Elias Msuya
Platinum Member
- Dec 23, 2011
- 267
- 1,014
Adv. E. Kilatu, LLB & LLM (Const. & Admn. Law)
Utangulizi
Siku chache zilizopita Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam alitoa Tamko linalotishia watu kufika mahakamani ili kushuhudia kesi ya kihistoria inayohusu kiongozi wa kisiasa kutuhumiwa na kosa kubwa kabisa la uhaini.
Ni ya kihistoria Kwa sababu tofauti na zile za mwaka 1964 na za miaka 1980 tuhuma hii inamhusu mwenyekiti wa taifa wa chama cha upinzani bila kuhusisha jeshi au walau mgambo. Pia ni ya kihistoria Kwa sababu inahusu mtu ambaye tayari alishapita uvuli wa mauti na kapona. Ni ya kihistoria Kwa sababu inahusu mtu aliyepata kugombea urais wa nchi na Mwanasheria nguli kabisa nchini.
Uhalali wa watu kwenda mahakamani kwenye kesi
Moja ya msingi wa muhimu kabisa ni kwamba kesi za jinai Kwa ujumla wake zinatakiwa kuendeshwa Kwa wazi. Hii ni Kwa mujibu wa kifungu cha 186 (1) cha Kanuni ya mwenendo wa Jinai, 1985 sura ya 20 ambacho kinasema mashauri yote ya jinai yataendeshwa mahali pa uwazi/ mahakama ya wazi (open court). Pamoja na kwamba Sheria haijatia tafsiri ya mahakama ya wazi; mahakama yenyewe imeshakuwa na tafsiri kwamba mahakama ya wazi ni ile haki ya watu wote kufika na kuingia kwenye mahakama na kushuhudia kesi bila kudhibitiwa.
Msingi wa kifungu hiki ni kikidhi Moja ya msingi wa asili ambao unataka haki isifanyike tu bali ionekane ikitendeka. Haki kuonekana inatendeka ni pamoja na uwazi katika uendeshaji wa shauri lenyewe. Kama shauri likiwa gizani haki inakuwa mashakani.
Kwa ulimwengu wa Sasa mahakama karibu zote zimeimarisha zaidi uwazi katika utoaji haki ikiwemo kurusha mbashara shauri mfano mzuri ni nchi ya Kenya na Uganda ambao ni marafiki zetu wa kihistoria.
Hatua ya uwazi Kwa Tanzania pia si ngeni sana pamoja na mapungufu ya hapa na pale hasa ya kikanuni juu ya kurusha mbashara (live streaming).
Kwa mujibu wa maamuzi wa mahakama kuu kwenye shauri la Baranguza dhidi ya Shule ya Sheria ya Tanzania mahakama ilisema hakuna zuio la kisheria kurusha mbashara isipokuwa tu kanuni za kuweka utaratibu bado kutungwa.
Hata hivyo, Kwa kesi zenye maslahi mapana zote tangu wakati wa ukoloni kwenye kesi ya uchochezi ya 1958 dhidi ya Julius Kambarage Nyerere hakuna mtu aliwahi kuzuiwa kuingia mahakamani kushuhudia kesi hiyo.
Uzoefu katika mahakama kuu ya Tanzania
Uzoefu umeinyesha kuwa mahakama kuu imekuwa ikilinda kwa wivu mkubwa haki ya wananchi kufuatilia mashauri hasa yenye maslahi ya umma hasa za viongozi wa kisiasa.
Tumeshuhudia mahakama ikitafuta kumbi kubwa ili kuwezesha watu wote kuingia mahakamani kufuatilia kesi.
Kuna nyakati hasa miaka ya 1995 kwenye kesi za uchaguzi mkuu mahakama iliopoona nafasi haitoshi ilienda mbali zaidi hadi kufunga spika nje ya mahakama ili umati uliofurika usikilize kesi hiyo.
Hivyo hivyo, kwa wamka 2010 pale Arusha kwenye kesi ya uchaguzi dhidi ya God bless Lema, Mahakama ikifanya ivyo pia na shauri likaendeshwa Kwa uwazi. Aidha, tumekuwa na kesi za Halima Mdee dhidi ya Chadema na zile zilizohusu Mbowe na Jamhuri watu kwa mamia waliruhusiwa kuingia mahakamani kufuatilia.
Uzoefu wa uendeshaji wa mashauri yanayohusu viongozi wa kisiasa Mahakama ya Kisutu
Pamoja na kwamba haki ya watu kuingia mahakamani kufuatilia mashauri ipo kisheria, kwa kiasi kikubwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam iliyopo Kisutu imekuwa na matukio machache hasa miaka mitano iliyopita ya wafuasi wa vyama kuzuiwa na Jeshi la Polisi kuingia mahakamani kufuatilia kesi dhidi ya viongozi wao.
Kuna wakati ambapo Wanachama wa Chadema walizuiwa na kupigwa mabomu na wengine kufunguliwa mashauri katika mahakama ya Mwanzo ya Wilaya ya Ilala ya Kariakoo, shauri ambalo liliibua hisia kali na kwa vile wakati ule sheria haikuruhusu wakili mahakama za Mwanzo wengi.
