Sasa nimekuelewa. Kwamba unataka kwenye kusherehekea ushindi kila shabiki awe mstaarabu, muungwana, mzalendo na mnyenyekevu kwa kadri unavyohisi wewe ni sahihi. Hilo haliwezekani popote pale duniani. Unapaswa kusikiliza maoni na matamshi ya wahusika wakuu wa timu inayoshangilia. Laiti kauli hizo zilizokuudhi zingetolewa na Kocha (aliyewashukuru Watanzania wote) na/au viongozi wengine, ungekuwa na hoja. Ni lini Simba na Yanga zinapofungana umesikia mashabiki wa aliyeshinda wakimpa pole mtani wake mitaani? Umepata kusikia shangwe za mtani aliyeshinda zisimnange mpinzani wake? Wakati wa kusherehekea ushindi, aliyeshindwa anapaswa kujua, kujiandaa na kustahamili kauli za maudhi, ambazo mara nyingi ni mfululizo wa kutambiana kulikoanza kabla ya mpambano. Simba kuitwa wa mchangani/matopeni hajatukanwa na Yanga. Yanga kuitwa gongowazi hajatukanwa na Simba. Kama pilipili inavyonogesha ladha ya chakula licha ya kuwasha, ndivyo utani kama huu unavyonogesha ladha ya mpira licha ya kuwa haumpendezi aliyeshindwa.