Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 5,352
- 15,876
Abdul Nondo amezungumza hayo leo Mei 23, 2026 Jijini Dar es Salaam. kwenye Hoteli ya Land Mark Hotel , Riverside Ubungo.
KUFUNGUA MASHTAKA DHIDI YA CLAYTON REVOCATUS CHIPANDO (BABA LEVO) KWA KUNICHAFUA, KUNIDHALILISHA, KUNIVUNJIA HESHIMA, KUTWEZA UTU WANGU NA KUONGEA UONGO DHIDI YANGU.
Ndugu waandishi wa habari ,naomba nianze kwa kutengeneza msingi.Mnakumbuka tarehe 7/Machi/2018,nikiwa mwanafunzi kabisa wa shahada chuo kikuu cha Dar es salaam (UDSM),pia nikiwa mwenyekiti wa taasisi ya utetezi wa wanafunzi Tanzania (Tanzania Students Network Program-TSNP).Nilitekwa Dar es salaam na kutupwa Iringa,Mafinga maeneo ya kiwanda cha Pareto na baadaye kusaidiwa na kufikishwa katika kituo cha Polisi cha Mafinga.Nilihojiwa na kuchukuliwa maelezo juu ya tukio hili la utekwaji dhidi yangu,baada ya dakika 30 kupita niligeuzwa kutoka kuwa mlalamikaji na muhanga wa tukio la utekwaji na kuwa mtuhumiwa wa kusema uongo.Matukio mengine yaliyofuata ni kusimamishwa chuo,na kuambiwa sio Raia wa Tanzania na Idara ya Uhamiaji.
Nikafunguliwa kesi ya jinai namba 13 ya mwaka 2018 na Jamhuri (Criminal Case No.13 of 2018, Republic Versus Abdul Mahmoud Omary Nondo) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Iringa,nikituhumiwa kosa la kutoa taarifa za uongo kwamba nimetekwa ikiwa sio kweli na kwamba nilijiteka na kwenda kwa mpenzi wangu Iringa.Katika mwenendo wa kesi hii,nikitetewa na mawakili wangu Jebra Kambole na Charles Luoga nilitoa ushahidi wangu juu ya tukio lote la kutekwa hadi kufikishwa Mafinga,Iringa na baadaye kituo cha Polisi Mafinga,nilipeleka mashahidi wangu.Polisi na upande wa mwendesha mashtaka nao walihitajika kupeleka ushahidi na mashahidi wao ili kuthibitisha tuhuma zao dhidi yangu kwamba nimejiteka,na wakahitajika waoneshe huyo mpenzi wangu niliyemfuata Iringa.Ila hakuna ushahidi wowote wa maana uliowasilishwa Mahakamani.
Na hivyo,tarehe 05/Novemba /2018 Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa chini ya Hakimu Liad Mohamed Chamshama ikatoa hukumu kwamba nimeshinda kesi na kuniachia huru.Mahakama ilitamka kwamba upande wa mwendesha mashtaka wameshindwa kuthibitisha tuhuma zao dhidi yangu sio tuu katika kiwango cha “Beyond Reasonable Doubt” ambacho ni kiwango cha juu zaidi cha uthibitisho katika kesi za jinai (Criminal Cases) bali hata kile kiwango cha kesi za madai “The balance of Probability“(Uwiano wa uwezekano) wameshindwa kukifikia pia,ambacho ni kiwango cha chini sana katika kuthibitisha kesi za madai(Civil Cases).Mahakama ilisema katika aya ya mwisho ya Hukumu “With the above observations, this court resolves that
the prosecution side has failed to prove the two indictments leveled against the accused even to the balance of probability the principle used in the civil cases, thus hereby acquitted”.
