BigTall
JF-Expert Member
- Mar 9, 2022
- 706
- 1,716
Salaam, ndugu Mwanasheria Garatwa.
Nimeona andiko lako na uchambuzi wako juu ya suala la kuenguliwa mgombea wetu wa kiti cha Urais ,Mh.Luhaga Joelson Mpina huku ukielekeza lawama kwa chama chetu kufuatia kinachoitwa malalamiko ya mdada anayedaiwa kuitwa Monalisa Ndala.
Kwanza nikupongeze kwa jitihada zako za kujipa muda na kuchambua mambo haya kwa lengo la wengine kupata uelewa,lakini tunashauriwa kabla ya kuchambua,kutoa maoni au hitimisho kwa jambo lolote ni vyema kujipa muda kutafuta taarifa ili uwe na taarifa sahihi na kamilifu ili kuepuka upotoshaji.
Suala hili lipo Mahakamani Kuu ila nitajitahidi kuelezea juu juu kulingana na muktadha wa mambo uliyogusia kuepuka kuingilia yaliyo Mahakamani ili upate uelewa wa jambo hili.
Mwanasheria Garatwa ,ni vyema ukaelewa ya kwamba suala hili haikuwa hoja ya malalamiko ya Monalisa dhidi ya chama chetu ,bali ilikuwa hoja ya watu kadhaa wenye mamlaka walioamua kumtumia Monalisa Ndala ili kufanikisha dhamira yao ya kupambana na chama chetu na Mgombea wetu wa Urais. Ni vyema kufahamu kuwa Monalisa alipewa script tuu ya kucheza huku akiahidiwa maslahi binafsi.
Hao watu wenye mamlaka walimpa Monalisa Script ya kanuni za kudumu za uendeshaji chama za mwaka 2015 toleo la 2016 kanuni ya 16(4) wakimtuma ahoji hiyo ndani ya chama kwa kumuandikia barua Katibu Mkuu na kumpa nakala Msajili na Tume ya uchaguzi.
Maudhui ya namna hiyo hiyo alimuandikia Msajili tarehe 19/Agosti/2025 kwa njia ya kukishtaki chama kwamba kimekeuka kanuni zake , kanuni ya 16(4) ya kanuni ya uendeshaji chama ya 2015 toleo la 2016.
Ndugu Mwanasheria Garatwa, kanuni ya 16(4) ya kanuni za uendeshaji chama za 2015 toleo la 2016 inasema "Mtu kuwa na Sifa ya kugombea Urais inapaswa awe mwanachama wa ACT Wazalendo kwa muda usiopungua mwezi mmoja kabla ya tarehe ya mwisho ya uteuzi ya Mgombea".Hayo juu ndio yalikuwa madai makubwa ya huyo anayeitwa Monalisa Ndala katika kandarasi na mradi huo. Msajili akatuandikia barua tarehe hiyo 19/Agosti /2025 akihitaji chama tumjibu Monalisa katika madai yake hayo .
Ndugu yangu Mwanasheria Garatwa, katiba yetu ya chama haijawahi kuwa na hiyo ibara inayoweka masharti kwa mgombea wa Urais bali kanuni zetu za 2015 toleo la 2016 ndiyo ilikuwa na hiyo kanuni ambayo ni kanuni ya 16(4) ila mwaka 2024 chama chetu kupitia vikao vyake kamati Kuu na Halmshauri Kuu ilifanya marekebisho ya kanuni na hivyo tukawa na kanuni za uendeshaji wa chama toleo la 2024 ambapo ilifuta hizo kanuni za 16(4) na mabadiliko mengine.
Hivyo hoja ya kanuni ya uendeshaji chama ya 2015 toleo la 2016 kanuni ya 16(4) iliyokuwa inaweka masharti kwa mgombea Urais ikawa imekufa na kuzikwa,sababu haikuwa na relevance tena sababu haitumiki ,ni ya zamani na imeshafutwa na katika kanuni Mpya za uendeshaji chama toleo la 2024 haipo na hakuna hiyo kanuni.
Ndugu Mwanasheria Garatwa,msajili sababu alikuwa na nia ovu dhidi yetu na kuona hoja za Script alizopewa Monalisa katika mradi na kandarasi hazina mashiko tena sababu ni hoja za kanuni ya zamani na haifanyi kazi , Msajili akaendelea kutumia kivuli cha Monalisa mdada aliyekubali kutumika kama TOILET PAPER kwa maslahi yake binafsi ili Msajili kutafuta uhalali wa kutushughulikia.
