TUTAFAKARI JUU YA JAMII YETU
1. Maadili ni ya lazima katika kujenga jamii.
Hatuwezi kuishi katika jamii ya watu bila dira ya kimaadili. Watu wote, hata wale wasiomwamini Mungu wanahitaji dira ya kimaadili ili msimamo wa kimaadili kuongoza jamii yao. Bila hivyo, jamii inakengeuka na kuwa uwanja wa mashindano ambamo wenye kumudu na wenye nguvu wanakuwa na fursa ya kuishi vizuri na wanaobaki wanasakamwa na maisha duni. Jamii ya namna hii inapoteza hulka na wasifu wa kuwa jamii ya wanadamu.
Kwetu sisi tunaomwamini Mungu, tunatambua na kukiri kuwa Mungu aliumba ulimwengu katika mchakato endelevu ambamo kwa kutaka kwake, aliwapa wanadamu nafasi na wajibu wa pekee.
Mungu alimuumba mwanadamu katika sura yake, akamjalia akili, utashi na moyo ili kumwezesha kushiriki katika mchakato huu wa uumbaji na kuifanya dunia iwe mahala pa kiutu, ambamo kila mmoja ana nafasi yake, haki na wajibu wake. Kwa hiyo, hadhi ya utu wa kila mwanadamu na ubora wa jamii nzima ndio msingi mkuu wa mambo ya kijamii na ndio msingi wa kutengeneza sera za kijamii. Kila mwanadamu amekirimiwa sifa ya asili na uwezo wa kutambua nini maana ya kuwa mtu. Sheria ya asili inaongoza dhamiri ya kila mtu na ya jamii.
Uwezo huu ni lazima ujengwe kwa bidii na kufanyiwa tathmini endelevu kama mtu binafsi na kama jamii. Sehemu moja ya uwepo wetu kibinadamu na kuwa na uwezo wa kuchagua na kufanya maamuzi ni kwamba tunaweza kuchagua mema ama maovu. Hata hivyo kuna jeraha katika tabia ya mwanadamu ambalo ni uwezo wa kufanya maovu.
Upande mmoja kuna hali au uwezo wa kutenda maovu kama mtu binafsi, lakini pia kuna dhambi ya jamii, maovu tunayofanya kama jamii, au kama kikundi ndani ya jamii. Kwa maovu hayo watu binafsi au makundi fulani katika jamii wanakuwa ndio wahanga.
Ndio maana lazima tujifunze kuwa na mwenendo mwema na kukubaliana kushughulikia maisha ya pamoja yanayofuata haki na wajibu ambazo msingi wake ni hadhi ya utu wa kila mmoja. Hizi ndizo tunu au thamani za jumla na mtu hawezi kuondolewa haki na wajibu hizo.
Jamii inaweza kuwa ya kiutu ikiwa tu inaheshimu hadhi ya kibinadamu ya kila mmoja, kujali faida ya jamii nzima, Kumwezesha kila mmoja kuchukua nafasi yake na kujenga kwa mshikamano ubora wa maisha ya wote.
Ili jamii iwe ya kiutu, lazima iishi kwa kuzingatia Ukweli Uhuru Haki Upendo.
2. Sera za kijamii lazima zionyeshe dira ya kimaadili.
Shughuli zote za kiuchumi na maendeleo ya vitu lazima viwe katika kumhudumia mwanadamu na jamii. Uzalishaji kiuchumi, utajiri, bidhaa za vitu, ugawaji wa faida, kugawana uchangiaji na kubeba majukumu lazima vilenge kumnufaisha mwanadamu na watu wote katika jamii iwe hapa nchini ama katika upeo wa kimataifa.
Katika msingi huu tunaona kwamba nguvukazi (watu) ni muhimu kuliko mtaji, (vitu), inamaanisha kwamba kujitafutia faida ni halali lakini isiwe kwa gharama ya wengine au kuwanyima wengine haki zao. Ni kwamba kufanya biashara ama kuendesha Taasisi ya Fedha haifai iwe ni shughuli ya kiuchumi tu, ila inapaswa ifungamanishe tunu za kijamii zinazowekwa katika sera zao ambazo zinaheshimu hadhi ya utu wa watu. Mfano; kulipa mshahara unaotosheleza mahitaji muhimu, kurekebisha riba, kuweka bei za bidhaa au mazao zilizo za haki.
Tunaweza kukubali kuwa mfumo wa soko huria una mazuri mengi na unaweza kuwa chombo kizuri katika kutenda haki. Lakini uhuru huo unapaswa kudhibitiwa ili uwe wa kuhakikishia uwiano, hadhi ya utu wa wenye kipato cha chini, maskini na wasio na uwezo.
Serikali, kwa hiyo ina wajibu wa kuingilia kati ili kuyakabili mambo ambayo yanaonyesha matumizi mabaya ya uwezo wa kiuchumi na kuleta uonevu kwa walaji na soko kama tunavyoona sasa katika sekta ya fedha, ya nishati na ya madini na vile vile katika biashara ya fedha kimataifa.