Mapema mwaka 2019, upande wa mwendesha mashtaka wakakata rufaa katika Mahakama Kuu Iringa (High Court) dhidi ya Hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya Iringa iliyonipa ushindi. Hukumu ya Rufaa ya Mahakama kuu chini ya Jaji P.M. KENTE yenye kurasa 26 ilitolewa tarehe 23/Desemba/2019,ambapo pia nilishinda tena kesi hii katika ngazi ya Mahakama kuu kupitia rufaa waliyokata.Katika Hukumu Jaji Kente alirudia maneno yaleyale ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa chini ya Hakimu Liad Mohamed Chamshama kwamba wakata rufaa (waendesha Mashtaka) wameshindwa kuthibitisha sio tuu katika kiwango cha “Beyond Reasonable Doubt” bali hata kile cha“The balance of Probability “ wameshindwa. Anasema Jaji KENTE katika aya ya mwisho katika Hukumu “As the Latin Maxim goes, Nulla Poena Sina Lege, I would for these reasons find, like the learned trial Magistrate, that the appellant’s guilt had not been proved at all leave alone being proved beyond reasonable doubt. I would therefore dismiss this appeal in it’s entirely, as I hereby do.It is so ordered”.Mei 11,2020 Mkurugenzi wa Mashtaka alikata rufaa tena katika mahakama ya Rufani Tanzania,Masjala ya Iringa kupinga maamuzi ya Mahakama kuu(High Court) yaliyonipa ushindi,ambapo Kesi ilipangwa kusikilizwa katika Mahakama ya Rufani Masjala ya Iringa mbele ya majaji wa Rufani watatu ,Jaji Lila,Jaji Kitusi na Jaji Mwampashi tarehe 23/03/2022 ,saa 3:00 Asubuhi,amabayo ilikuwa kesi ya rufaa namba 30 ya mwaka 2020 kati ya Mkurugenzi wa Mashtaka dhidi ya Abdul Mahmoud Omary Nondo.Ilipofika tarehe hiyo 23/03/2022 kabla ya kesi kuanza upande wa mwendesha mashtaka wakawasilisha ombi mahakamani mbele ya majaji kwamba mkurugenzi wa mashtaka nchini (DPP)hana nia ya kuendelea na kesi/Rufaa hiyo kwa mujibu wa kanuni ya 77(4) ya kanuni za mahakama ya Rufani,hivyo Mahakama ya Rufani wakaondoa kesi.
Tukio la pili la utekaji dhidi yangu ,tarehe 1 Desemba.2024 saa 11 Alfajiri katika Stendi ya Mabasi ya Magufuli ,Mbezi Louis ,Jijini Dar es salaam nilitekwa na watu zaidi ya wanne walionivamia kunikaba koromeo kiasi cha kushindwa kupumua na kuniingiza kwenye gari aina ya Landcuiser nyeupe kwa nguvu hadi sehemu nisiyoijua,nikipigwa
,kuteswa na kuumizwa na baadaye kutupwa katika ufukwe wa Cocoa-Beach.Nikasaidiwa na Bodaboda kupelekwa Ofisi ya Makao Makuu ya chama ACT-Wazalendo ,Magomeni majira ya saa 5 usiku na baadaye nikapelekwa Hospital ya Aghakhan kwa matibabu,nikalazwa kwa wiki moja na siku kadhaa. Polisi walitoa taarifa mara kadhaa juu ya tukio la utekwaji dhidi yangu,Polisi walinichukua maelezo nikiwa hospital na wakasema wamefungua jalada la uchunguzi ili kubaini watekaji. Nasikitika kusema hadi sasa hakuna taarifa yeyote ya uchunguzi kubaini walioniteka.