Ndugu mwanasheria Garatwa ,Msajili alihoji kupitia kanuni za uchaguzi toleo la 2024 ,akatumia kanuni ya 9(a) inayosema "Mtu anayetaka kugombea uongozi KATIKA CHAMA atapaswa kuwa mwanachama wa ACT Wazalendo si chini ya siku 7 kabla ya tarehe ya mchakato wa uchaguzi kuanza".Msajili akataka kuhitimisha kwamba Mgombea wetu ndug. Luhaga Joelson Mpina tangu achukue fomu kugombea nafasi ya Urais ndani ya chama hana siku 7 tangu mchakato wa uchaguzi kuanza,hivyo hana Sifa.
Jambo ambalo Msajili alijipotosha kwa nia ovu kabisa kutumia kanuni vibaya ili kutimiza malengo na dhamira yake . Hii kanuni ya uchaguzi toleo la 2024 ni kanuni inayohusu uchaguzi wa ndani ya chama kama kiongozi wa chama, mwenyekiti wa chama, mwenyekiti wa Vijana au Wanawake ,Wazee, Mjumbe wa Kamati Kuu au Halmshauri Kuu na sio mchakato wa uchaguzi wa wa kiserikali (kura za maoni ) kupata wagombea Udiwani , Ubunge, Uwakilishi au Urais.
Ndugu mwanasheria Garatwa, hili msajili alielezewa vizuri sana, kwamba ndani ya chama chetu tuna aina kuu mbili ya michakato ya kiuchaguzi.Chaguzi za ndani ya chama(unaohusu uchaguzi wa kuchagua viongozi wa chama) na mchakato wa chaguzi za kiserikali (Unaohusu mchakato wa kura za maoni ) kupata wagombea Udiwani , Ubunge, Uwakilishi na Urais.Na Katiba yetu ya chama toleo la 2024 imedhihirisha hili katika ibara ya 108(1) na (2) kamati Kuu imepewa mamlaka kutunga kanuni na miongozo (Subsidiary legislations) na kuidhinishwa na Halmshauri Kuu kwa ajili ya utekelezaji mzuri wa sera na malengo ya chama .
Ndugu Mwanasheria Garatwa,Chama chetu kinatumia Subsidiary legislations mbili tofauti katika kuongozea chaguzi mbili tofauti. Chama chetu kinatumia kanuni (Regulation) yaani kanuni ya uchaguzi toleo la 2024 kwa chaguzi za ndani ya chama tuu, kama kumpata kiongozi wa chama ,wenyeviti ,Makatibu , Wajumbe wa Kamati Kuu na Halmshauri Kuu, viongozi wa Ngome za chama Vijana, Wanawake na wazee.
Ndugu , Mwanasheria Garatwa.Pia chama chetu, kinatumia mwongozo(Guideline) wa uteuzi wa wagombea ndani ya chama kwa chaguzi za kiserikali kama Diwani , Uwakilishi, Ubunge na Urais ,tunatumia Muongozo ambao kila kipindi cha uchaguzi Mkuu Kamati Kuu inapitisha na hii ni kwa mujibu wa Katiba yetu ya chama toleo la 2024 ibara ya 71(1)(iii) inayoeleza kwamba "Kamati Kuu ya Chama itapitisha ratiba na miongozo ya uteuzi wa Wagombea ndani ya chama kwa chaguzi za kiserikali kama madiwani , wawakilishi , wabunge na Urais.
Mwongozo huu unaweka taratibu , mchakato na Sifa za wagombea n.k . katika kila uchaguzi wa kiserikali baada ya miaka 5 ,tunapitisha mwongozo wa ndani wa uteuzi wa Wagombea uchaguzi wa kiserikali,mfano Mwongozo wa sasa tumeupitisha kamati Kuu na kuidhinishwa Halmshauri Kuu tarehe 23/Februari/2025.
Ndugu Mwanasheria Garatwa,binafsi naweza sema Msajili wa vyama vya siasa alikuwa na nia ovu dhidi yetu kwani hata baada ya kupewa maelezo ya kutosha na kueleweshwa na chama chetu, bado aliendelea kusisitiza kwamba kanuni za uchaguzi toleo la 2024 ndizo anazozitambua tuu huku akishikilia msimamo wa kanuni ya 9(a) ya kanuni ya uchaguzi toleo la 2024 ambayo ni kanuni inayohusu uchaguzi wa ndani ya chama. Na ndiyo maana ndani ya hiyo kanuni utakuta ngazi za uchaguzi Tawi ,Kata ,Jimbo na Mkoa ni wazi uchaguzi wa kiserikali hauna ngazi ya Tawi ,Wala ngazi ya Mkoa .
