Zanzibar: 25 matatani kufanya biashara bila leseni

Zanzibar: 25 matatani kufanya biashara bila leseni

Suley2019

JF-Expert Member
Joined
Oct 7, 2019
Posts
2,203
Reaction score
5,610
Watu 25 wakiwamo mameneja mauzo wa baa wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kufanya biashara bila ya leseni katika operesheni iliyoendeshwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Vileo Zanzibar, Abdulrazaki Abdulkadiri na askari waliokuwa na silaha

Watuhumiwa hao wamesomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Malindi, Mwanahidi Abdalla Othman, wakiwamo wanaume saba na wanawake 18 na wote walikana mashtaka yao isipokuwa mmoja alikiri kosa na kutakiwa kulipa faini ya Sh. 800,000.

Mwendesha mashtaka kutoka Jeshi la Polisi, Suleiman Masoud, alisema watuhumiwa wanakabiliwa na mashtaka ya kufanya biashara ya vileo bila kuwa na leseni kitendo ambacho ni kinyume na Sheria ya Bodi ya Udhibiti wa Vileo Zanzibar Namba 9 ya mwaka 2020.

Hata hivyo, Hakimu Mwanaidi Abdalla Othman, alisema dhamana kwa watuhumiwa ipo wazi kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili wenye vitambulisho, fedha taslimu Sh. 200,000 na dhamana ya maandishi Sh. 300,000 kabla ya kupandisha dhamana ya fedha taslimu kufikia Sh. 400,000 kwa kila mshtakiwa.

Wakili wa watuhumiwa, Alex Paul, alipinga na kuomba mahakama kuangalia upya masharti ya dhamana kwa madai haiwezekani shtaka moja masharti ya viwango vya dhamana yawe tofauti na kuwapa wakati mgumu washtakiwa.

Hakimu Mwanaidi alisema kesi hizo zitaendelea kutajwa kwa washtakiwa kwa tarehe tofauti kwa kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka na washtakiwa baada ya kukana mashtaka dhidi yao.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kiongozi Mwandamizi wa Jumuiya ya Wauza Vinywaji Zanzibar, Hussen Ali Kimti, alisema wamesikitishwa na Bodi ya Udhibiti wa Vileo Zanzibar kuvunja amri ya Mahakama Kuu ya kusitisha utekelezaji wa tozo mpya ya leseni za baa mpaka kesi ya msingi waliofungua kumalizika visiwani humo.

Alisema baada ya Sheria namba tisa ya Bodi ya vileo ya mwaka 2020 kuanza kutumika Jumuiya ya wauza vileo Zanzibar iliamua kufungua kesi ya kupinga tozo za leseni kwa kupandishwa kwa zaidi ya asilimia 200 bila ya kushirikishwa wadau katika sekta hiyo.

“Tulifungua kesi kupinga tozo ya leseni kupandishwa kutoka milioni mbili hadi milioni 4.8 kwa kila baa na masharti ya baa ziwe umbali wa mita 1,000 kutoka maeneo ya huduma za jamii kama shule, nyumba za ibada hospitali na makazi, sisi tunaona baa zote zitafungwa kwa mujibu wa sheria hii na watu kupoteza ajira,” alidai Kimti.

Alisema kupitia kesi namba moja ya mwaka 2021 chini ya Jaji Fatma Hamid, Jumuiya hiyo dhidi ya Mwanasheria Mkuu na Bodi aliwataka kusitisha utekelezaji wa tozo mpya za leseni hadi kesi ya msingi itakapomalizika, lakini bodi hiyo imeshindwa kuheshimu.

Alisema mamlaka za serikali zinatakiwa kuheshimu mihimili mitatu ya dola, Serikali, Baraza la Kutunga Sheria na Mahakama, lakini kitendo cha kuwakamata mameneja mauzo wa baa na kuwashtaki wakati kuna zuio la mahakama ni kutoheshimu muhimili huo.

Pia, alidai kitendo askari polisi kwenda usiku na kuwakamata wakiwa na silaha za moto na kuwaweka mahabusu kama majambazi hakileti sura nzuri katika kuendeleza sekta ya biashara na kuwainua wajasiriamali Zanzibar.

“Kati ya watu waliokamatwa mmoja alikuwa na mtoto wa miezi sita ameshindwa kumnyonyesha mpaka siku ya pili majira ya saa 10 jioni baada ya kuachiwa kwa dhamana,” alidai.

Wakati hayo yakitokea Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar na Bodi ya Vileo wamefunguliwa mashtaka ya kuvunja sheria ya udhibiti wa vileo namba tisa ya mwaka 2020 na Bodi ya Jumuiya ya Maimamu Zanzibar baada ya kutoa vibali vya kuingiza pombe kwa kampuni zaidi ya tatu kinyume na kifungu cha 33(1) pamoja na kushindwa kusimamia masharti ya utoaji leseni ya baa.
 
Back
Top Bottom