Katika mazingira haya ya maumivu ,hofu, wasiwasi na kutokuwa na majibu yeyote ya uchunguzi kubaini walioniteka mimi ,na walioteka wengine na ambao hawajulikani
walipo hadi sasa.Katika mazingira ambayo matukio ya utekaji bado yanaendelea hadi sasa,katika mazingira ambayo jamii na watanzania tunapambana kutaka mamlaka kuchukua hatua Madhubuti kukomesha matukio ya utekaji nchini.Mtu anayeitwa Clayton Revocatus Chipando (Baba Levo) anapata wapi ujasiri na nguvu ya kunidhihaki,kunichafua na kusambaza uongo dhidi yangu juu ya matukio mawili ya utekaji yalinitokea,akisema sijawahitekwa bali nilijiteka mwenyewe mara mbili na mara ya kwanza nilikutwa kwa mpenzi wangu Iringa na mara ya pili nilidanganya. Clayton Revocatus Chipando (Baba Levo) amekuwa akirudia rudia kauli hizi za uongo mara kwa mara katika majukwaa tofauti na maeneo mbalimbali bila kujali athari yake.
MARA YA KWANZA ALITAMKA KUPITIA CHOMBO CHAKE CHA HABARI CHA
SEVEN MEDIA (SevenMediatz).
Tarehe 06/Julai/2025 Asubuhi katika Ofisi Kuu za Seven Media (Seven Media HQ) Mikocheni ,Jijini Dar es salaam. Clayton Revocatus Chipando (Baba Levo) alitamka maneno haya ya uongo dhidi yangu huku akijua fika maneno hayo ni ya uongo ,alisema “Abdul Nondo ndiyo mtu pekee ambaye ashajiteka mara mbili Abdul Nondo,mara mbili.Muulizeni Abdul Nondo ,mara hizi mara mbili.Anasingizia ,anasingizia kwamba ametekwa mara ya kwanza akagundulika yuko Iringa umenielewa vizur”. Maneno haya yalichapishwa na kusambazwa kupitia chombo chake cha habari kiitwacho Seven Media na baadaye vyombo vingine vya habari.MARA YA PILI ALITAMKA KUPITIA KUNDI LA WHATSAAP LA KIGOMA YETU MPYA.
Tarehe 15/Machi/2026 kwenye kundi la WhatsAp la Kigoma yetu Mpya lenye jumla ya wanachama (Members) 462 ambao ni wananchi, viongozi vyama, vijana,viongozi wa dini ,viongozi wa serikali na watu tofauti. Clayton Revocatus Chipando (Baba Levo) aliandika pia maneno ya uongo dhidi yangu wakati nikiwa katika mjadala na mtu , akasema “Lumenyela unabishana na Mtu Alishawahi kujiteka mara mbili?.MARA YA TATU ALITAMKA KUPITIA CHOMBO CHA HABARI CHA STAR TV.
Tarehe 3/Mei/2026 siku ya Jumamosi saa 3:30 usiku katika Wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam, Clayton Revocatus Chipando (Baba Levo) alifanya mahojiano katika kipindi cha “MEDANI KUU LIVE” kinachoongozwa na mtangazaji Chief Odemba.Kipindi huwa kinarushwa kupitia STAR TV (Mainstream Media). Muandishi Chief Odemba alimuuliza , Clayton Revocatus Chipando (Baba Levo) Kwanini anaamini ya kwamba Abdul Nondo anajiteka mwenyewe na hatekwi?. Clayton Revocatus Chipando (Baba Levo) aliendelea kuongea uongo dhidi yangu akisema “Kwasababu mimi namjua Abdul Nondo anapenda sifa,anapenda atrendi,anapenda apate umaarufu kwa hiyo hayo matukio ni ya watu wanaopenda umaarufu ,anatumia matatizo ambayo watu wengine yanawakuta ya ukweli ,alafu yeye anayabadilisha kwa ajili ya kutengeneza trendi , mimi nazungumzia yeye (Abdul Nondo), sababu yeye ndiyo Jeshi la Polisi lilimkuta Iringa kwa demu
,ninachokizungumzia alijiteka Dar es salaam akaja kujitekua Iringa”.Clayton Revocatus Chipando (Baba Levo) amekuwa akitamka na kusambaza uongo huu mara kwa mara huku akijua maneno haya ni ya uongo,ni maneno yanayoniumiza
,kunichafua na kuondoa heshima yangu katika jamii na umma wa watanzania ,lakini ni maneno yenye dhihaka sio tuu kwangu kama mhanga bali kwa wahanga wengine wa utekaji na ndugu wa wahanga.Pia ni maneno yanayoendelea kudogodesha ukubwa wa matukio ya utekaji nchini ili yaonekane ni matukio ya kutengeneza,maigizo na uongo.Nakutaka kuaminisha umma kwamba matukio hayo hayapo nchini.
