15. JKT ya kweli haikufa - ililala. Na wa kuamsha ni wewe

15. JKT ya kweli haikufa - ililala. Na wa kuamsha ni wewe

CHAGOSI GERALD

Senior Member
Joined
Jan 25, 2020
Posts
162
Reaction score
286
Sikiliza sasa…

JKT ile ya Mwalimu haikufa, hapana.
Ile taasisi ya kujenga taifa - iliwekwa chumba cha giza, ikafungwa taa, halafu ikafunikwa shuka ili ionekane imekufa.
Lakini bado inavuta pumzi, bado moyo wake unadunda taratibu kama mtu aliyelala usingizi mzito.

Swali ni moja:
Ni nani wa kuifungua pazia ili ipumue?
Jibu ni jepesi kama jua la asubuhi: Wewe.

LAKINI…

Kuna watu leo wanakupigia makelele juu ya D9, juu ya maandamano ya kisiasa, juu ya “mkombozi huyu na yule”.
Kama kwamba wao ni malaika walioshuka na vipepeo vya dhahabu.
Kumbe ni madalali tu - ndiyo, madalali!
Wamebeba makovu ya risasi kama beads za mshipi wa sala ili waonekane mashujaa wa taifa, wakati wamejaa ujanja wa kutafuta airtime na kuchuma machungu kwa mgongo wa wengine.

Ukweli mchungu ni huu:
Hao sio wanaharakati; ni wafanyabiashara wa machungu ya umma.
Na wanasiasa?
Acha tu - wanasiasa ni kama noti iliyochanika: inakataliwa madukani lakini wao wanaitumia kama kisingizio cha kupigia kelele mbele ya watu.

Kwahiyo, usije ukajidanganya:
Hamkimbizani kumrudisha Lisu wala kumshusha Samia.
Hapana.
Hao ni upande mmoja wa sarafu moja.
Sio malaika wa nuru na pepo wa giza — ni mdudu mmoja mwenye sura mbili.

MAANDAMANO YA AMANI? NDIO. MAANDAMANO YA WATU WAZIMA, SI MA-D9.

Kama kuna kitu cha kuandaliwa, basi ni maandamano ya amani yenye akili, sio yale ya kufuata mtu mwenye kipaza sauti na kichwa kilichoshonwa na daktari wa KCMC baada ya risasi kumgonga.

Maandamano ya kuonyesha:
-Tunajua nchi hii ni yetu.
-Tunajua vijana sio mawe ya kutupwa kwenye moto.
-Tunajua JKT haipaswi kuwa kambi ya kufua misuli tu, bali kiwanda cha taaluma, ajira, weledi, na uongozi.

Maandamano yanayosema:
“JKT irudishwe kwenye malengo yake ya awali. Irudishwe kwa vijana. Irudishwe kwa taifa.”

Si ya kupambana na jeshi.
Hapana!
Wale ni ndugu zetu.
Tumekula nao ugali, wengine tumekaa nao mwanzoni mwa mkanda wa viapo, tumelala nao kwenye baridi ya asubuhi za Aprili tukifanya parade ya utii.
Wawaue nani?
Kwa sababu gani?
Kwa sababu tunataka JKT iwe taasisi, sio kivuli chake?

Haiingii akilini.

KWANINI HAYA YOTE YALITOKEA?

Kwa sababu tangu 1995, mfumo uliingia kama mwewe anayeiba kifaranga - kimya, lakini makucha yake ni ya chuma.
Ukaigeuza JKT kuwa tangazo tu la TV na uwanja wa kukimbia, sio injini ya uchumi.

Matokeo?
-Taaluma inafukuzwa nyuma ya geti.
-Vijana wanapimwa misuli badala ya ubongo.
-Maafisa bora wanazaliwa kwa bahati, sio kwa mfumo.

Wenye F4 na La7 wanapita kama maji kwenye bomba, wakati wenye akili za kupanga kesho ya taifa wanazuiwa kama sumu.

Umewahi kujiuliza kwanini?
Kwa sababu mfumo unaogopa mtu mwenye kichwa kinachofikiri.
Akili ni sumu kwa mfumo uliooza.
Ndiyo maana wale wanaopata nafasi za juu kwenye mafunzo ya uafisa, mara nyingi ni kupitia njia ambazo ukizitaja unachekwa - njia za panya, “ndugu wa fulani”, au dili la “mjomba yupo pale”.

Na watu hawa wanataka ujitoe kwenda JKT bila kuuliza maswali?
Kama nani?
Kwa nini?
Kwa mfumo upi?
Wa nani?

Ndiyo maana nasema kwa sauti ya mwendawazimu:
Kujitolea JKT siku hizi bila mfumo kurekebishwa ni hekima ya mpumbavu.

KWA HIYO…

Kama hatutasema,
kama hatutatembea,
kama hatutadai,
kama hatutaamsha ile JKT ya Mwalimu iliyolala kwenye kitanda cha historia-

Watoto wenu, wajukuu wenu, na vitukuu wenu wataendelea kuwa watumishi wa mfumo unaowanyonya kama pamba kwenye mashamba ya zamani.

Na mtawaangalia tu wakienda kambini, wakirudi na misuli, lakini bila ajira, bila nafasi, bila mfumo wa kuwainua.

BASi! IMETOSHA!

Wakati ni huu.
Sio wa kupigana.
Sio wa kutupiana mawe.
Ni wa kuamka.
Wa kuikumbusha nchi kwamba JKT ilikuwa ndoto ya kujenga taifa, sio jukwaa la kudhalilisha vijana.
Wa kutangaza kwamba uzalendo sio risasi, sio uniform - ni utashi wa kuweka taifa mbele dhidi ya mifumo ya kifisadi.

Na kuanzia leo:
JKT ya kweli haijafa.
Inasubiri mlango ufunguliwe.
Na ufunguo upo mkononi mwako.
 

Attachments

  • FB_IMG_1766229541352.jpg
    FB_IMG_1766229541352.jpg
    278.6 KB · Views: 32
Back
Top Bottom