Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,872
- 34,363
Na Ramadhan Semtawa
MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma, Zitto Kabwe amesema kuna ugumu katika kuzipata Sh42.6 bilioni zilizobaki katika uchunguzi wa fedha za EPA kwa kuwa hadi sasa haijulikani zilipo.
Fedha hizo ni kati ya Sh139 bilioni zilizochotwa kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), ambazo wizi wake ulibainika katika mahesabu ya kati ya mwaka 2005 na 2006. Tayari Sh70 bilioni zimesharejeshwa na wezi baada ya kuahidiwa msamaha huku zaidi ya watu 20 wakifikishwa mahakamani kwa mashtaka ya kuiba, kushiriki au kula njama za kuiba fedha hizo.
Uchunguzi wa wizi huo mkubwa haukuweza kubaini fedha hizo kutokana na mpango wa kuzichota kuhusisha mitandao iliyovuka mipaka, tatizo lililomfanya Rais Jakaya Kikwete kuunda kikosi kazi cha kuchunguza fedha hizo mwaka mmoja uliopita.
Kiasi hicho cha Sh42.6 bilioni kinatajwa kuchotwa na makampuni 9 ambayo nyaraka nyingi za kughushi zinaonyesha kuwa kampuni hizo zinatokea nje ya nchi, ikiwemo kampuni ya Marubeni ya Japan.
Akizungumza na gazeti hili jana, Zitto alieleza kuwa tatizo kubwa linaweka wingu katika upatikanaji wa fedha hizo ni kampuni ya M/S Lazard Freres kutopewa hadidu za rejea za kushughulikia wizi huo.
Agosti mwaka juzi Rais Kikwete alikiongezea muda kikosi kazi hicho kuendelea kutafuta kiasi cha Sh42.6 bilioni ambazo kumbukumbu zake nyingi ziko nje ya nchi hivyo kuhitaji ushirikiano wa nchi husika, ikiwa ni pamoja na polisi wa kimataifa, maarufu kama Interpol.
Hata hivyo, Zitto anaona hakuna matumaini tena ya kurejeshwa kwa fedha hizo baada ya kuona ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma, alisema tatizo kubwa ni kampuni ya Lazard haikupewa hadidu za rejea kukagua kiasi hicho.
Lazard, ni kampuni iliyo na makao yake nchini Ufaransa na ambayo imeingia mkataba na BoT kwa ajili ya kukagua deni halisi la EPA na kama kuna wadai halali wanaopaswa kulipwa na au taasisi hiyo kuu ya fedha ya nchini isilipe madeni hayo, na athari zinazoweza kutokea kama isipolipa.
Zitto anaamini kuwa Lazard ni kampuni ambayo ina utaalamu ambao ungeweza kusaidia kubaini fedha hizo zilipo kama ingekuwa imepewa hadidu za rejea za kufanya hivyo.
"Hadi sasa mambo yanaonekana kuwa magumu... unajua Lazard ndiyo ilipaswa kukagua hizo fedha lakini katika hadidu za rejea haikupewa kufanya hivyo, kwa hiyo kuna tatizo," alisema Zitto akionyesha wasiwasi.
Takwimu za awali zinaonyesha kuwa hadi mwaka 1999 deni ambalo serikali ilitakiwa iwalipe wadai wake kutokana na fedha zilizotengwa EPA lilifikia dola 623 milioni za Kimarekani, ambazo kati ya hizo dola 325 milioni zilikuwa ni deni la msingi na dola 298 ni riba na baadaye deni likaongezeka hadi kufikia dola 677 milioni za Kimarekani.
Mwaka jana, kamati hiyo ya Zitto iliitaka serikali kuangalia uwezekano wa kuipa kazi kampuni ya Lazard kukagua wizi wa kiasi hicho cha fedha ikisema kuwa ina uzoefu na uwezo wa kitaalamu, tofauti na kikosi kazi kilichoundwa na rais.
Hata hivyo, Waziri wa Fedha na Uchumi alisema mamlaka ya kugeuza uchunguzi huo yalikuwa ni ya rais ambaye tayari aliunda kikosi kazi chini ya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Johnson Mwanyika, ambaye kwa sasa amestaafu.
Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu aliwahi kuliambia gazeti hili kuwa taasisi hiyo isingeweza kuipa Lazard kazi ya kukagua kiasi hicho kwa kuwa tayari rais alishaunda kikosi kazi
Chanzo: Gazeti la Mwananchi