TULILA : CHANZO CHA UMEME WA MAJI ULIOMALIZA MGAO WA UMEME MJINI SONGEA
Na Albano Midelo
Kwa miaka mingi mji wa Songea umekuwa unakabiliwa na mgawo mkali wa umeme hali ambayo imekuwa ikirudisha nyuma maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika mji huo ambao ndiyo kioo cha Mkoa wa Ruvuma.
Mchawi mkubwa wa tatizo la umeme katika mji wa Songea ilikuwa kuendelea kutumia Jenereta chakavu ambazo zilikuwa zinatumia vipuli chakavu na changamoto ya mafuta ambayo yalikuwa yanakwisha mara kwa mara.

Rais Mstaafu Jakaya Kikwete Agosti 2009 alifanya ziara katika Mkoa wa Ruvuma kwa lengo la kuangalia shughuli za kimaendeleo na changamoto zinazowakabili wananchi wa mkoa huo.
Siku ya kwanza ya ziara yake Rais Mstaafu Kikwete wakati anapita barabarani akitokea uwanja wa ndege wa Songea alishuhudia wananchi wakipiga kelele na kudai umeme huku wamewasha taa mchana kutokana na hali halisi ya tatizo sugu la umeme wa kutoaminika katika mji wa Songea ambalo lilikwamisha shughuli za kijamii na kiuchumi.
Rais Mstaafu Kikwete alisikitishwa na kasi ndogo ya kushughulikia ufumbuzi wa tatizo la vipuri vya mashine za kufulia umeme katika mji wa Songea hali liyosababisha kumwagiza Meneja wa TANESCO mkoa wa Ruvuma wakati huo injinia Monica Kebara kufuatilia ili kujua vipuri vya mashine hizo vipo wapi na alitaka kupata ripoti ya vipuri hivyo na mwenendo mzima wa matengenezo ili wananchi wafahamu kila hatua.
Rais Kikwete hakuishia hapo, badala yake aliahidi kuileta mashine mpya ya kufua umeme ambayo aliamini ingeweza kumaliza tatizo la mgawo mkali wa umeme katika mji wa Songea hivyo mgawo mkali wa umeme kubakia kuwa historia.
Baada ya kufungwa mashine mpya ya Rais Kikwete aina ya ABC yenye uwezo wa kuzalisha megawati 1.6 angalau tatizo la mgawo mkali katika mji wa Songea lilipungua kwa miaka takribani mitatu, ingawa matatizo ya mafuta na vipuri yaliendelea na kuathiri umeme katika mji wa Songea.
Hata hivyo baada ya miaka hiyo tatizo la mgawo mkali wa umeme liliongezeka kutokana na kile ambacho kilitajwa na TANESCO kuwa ni kuharibika kwa mashine kutokana na vipuri kuharibika.
Tangu mwaka 2016 tatizo la mgawo wa umeme katika mji wa Songea limebakia kuwa historia mara baada ya TANESCO Ruvuma kuanza kununua umeme wa maji kutoka Tulila mto Ruvuma.
Chanzo hicho kinamilikiwa na watawa wabenediktine wa Mtakatifu Agnes Chipole Jimbo Kuu Katoliki la Songea ambapo sasa tatizo la umeme katika mji wa Songea limebakia kuwa historia.
Akizungumza kwa niaba ya Mama Mkuu wa Shirika hilo, Sr.Richards Chiwinga(OSB) anasema wana mashine mbili ambazo zina uwezo wa kuzalisha megawatts tano ambapo TANESCO Ruvuma ndiyo wateja wao wakuu ambao wanawauzia umeme huo.
“Mji wa Songea unahitaji megawatts kati ya 3.5 hadi 4.5 hivyo tunabakiwa na ziada ya umeme, TANESCO wamezima majenereta yao chakavu ambayo yalikuwa yanasababisha mgawo wa umeme, hivi sasa wanatumia umeme wetu wa maji unaozalishwa toka hapa’’,anasisitiza Sr.Chiwinga.
Soma zaidi : source :
Tulila:chanzo cha umeme wa maji kilichomaliza mgawo wa umeme mjini Songea