Mimi ni mvumilivu sana wa kisiasa ,sio rahisi kuumizwa au kuyumbishwa na maneno ya kisiasa dhidi yangu ,ila haya kwangu sio maneno ya kisiasa ni maneno ya uongo na dhihaka dhidi ya utu wangu,maumivu yangu,machungu yangu na ya wahanga wote wa matukio ya utekaji, ni maneno ya uongo na dhihaka yenye nia ya kurudisha nyuma mjadala wa umma wenye dhamira ya kutafuta suluhu na ukomeshaji wa matukio ya utekaji nchini ,ni maneno ya uongo na dhihaka dhidi usalama wangu pia sababu unavyosambaza uongo dhidi yangu kwamba nina jiteka maana yake unaniweka kwenye hatari zaidi ya Maisha na usalama wangu kwa kutaka umma wa watanzania wanipuuze na wapuuze uhai wangu siku ikitokea tena tukio la utekaji dhidi yangu.
Hivyo basi,nimedhamiria kufungua kesi ya kashfa /udhalilishaji(Defamation Case)Mahakamani na tayari nilimuagiza wakili wangu ,Wakili Msomi Hekima Mwasipu kutoka Matwiga Law Chambers kuanza mchakato wa kufungua mashtaka mara moja dhidi ya Clayton Revocatus Chipando.Tayari mchakato umeanza tarehe 20/Mei/2026 tumemtumia barua (Demand Notice) Clayton Revocatus Chipando (Baba Levo) ya kusudio la kufungua mashtaka dhidi yake baada ya siku saba kama hatotekeleza masharti yafuatayo.
Kuomba radhi kwa umma kupitia vyombo vya habari vikubwa na vyombo vya habari alivyotumia kusambaza uongo,kashfa na udhalilishaji huo dhidi yangu.
Kuahidi umma wa watanzania kwamba hataendelea kusema na kusambaza uongo bali atazingatia ukweli,uaminifu na uhakika katika taarifa zake anazochapisha mitandaoni na vyombo vya habari,na kwamba atajizuia kutumia vibaya nafasi yake ya kisiasa na chombo chake cha habari kwa kuumiza watu kupitia maneno ya uongo,udhalilishaji na kashfa.
Kwamba kutokana na maumivu makubwa aliyonisababishia,heshima na utu wangu kuchafuka katika jamii kutokana na maneno yake ya uongo,ya kashfa na ya udhalilishaji dhidi yangu. Nimemuagiza wakili wangu Hekima Mwasipu amuelekeze Clayton Revocatus Chipando (Baba Levo) kulipa kiasi cha shiling Milioni miatano (Tsh.500,000,000) malipo haya ni matokeo ya tabia yake ya kunichafua,kuniumiza
,kunidhalilisha na kuharibu taswira yangu mbele ya umma kutokana na meneno yake ya uongo dhidi yangu.
Asipotimiza masharti haya matatu ndani ya siku 7 kuanzia jana tarehe 22/Mei/2026 siku aliyopata barua rasmi hadi tarehe 30/Mei/2026, nitafungua mashtaka dhidi yake kupitia Wakili wangu na tutakutana mahakamani.Alete mashahidi na ushahidi wake wa
kuthibitisha mimi kujiteka mara mbili kama anavyonichafua ,kunidhalilisha ,kunivunjia heshima na kutweza utu wangu mbele ya umma wa watanzania kwa kusambaza kauli za uongo dhidi yangu.
Ahsanteni!
Imetolewa na, Abdul Omary Nondo.
23/Mei/2026, Dar es salaam.