3. Utekelezaji wa masuala mbalimbali katika Tanzania leo
Kuna mambo mengi tunayotakiwa kuyatafakari kwa mtazamo huu wa kimaadili.
a) Tumepoteza uwiano kati ya mtaji na nguvukazi.
Katika zama zetu hizi, mtaji, fedha, faida na ukuaji wa uchumi vimekuwa ndio kipaumbele dhidi ya mambo ya kijamii na mahitaji ya kijamii ya watanzania wengi. Hali ilivyo sasa ni lazima tuache maneno na kuchukua hatua. Suala kama la mshahara toshelezi, huduma ya afya katika mahospitali na ubora wa vifaa na mazingira ya elimu, na karo katika shule za binafsi, gharama ya usafiri, kuchangia elimu ya juu, huduma ya maji safi haya yote yanahitaji kuangaliwa zaidi.
Yatubidi sasa tuache kusema kwamba hakuna fedha hili ni suala la utashi wa kisiasa na kutambua vipaumbele kimaadili. Watu sasa wanajisikia vibaya na hivyo hasira inajengeka. Hapa ni lazima tuchukue wajibu wetu.
b) Utamaduni wa bahasha
Hapa hatuhitaji kuzama katika maelezo ya kina, kwani kwa hakika, sote tunaelewa kinachozungumziwa hapa. Malipo ambayo hayako katika mfumo wa kawaida na wa kisheria wa nguvukazi na gharama. Malipo ya namna hii yamekuwa ni mfumo sanjari wa kujipatia kipato. Tatizo hapa ni kwamba mfumo huu ni kwa wale tu ambao wanaweza kuingia katika mfumo wenyewe.
Malipo ya bahasha yanafanyika kimya kimya, bila uwazi na hayapo katika udhibiti, hayatozwi kodi na wala hayana msingi wa kisheria. Haya ni mambo ambayo ni kinyume na maadili, ni matendo maovu. Tunaelewa kuwa kuna malipo halali kama bonasi, motisha kwa ajili ya kuboresha utendaji, malipo ya ziada kwa ajili ya utendaji au utumishi bora, zawadi kwa bidii na ubora wa kazi. Haya ni malipo halali, hayapingani kinyume na maadili.
Kumpatia malipo bahasha mtu kwa kuhudhuria mkutano ambao ni sehemu ya kazi yake au kwa mtu unayempelekea ombi lako au mradi wako haya sio sawa, ni makosa. Huu ni mwelekeo unazidi kujijenga katika nyanja nyingi. Hakuna haja ya kuendelea.
Hatari ya kuendeleza utamaduni wa bahasha ni kuwapatia wachache fursa ya kipato na kujenga tabaka la matajiri na kuwaacha walio wengi wakiwa na vipato duni na maisha duni.
Katika utamaduni wa bahasha hatari kubwa zaidi ni kwamba inabomoa maadili ya jamii juu ya kazi na uwajibikaji. Halikadhalika fikra ya kujali, kuthamini na kupenda kufanya kazi vinadhoofishwa. Katika msingi wa kimaadili kinachozingatiwa ni ubora wa kazi, thamani au tunu ya mradi na majukumu mtu anayoyabeba. Inamaanisha thamani ya mchango wa mtu anaoutoa kwa njia ya kazi yake. Katika utamaduni wa bahasha, haya yote hayazingatiwi.
Utamaduni wa bahasha unawajengea watu fikra kwamba haijalishi nini unachofanya, lakini cha msingi ni lazima kuwa mjanja na kutumia mitandao. Na madhara yake ni kushuka kwa maadili, na watu kutojali na kuthamini kazi ya mwanadamu na kutamani furaha ya kufanya kazi ambayo mtu huipata katika maana ya kuwa na hadhi ya utu wa mwanadamu.
Stahili na sifa njema, uwajibikaji, wajibu wa kuhudumia wengine ni tunu ambazo zinafifia na kupotea na badala yake uchoyo na ulafi, tama iliyokithiri ya kupata mali, ufujaji ndizo tabia zinazoshamiri miongoni mwa watu.
c) Takrima
Kwa miaka kadhaa viongozi wa dini wamekuwa wakisema kwamba takrima ni malipo yasiyo halali hasa inapotumika wakati wa uchaguzi. Lakini wagombea, halikadhalika wananchi kwa jumla wamekuwa wakiendelea kufurahia takrima. Ikiwa kweli tunataka kujenga utamaduni wa demokrasia ya kweli na kuiwezesha nchi yetu kunufaika na siasa ya vyama vingi, sasa ndio wakati wa kulifanyia kazi tatizo la takrima kwa makini.
Ukweli ni kwamba kinachotokea wakati wa uchaguzi hakihusiani kabisa na takrima, bali ni biashara kabisa. Wagombea wanawaendea wapiga kura kuwalaghai wawape kura zao, na wapiga kura wanafurahia kupokea fedha au zawadi ndogo ndogo. Ni biashara ya kubadilishana kura fedha/zawadi za vitu vidogo vidogo.
