Luteni
JF-Expert Member
- Jan 9, 2010
- 2,274
- 302
NAIBU katibu mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe ametinga wilayani Kibaha kuwaomba wananchi kumuongezea nguvu bungeni kwa kuwachagua wabunge wengi kadri iwezekanavyo wa kambi ya upinzani ili kwa pamoja waweze kwenda kuibana serikali ili iweke mazingira mazuri ya maisha wa Watanzania.Waliokuwa wanasema Chadema haikujipanga kwa kampeni walikosea, baada ya Zitto kusawazisha mambo nyumbani ameanza kampeni zake katika mikoa ya Pwani na Kusini kwa lengo maalum.
Mgombea huyo wa ubunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini aliueleza umati mkubwa wa wananchi waliohudhuria mkutano wa kampeni wa chama hicho kuwa katika kipindi hiki anahitaji wasaidizi wengi bungeni ili kila mmoja kwa nafasi yake akatetee maisha ya wananchi ambao wengi wao ni masikini na kwamba akiachwa yeye peke yake, atachelewa kukamilisha dhamira yake ya kuhakikisha kila mtu anakuwa na maisha bora.
Zitto alitoa ombi hilo juzi kwenye viwanja vya Mwendapole wakati wa mkutano wa kampeni wa Chadema. Zitto, mmoja wa wabunge waliojipatia umaarufu kutokana na uwezo wa kujenga hoja na kuibana serikali, alisema amelazimika kusafiri kutoka Kigoma kwa ajili ya kuwaomba wananchi wamuongezee nguvu bungeni.
"Ndugu zangu wa mkoa wa Pwani, hakuna asiyefahamu (kashfa ya zabuni ya ufuaji umeme wa dharura iliyokwenda kwa kampuni ya) Richmond na (wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje) EPA," alisema Zitto.
"Haya mmeyajua baada ya kazi nzuri iliyofanywa na wawakilishi wenu ambao ni wabunge kutoka kambi ya upinzani, bila hao msingesikia na wala msingejua na mngeendelea kutafuniwa fedha zenu za kodi ambazo kwa sasa zingesaidia kuinua maisha yenu.
"Hivyo, ili tuweze kuibua mengine, maana ninaamini yapo mengi tu, mniongezee nguvu kwa kunipa wabunge wengi kadri iwezekanavyo hapo Oktoba ili kwa pamoja tukafanye kazi ambayo muda si mrefu mtaona manufaa yake."
Kiongozi huyo alisema miaka 50 ambayo serikali iliyopo madarakani imekaa imetosha kabisa kuthibitisha kuwa imeshindwa kutimiza matakwa ya watu wake na hivyo sasa ni kipindi cha mapinduzi na kuwataka wananchi wakiweke chama kingine chenye dhamira ya kuinua maisha ya watu wake, ambacho alikitaja kuwa ni Chadema.
Monday, September 20, 2010
Mgombea ubunge jimbo la kibaha mjini.
Mgombea Ubunge wa jimbo la Kigoma Kaskazini,kwa chama cha CHADEMA,Mh Zitto Kabwe jana alianza rasmi mzunguko wa nchi nzima kuwasaidia wagombea Ubunge na Udiwani wa CHADEMA katika majimbo na Kata zao.Jana alikuwa mjini Kibaha akimnadi mgombea Ubunge kwa jimbo hilo la Kibaha Mjini ,Bw.Habibu Mchange.