Lakini pia kanuni ya 51 ya kanuni hii ya uchaguzi kuna maelezo kuhusu rufaa kwa za kiongozi wa chama (KC), Mwenyekiti Taifa,Makamu Mwenyekiti Taifa na Wajumbe wa Halmshauri Kuu,hii ni dhahiri inaonesha kanuni hizi ni kwa uchaguzi wa ndani ya chama.Pia ukisoma kanuni ya 48 na 49 kanuni zinaelezea duru ya pili ikiwa kura za wagombea zimefungana katika mchakato wa uchaguzi wa kiserikali hakuna duru ya pili katika kura ya maoni ila kama kura zimefungana ni vikao vya uteuzi (Kamati Kuu ) ndio huamua nani wa kumteua,hivyo hii inadhihirisha kanuni hizi ni kwa uchaguzi wa ndani tuu na sio uchaguzi wa kiserikali kama msajili alivyong'ang'ania.
Ndugu Mwanasheria Garatwa,lengo letu la kuweka sharti la Mgombea wa nafasi ndani ya chama kutimiza angalau siku 7 katika kanuni ya 9(a) ya kanuni ya chama toleo la 2024 ,ni kwasababu tunaamini ndani ya siku 7 kabla ya mchakato wa uchaguzi kuanza,mwanachama huyu Mpya atakuwa sio Mpya tena atakuwa amejifunza tamaduni na taratibu za ndani ya chama ,misingi na miiko ya chama,kujua wajibu wa nafasi yake ndani ya chama na sisi chama pia kumjua vizuri sababu ni nafasi ya ndani ya chama anayokwenda kuitumikia hivyo ni muhimu ajue mambo hayo.
Ndugu, Mwanasheria Garatwa.Msajili kwa nia ovu dhidi yetu aliamua kutumia kanuni ya 9(a) ya kanuni ya uchaguzi toleo la 2024 inayohusu uchaguzi wa ndani ya chama kumuengua Mgombea wetu wa Urais kwamba hana Sifa sababu hana siku 7 tangu amejiunga kwenye chama kabla ya mchakato wa uchaguzi kuanza (Ambao mchakato huo ni mchakato wa uchaguzi wa ndani ya chama).
Msajili kwa nia ovu aliamua kutotambua mwongozo wa uteuzi wa 2025 unaohusu mchakato wa kura za maoni na uteuzi ndani ya chama kwa uchaguzi wa kiserikali. Msajili alipaswa kujikita kwenye mwongozo kama ilivyoelezewa ibara ya 71(1)(iii) ya Katiba yetu ya chama toleo la 2024, kuangalia kama Mgombea wa Urais Mh.Luhaga Mpina kama ana Sifa au kama taratibu zilifuatwa kwa mujibu wa Mwongozo wa uteuzi na sio kanuni ya uchaguzi toleo la 2024 ambayo yenyewe inajikita kwenye uchaguzi wa ndani ya chama tuu . Mgombea wetu wa nafasi ya Urais Mh.Luhaga Mpina hana mahusiano na kanuni za uchaguzi za chama.
Ndugu, Mwanasheria Garatwa.Msajili wa vyama vya siasa kwa nia ovu ameamua kudogodesha mwongozo na kuuona haufai sababu tuu hautimizi malengo yake ovu dhidi yetu na Mgombea wetu. Hivyo akaamua kutumia kanuni inayohusu uchaguzi wa ndani ya chama kumuengua Mgombea wetu. Kanuni na Mwongozo zote ni subsidiary legislations au delegated legislations au subordinate legislations au secondary legislations ambazo zote hutengenezwa kwa dhamira ya kuelezea utekelezaji wa mipango,sera na taratibu kwa upana kulingana na Sheria (act ) au katiba.
Na hizi hutengenezwa kwa mujibu wa Sheria (act ) au kwa mujibu wa Katiba. Kama kanuni (regulation) imetengenezwa kwa mujibu wa Katiba haiwezi kuwa na hadhi tofauti na Mwongozo uliotengenezwa kwa mujibu wa Katiba pia. Na huu Mwongozo wetu wa uteuzi katika chaguzi za kiserikali umetengenezwa kwa mujibu wa Katiba ya chama toleo la 2024 ibara ya 71(1)(iii) na ibara ya 108(1).
Ndugu Mwanasheria Garatwa , katika hili hakuna sehemu yeyote ambapo chama chetu kina makosa bali tuu ni hila, hujuma na nia ovu ya Msajili na dola dhidi ya Mgombea wetu na Chama chetu . Lakini pia hata kama kungekuwa na mgongano wowote wa kanuni au mwongozo katiba yetu ya chama toleo la 2024 ibara ya 108(3) inasema "Mgongano wowote utakaotokea baina ya kanuni au mwongozo wa katiba au Sheria na Katiba ya nchi basi ,(i) katiba na Sheria za nchi zitachukua nafasi ya kwanza (ii) Katiba hii ya chama itatamalaki mbele ya kanuni na miongozo ya chama . Bila aibu Msajili akaamua kutamka ya kwamba Mgombea wetu wa nafasi ya Urais hana Sifa ya kugombea.