Lakini lazima kuelewa kuwa uchaguzi katika jamii ya kidemokrasia ni jambo lenye maana kubwa linalochukuliwa na kufanyika kwa makini. Ni jambo linalohusiana na namna taifa litakavyoongozwa, na watu wenye mawazo gani na watajali na kuweka vipaumbele gani na sera zipi haya yakiwa yamefungamanishwa na aina ya watu wanaoshika uongozi.
Wakati umefika sasa wa kuangalia suala la vyanzo vya fedha za uchaguzi za vyama vya siasa. Vyama vinapata fedha kiasi gani na kutoka wapi? Fedha hizo zinatumikaje? Je, taasisi za umma na za huduma zinahusika vipi? Ni wakati sasa wa kudai uwazi katika mambo haya, haifai yabaki kuwa katika siri kwa kuwa yanahusu maisha ya jamii yetu.
d) Rushwa
Hili ni suala la kimaadili kwanza. Kudhani kwamba Polisi, Mahakama au TAKUKURU ndio vyombo pekee vya uhakika katika kupambana na rushwa ni kujibu kwa njia rahisi mno. Ukweli ni kwamba rushwa imeshamiri kwa sababu watu wengi wanapenda rushwa na wanafanya vitendo vya rushwa.
Lazima tuanzie hapa na kuanza kampeni ya kujenga upya maadili. Viongozi wa kidini lazima waongoze jitihada hizi. Lakini pamoja na viongozi wa dini kuna mabadiliko pia yanayohitajika katika ngazi itakayohusisha asasi na miundo. Suala zima la upatikanaji wa taarifa na sheria ya usiri katika utumishi wa umma, maandalizi na maamuzi ya mikataba mikubwa hufanyika katika usiri mkubwa wakishirikishwa watu wachache tu wanaokubalika ni changamoto inayodai kukabiliwa. Kuna pia desturi ambayo imejengeka ambayo ni hatari. Desturi hii ni kuunganisha mambo ya kibiashara na uongozi wa kisiasa. Vile vile kuna kukosekana udhibiti na uchunguzi na pia kunakosekana uwiano katika mgawanyo wa madaraka kati ya mikono mitatu ya Serikali Dola, Mahakama na Bunge.
Haya sio masuala ya kisiasa au kisheria tu. Haya kwanza kabisa ni masuala ya kimaadili. Lazima tuanzie katika dira tunayoiwekea jamii yetu na kwa vipi jamii yetu inavyoweza kujipanga. Dira hiyo inajengwa katika msingi wa kimaadili wa taifa letu na sheria ya asili kama ulivyoelezwa hapo.
Katiba ni matokeo tu ya dira hiyo, na imeandikwa katika namna ya mkataba wa kijamii. Serikali inayokuwa madarakani sio mtawala wa mkataba huu wa kijamii, bali serikali inakuwa mtumishi wa Katiba na mkataba wa kijamii.
HITIMISHO:
- Kusimama katika ukweli, kuruhusu ukweli ujulikane na uzungumzwe, kutasaidia kupunguza tabia ya kusema uongo, majungu na kuongeza sifa nzuri katika jamii.
- Kuwa na kiburi cha kutotambua na kukubali makosa ni jambo linalovunja mshikamano wa kijamii na kujenga hali ya kutoaminiana.
- Kuishi katika hali ya kukataa ukweli wetu, kutotaka kuona na kutambua ukweli wa tabia yetu kibinafsi na kijamii, kunapunguza au kudhoofisha nguvu ya kimaadili ya jamii na kuizuia marekebisho yanayohitajika katika kushughulikia makosa na madhaifu yetu. Tusiogope kuwaelimisha watu kufanya ukosoaji wenye kuleta mawazo yenye kujenga, na pia kuwatia moyo kushiriki katika maamuzi.
- Hasira takatifu ni tunu au fadhila ya kimungu. Mara nyingi tunaona katika vifungu mbalimbali ndani ya Biblia jinsi Mungu akiongea kwa hasira na katika hali ya kukasirishwa na kukerwa anapowaona maskini, wasio na uwezo wakiwa ndio wahanga. Na pia hasira ya Mungu inawaka juu ya watu wanaowatumia wengine vibaya.
Tunahitaji moto huo katika mioyo yetu, tusimame upande wa maskini na kuwatetea na vivyo hivyo kwa wale wasio na fursa, tuweze kukataa rushwa na kuachana na mambo yanayowasababishia watu mateso hata kifo. Tuombe kuwa na hasira hii kila tunapoona mambo mbalimbali yanayodhihirisha kuwa watu hawajaliani.
Tuchukue changamoto hii kama wito na tuitikie kwa kuwajibika na kazi hii. Mungu abariki jitihada zetu.
+Paul Ruzoka
Askofu Mkuu wa Tabora
Mwenyekiti wa Tume Haki na Amani
Baraza la Maaskofu