Waliamini shauri hilo lilipelekwa huko na Jamhuri kimkakati Kwa vile lingeweza kufunguliwa kwenye mahakama ya Kisutu.
Mipaka ya mamlaka ya polisi kwenye maswala ya haki
Najua polisi hawachelewi kuja na hoja za kiintelijensia. Hata hivyo, swali la kujiuliza kwa nini Mahakama Kuu watu hawajawahi zuiliwa ila hiyo tabia inafanywa kwenye mahakama za chini tu?
Na hata ingekuwa kweli kuna polisi wanenusa uhalifu jukumu lao ni kuimarisha ulinzi na kubaini wahalifu badala ya kuvunja haki za msingi za raia. Napenda kusisitiza pakiwa na ulazima wowote wa kuathiri haki hatua hiyo ni lazima iwe na uhalali wa kisheria (legality), iwe ni lazima kuchukua hatua hiyo na kwamba hapana namna nyingine na mwisho usichikue hatua kwenye kiwango cha kupindukia.
Kwenye mazingira yetu kazi ya polisi ni kuhakikusha watu hawaingii na silaha yoyote na kuimarisha ulinzi dhidi ya hujuma yoyote Kwa wananchi au Kwa mahakama. Ila kuzuia watu kwenda mahakamani si hatua sawa kisheria.
Athari za Polisi Kuingilia Himaya ya Mahakama
Kama mahakama hasa za chini ikiwemo Kisutu zisipoamua kulinda haki za raia kuingia mahakamani Kwa mujibu wa sheria na kuachia mwanya Kwa polisi kuamua nani aende mahakamani na nani asiende itajenga taswira mbaya kabisa na kubomoa kabisa msingi wa mgawanyo wa madaraka (separation of powers).
Mgawanyo wa madaraka ni msingi unaojengwa kwenye ibara ya 4 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, lakini pia ni msingi wa kihistoria wa mataifa yote duniani. Mwisho itaibua hisia kwamba utawala unamizizi unayopenyeza kwenye mihimili mwingine.
Ni muhimu mahakama za chini zilinde taswira yake Kwa wivu mkubwa kama ambavyo mahakama kuu Kwa ujumla wake imekuwa mfano Bora juu ya hilo. Mahakama ni chombo cha mwisho cha utoaji wa haki Kwa mujibu wa ibara 107A ya Katiba ya Tanzania, 1977; na ni muhimu kusitiza kuwa haki ni pamoja na haki ya kufika mahakamani kufuatilia jambo linalowahusu.
Lakini pia haki hii inalindwa na ibara ya 21 ya Katiba inayotoa haki Kwa raia kushiriki kwenye mambo yanayowahusu na hivyo Kwa vile Lissu ni mwenyekiti wa chama taifa wananchi wana maslahi na kesi yake. Aidha ni haki ya raia kupata taarifa Kwa mujibu wa ibara ya 18 ya Katiba yetu hivyo haki hiyo ni pamoja na kufika mahakamani kufuatilia kesi hii.
Hitimisho
Zuio lililotolewa na Jeshi la Polisi halina uhalali wowote wa kikatiba, kisheria na kimantiki. Ni uvunjifu wa misingi ya utawala wa sheria, utawala Bora na ni hatua ya dhahiri ya polisi kuvuka mipaka na kusigina Katiba na Sheria walizoapa kulinda. Kazi ya polisi iwe ni kuimarisha ulinzi TU badala ya kuminya haki.
Nitoe Rai Kwa wizara ya Katiba na Sheria pamoja na wizara ya mambo ya ndani kuchukua hatua stahiki ili kulinda taswira ya nchi yetu kwenye maswala ya utawala wa sheria.
Mwisho kabisa ni rai Kwa mahakama yetu tukufu itoe msimamo juu ya haki ya raia kufuatilia mashauri kwenye mahakama za wazi.
Soma Pia: Kesi dhidi ya Lissu ni kesi dhaifu sana, Jamhuri ondoeni hii kitu kabla hamjapata aibu
Wakili Komba
Kwa upande mwingine Wakili kiongozi wa Haki Kwanza Advocates, Aloyce Komba ameongeza akisema:
“Kipimo cha 4Rs za Mhe Rais Samia Suluhu Hassan ikiwemo uwazi, uvumilivu, na utawala wa bora wa Serikali yake inayomshtaki Tundu Lissu ni pamoja na kuifanya kesi husika isikilizwe katika Mahakama huru ikiwemo kuruhusu wasikilizaji hasa wafuasi wa chama cha Chadema.
“Mahakama isinyamaze katika hili. Itoe tamko kwamba ni haki ya kila mtu mwenye nafasi kwenda mahakamani kusikiliza mwenendo wa kesi yoyote ikiwemo hiyo ya Tundu Lissu yenye masilahi au mvuto mkubwa wa kisiasa kwa jamii (a public/political interest case).
“Waandishi wa habari wote (wa Umma na Wasio wa Umma) waruhusiwe ili kuepusha upotoshaji wa taarifa za kesi hiyo. Lengo liwe ni Umma wa Tanzania kupewa taarifa sahihi kwa Mujibu wa Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari ya Mwaka 2016 na Sheria Zingine za Haki Jinai.”