Ndugu, Mwanasheria Garatwa katika kipindi hiki cha mchakato wa uchaguzi kuanza ,kwa kuzingatia Mgombea wetu Mh.Luhaga Joelson Mpina alikuwa tayari amechukua fomu,amehakiki , amewasilisha mapendekezo ya ratiba ,ametafuta wadhamini na kupewa tarehe ya kurejesha fomu maana yake ni kwamba mamlaka (Mandate) ya Mgombea wetu wa nafasi ya Urais yalikuwa chini ya Tume ya Uchaguzi (INEC) na sio Msajili wa vyama vya siasa.
Msajili wa vyama vya siasa anaingia tuu katika hoja zinazohusu "Gharama za uchaguzi" kifungu cha 36 cha Sheria Na.1 ya Uchaguzi wa Rais , Wabunge na madiwani kinasema "Tume inaweza, katika siku ya uteuzi,
kukataa kumteua mtu kuwa mgombea wa kiti cha Rais iwapo itajiridhisha kuwa mtu huyo ameondolewa sifa
za kushiriki katika mchakato wa uteuzi na Msajili wa vyama vya Siasa kwa mujibu wa masharti ya Sheria
ya Gharama za Uchaguzi " . Sasa suala la Mgombea wetu Mh.Luhaga Joelson Mpina halihusu gharama za uchaguzi.
Lakini pia huyo Msajili wa vyama vya siasa ana fursa ya kuweka pingamizi kwa Tume ya uchaguzi,lakini pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali ana fursa ya kuweka pingamizi dhidi ya Mgombea na Mgombea mwingine ana fursa ya kuweka pingamizi kwa mujibu wa Sheria Na.1 ya uchaguzi wa Rais , Wabunge na madiwani kifungu cha 37(3) na pia kanuni za uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani kanuni ya 22(1),(2).
Hivyo Msajili , Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na wagombea wengine walikuwa na fursa ya kuweka pingamizi dhidi ya Mgombea wetu ,basi Msajili angetumia vyama vingine kuweka pingamizi dhidi ya Mgombea wetu kwa Tume kama ambavyo walimtumia Monalisa kuanzisha hayo malalamiko.
Ndugu Mwanasheria Garatwa,Tume ya uchaguzi (INEC) kwa mujibu wa Katiba yetu ya JMT ya 1977 ibara ya 74(7) inasema " Tume ya Uchaguzi itakuwa ni idara huru inayojitegemea, itafanya maamuzi yake rasmi kuhusu utekelezaji wa majukumu yake kwa vikao" .
Pia ibara ya 74 (11) ya Katiba yetu ya JMT ya 1977 inasema " Katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu ya masharti ya Katiba hii, Tume ya Uchaguzi haitalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu yeyote au idara yoyote ya Serikali, au maoni ya chama chochote cha siasa. Maelezo ya namna hii yapo pia kwenye Sheria Na.2 ya Tume ya uchaguzi ya 2024 kifungu cha 6(1).
Ndugu Mwanasheria Garatwa, jambo la kustaajabisha TUME ya Uchaguzi (INEC) iliamua kufuata maelekezo ya Msajili wa vyama vya siasa kinyume kabisa na Katiba, Sheria na kanuni za uchaguzi. Lakini pia kinyume kabisa na kifungu cha 36 cha Sheria Na.1 ya uchaguzi wa Urais , Wabunge na madiwani ya 2024. Kwa kukiandikia barua chama chetu tarehe 26 /Agosti /2025 jioni siku ile ambayo msajili alitoa maamuzi yake dhidi yetu na Mgombea wetu, Tume ya uchaguzi (INEC) katika barua yao waliamua kumuengua Mgombea wetu kabla ya kurejesha fomu,kabla ya kumsikia (Natural Justice) na kumzuia hata asisogelee geti la Ofisi ya Tume ya uchaguzi -Dodoma.
Ndugu Mwanasheria Garatwa, haya ndiyo maelezo yangu kwako kaka yangu.CCM wanamuogopa Mpina ,CCM haitaki Ushindani,CCM inaogopa vyama makini vya upinzani na ndiyo maana Tundu Lisu yupo ndani ,Mpina kaenguliwa.CCM inakaribia kujifia .
Kesi ipo Mahakamani tusubiri maamuzi ya Mahakama.
Ahsante.
Abdul Omary Nondo.
Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana Taifa-ACT Wazalendo.
29/08/2025.