Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 5,352
- 15,876
Ayoub alieleza hayo wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Jimbo la Chaani katika Kikao cha Kawaida cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja kilichofanyika katika Ofisi za CCM Wilaya ya Kaskazini B, Mahonda.
Kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ndugu Iddi Ali Ame, ambapo majimbo yote ya Mkoa wa Kaskazini Unguja yaliwasilisha taarifa za utekelezaji wa Ilani katika maeneo yao.
Katika taarifa yake, Mhe. Ayoub alisema moja ya azma kubwa ya kuomba ridhaa kwa wananchi wa Jimbo la Chaani ilikuwa ni kuhakikisha ustawi wa wananchi unaimarika sambamba na kasi ya ukuaji wa uchumi wa taifa.
Alisema tathmini ya Taifa ya Hali ya Uchumi wa Kaya (Household Budget Survey) imeonesha kuwa Wilaya ya Kaskazini A Unguja ni miongoni mwa maeneo yenye changamoto kubwa ya umasikini, ikiwa ni ya pili kwa kiwango cha umasikini, jambo lililosababisha kuwekwa kwa mkazo katika kuwasaidia wananchi wanaokabiliwa na mazingira magumu.
Alieleza kuwa katika hatua zilizochukuliwa, zaidi ya kaya 4,900 kati ya kaya 6,500 zilizopo katika Jimbo la Chaani zimefikiwa kwa kupatiwa msaada wa chakula, kitoweo na mavazi.
Kwa mujibu wa Mbunge huyo, jumla ya Shilingi milioni 186,452,000 zimetumika katika utekelezaji wa mpango huo, kiasi ambacho ni sawa na asilimia 45 ya fedha zote zilizotumika katika shughuli mbalimbali za maendeleo ndani ya Jimbo la Chaani katika kipindi cha miezi nane ya utekelezaji wa shughuli hizo.
Aidha, Ayoub alisema pamoja na hatua hizo za kusaidia wananchi wenye uhitaji, juhudi zinaendelea kuelekezwa katika kuwawezesha wananchi kujitegemea kiuchumi kupitia shughuli za uzalishaji, hususan kilimo ambacho ni tegemeo kubwa kwa wananchi wengi wa jimbo hilo.
Alisema wananchi wa Jimbo la Chaani kwa kiasi kikubwa wanategemea shughuli za kilimo, hivyo maandalizi yanaendelea ya kuandaa andiko la mradi wa kilimo pamoja na kuanzisha SACCOS ya wakulima itakayosaidia upatikanaji wa pembejeo, huduma za ugani na mitambo ya kilimo kwa wakati ili kuongeza tija.
Kikao cha Kawaida cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja kiliendelea na mjadala wa taarifa za utekelezaji wa Ilani kutoka majimbo yote ya mkoa huo, kwa lengo la kutathmini hatua zilizofikiwa na kuweka mikakati ya kuongeza kasi ya maendeleo kwa wananchi.