Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema hawezi kusaliti demokrasia na mageuzi ambayo yeye ameyapigania tangu akiwa na umri wa utoto.
“Mimi ni miongoni mwa watu tuliopachikwa jina la usaliti, kama binadamu, siwezi kujisikia vizuri kuitwa msaliti wa mageuzi na demokrasia kwa sababu tu nasimamia kile ninachokiamini ambacho wenzangu hawakubaliani nacho.”
Zitto anasema tuhuma hizo msingi wake ni watu kushindwa kukubali ukweli kila mtu ana mtazamo na msimamo juu ya jambo fulani.
“Hata hivi sasa ninapotofautiana na vyama vingine vya upinzani kuhusu nini kitangulie kati ya Katiba mpya na tume huru ya uchaguzi bado ninaonekana ni msaliti, jambo ambalo si sahihi hata kidogo,” anasema.
“Pengine tatizo langu linalosababisha kupachikwa majina mabaya, ikiwemo la usaliti ni kufikiri tofauti na wenzangu kuhusu namna bora ya kufikia mafanikio kwenye jambo tunalolipigania. Lakini kinachonipa faraja ni kwamba mwisho wa siku tunajikuta tutakuwa na msimamo wa pamoja katika kilekile kilichosababisha niitwe msaliti,” anasema Zitto.