa maelezo kuwa atarudi kumuona baadaye. Sasa je akipata dharura atasaidikaje?
Tutawezaje kumaliza hatari ya kupoteza mama na mtoto ikiwa mama hapati uangalizi wa kutosha akiwa anasubiri kujifungua?
Barabara yenyewe kufika eneo hilo la Zahanati ni changamoto, usafiri wa uhakika uliopo ni bodaboda tu.
HITIMISHO
Tunajua Serikali ina macho ya kufuatilia na masikio ya kusikia yote yanayoendelea nchini. Naomba watupe jicho lao kwenye Zahanati hii kwa kuisadia kuongeza wahudumu wa afya, vifaa tiba na majengo mengine kwa manufaa ya Wananchi wake wa Mtamaa.